ANKO KITIME: Bozi Boziana kanikumbusha mbali sana
Mwanamuziki Mbenzu Ngamboni Bokili maarufu kwa jina la Bozi Boziana alikuwa amekaribishwa nchini kufanya maonyesho kadhaa, taarifa hiyo imenifanya nirudishe kumbukumbu zangu miaka ya 90 wakati Tanzania ilikuwa soko kubwa la maonyesho ya bendi maarufu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Baada ya kila kipindi kifupi bendi maarufu zilialikwa kufanya maonyesho katika miji mbalimbali, na hakika katika maonyesho hayo havikukosekana vituko, na vingi vilitokana hasa na mambo ya fedha.
Kuna wakati Bozi Boziana alikuwa amealikwa na wafanyabiashara fulani na akawa na onyesho Oysterbay Hotel, jirani na ilipo Coco Beach kwa sasa. Wakati huo vyombo vyamuziki vilikuwa vikikodishwa kutoka bendi mbalimbali, katika onyesho hilo la Boziana, vyombo vilivyotumika vilikuwa ni vya Vijana Jazz Band.
Kwa kawaida wakodishaji walitanguliza nusu ya bei ya kukodisha na mara nyingi makubaliano yalikuwa kukamilisha fedha iliyobaki kabla ya kuisha kwa onyesho. Malipo yalitegemea makusanyo kwenye mauzo ya tiketi.
Siku hiyo kila kitu kilianza vizuri lakini muda wa kumaliza onyesho ulikuwa unakaribia watayarishaji wakawa hawaonyeshi dalili zozote za kulipa salio. Fundi mitambo alikuwa amepewa maagizo kuwa ikionekana kuna dalili ya kudhulumiwa fedha, aanze kunyofoa nyaya katikati ya onyesho.
Kama alivyoagizwa, fundi yule tuliyezoea kumuita Selemani Kidevu, akaanza kunyofoa waya mmoja mmoja watayarishaji haraka wakalazimika kulipa fedha zilizobakia kabla onyesho halijaharibiwa.
Kituko ambacho sitakisahau, kilitokea baada ya wafanya biashara wawili kwa pamoja walipomkaribisha Diblo Dibala na kundi lake. Diblo alikuja na bendi nzima akiambatana na wacheza shoo. Bendi ilifanya ziara mikoa ya nyanda za juu kusini na kuambatana na mmoja wa wafanyabiashara.
Wanamuziki wakarudi Dar es Salaam na kupokelewa na mfanyabiashara wa pili aliyeweza kuingia nao mkataba wa haraka haraka wafanye onyesho moja katika ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa jinsi mambo yalivyokwenda ni wazi yule mfanyabiashara wa kwanza aliyekuwa bado mkoani, alikuwa hana habari ya onyesho hilo jipya.
Makubaliano yalikuywa Diblo alipwe fedha zake kamili kabla ya kupanda jukwaani. Mfanyabiashara yule alikuja Vijana Jazz Band, wakati huo na mimi nikiwa mwanamuziki akiwa na nia ya kukodi vyombo. Kutokana na kilichotokea wakati wa onyesho la Bozi Boziana, katibu wetu wa bendi Rashid Pembe alimwambia ni lazima alipe fedha yote kabla ya kuondoka na vyombo.
Mheshimiwa yule hakuwa na fedha wakati ule na ilikuwa kama saa tisa mchana, akaahidi angerudi na fedha, lakini mpaka jua linatua hakuonekana tukaagana na kurudi makwetu tukijua biashara hiyo haipo tena.
Kule Chuo Kikuu tiketi zilianza kuuzwa mchana na hakika watu wengi walinunua tiketi.
Nikiwa tayari nimejitayarisha kulala kama saa tatu na nusu usiku, niligongewa mlango na Rashid Pembe, wakati huo nilikuwa naishi Mwananyamala Kamanyola, Pembe akaniambia, ‘E bwana ee yule jamaa wa mchana ameenda ofisini na amepewa kibali cha kuchukua vyombo atalipa kesho’. Nikamuuliza Pembe, ‘Mbona saa hizi amechelewa sana?’ Pembe akanambia vyombo tayari vimo kwenye gari, na mimi tu nasubiriwa, kinachotakiwa twende kuvifunga ukumbini.
Nilipofika kwenye gari nikamkuta mwanamuziki mwingine wa Vijana Jazz Band, Shomari Ally nae yupo, tukaanza safari ya kwenda Chuo Kikuu. Tulipofika na vyombo hali ilikuwa tete, wanafunzi waliokwishalipia kiingilio toka mchana walikuwa tayari wameanza kukasirika kuwa wametapeliwa, hivyo tulipokewa kwa matusi na kejeli. Kufikia kama saa tano ya usiku tulikuwa tumeweza kufunga vyombo, shida ikawa hakukuwa na dalili ya wanamuziki. Mbaya zaidi, yule mfanyabiashara alikuwa amewahi chuoni na kukusanya fedha zote za viingilio aliingia mitini, hivyo waliokuwa wamekata tama wakawa hawana mahala pa kurudishiwa fedha zao, hali ilikuwa tete.
Kumbe wakati huohuo mfanyabiashara yule pia alikuwa na mgogoro na Dally Kimoko ambaye alikuwa anataka fedha yake kabla ya kuondoka hotelini kama walivyokuwa wameahidiana. Inaonekana mfanya biashara yule alimpa lugha laini na kumuahidi kumlipa mara watakapofika ukumbini.
Saa sita hivi wanamuziki wakaingia, bila Dally Kimoko. Wakakaribishwa na matusi mengi, lakini wakaweza kutayarisha vyombo wakawa wanamngoja kiongozi wao. Dally Kimoko na wacheza shoo walifika eneo la ukumbi kama muda huohuo lakini wakawa wamebaki kwenye gari dogo aina ya Benz nyuma ya ukumbi wakisubiri kulipwa kwanza, mlipaji alikuwa kayeyeyuka.
Fujo ikaanza nje pale wanafunzi walipogundua kuwa Dally Kimoko yumo kwenye gari na hataki kutoka, wanafunzi wakambeba Dally Kimoko juu juu toka kwenye gari lake ambalo wakati huo walikuwa wameshalitoa upepo na hata kukwangua rangi, wakambeba mpaka jukwaani.
Katika hekaheka hizo wacheza shoo wakaibiwa nguo zao, za kazi, effects za gitaa la Dally Kimoko na hata passports. Jitihada za kubembeleza vitu hivyo virudishwe hazikusikilizwa. Ukumbi ulijaa kelele za wanafunzi wakisema, ‘Piga au hutoki humu’ ilikuwa inatisha.
Microphone kadhaa za bendi zikanyofolewa na waliozinyofoa kukimbia nazo, ilikuwa mbaya. Dally Kimoko akalazimika kupiga nyimbo za papo kwa papo kupunguza mzuka, wakati huo ilikuwa kama saa nane usiku. Sikumbuki aliyepata wazo la kwenda kwenye kituo cha polisi cha pale chuoni, na hatimae wanamuziki wale wakapata msaada kurudi hotelini kwao na sisi tukafunga vyombo vyetu, baadae tukakesha kituoni tukitoa ripoti ya upande wetu.