Prime
Shoo za kale, za sasa na utofauti uliopo
Unapoamua kuzungumzia burudani hasa ya muziki basi hakika huwezi kuacha kutaja shoo ambazo zimekuwa zikifanywa na wasanii kwenye mikoa mbalimbali hapa nchini kwetu, mara nyingi shoo hizo ndizo ambazo zinamkutanisha msanii na mashabiki wake na humsaidia msanii kuweza kufahamu ni jinsi gani muziki wake unakubalika na ni vipi aongeze bidii kwenye kazi yake ili aendelee kuwa na mashabiki wake kila anapokuwa anatoa kazi mpya.
Kipindi cha miaka ya hivi karibuni kama mitano nyuma zimefanyika shoo nyingi sana ambazo kila moja imejiwekea rekodi yake ya kipekee kutokana na mpangilio wa matukio ambayo yamekuwa na ubunifu wa hali ya juu na kufanya mashabiki kuvutiwa na shoo hizo kila zinapotokea kwenye eneo husika, na kufanya umati kuwa mkubwa jambo ambalo linafanya sanaa kuwa kubwa kadri siku zinavyokwenda na muziki wetu kufika mbali zaidi kimataifa.
Turudi nyuma kidogo miaka kama 10 iliyopita ambapo kulikuwa na matamasha machache ukilinganisha na ya sasa ambapo wasanii walikuwa wakifanya shoo kwenye mkoa fulani basi ni lazima waweke rekodi ya kipekee kutokana na kutofika mikoani humo mara kwa mara, tofauti na sasa msanii hata yeye mwenyewe akiamua kwenda kufanya shoo mkoa wowote anaenda tu, zamani matamasha yaliyokuwa yakifanywa mikoani yalikuwa yakiacha historia ambayo mara nyingi huwa haijirudii kutokana na ubunifu uliokuwa ukitumika ni wa kipekee sana na wasanii hao walikuwa na nyimbo ambazo zilikuwa zikigusa watu wa rika zote.
UTOFAUTI ULIOPO
Utofauti uliopo kati ya shoo za miaka ya nyuma na sasa ni kutokana na kwamba hivi sasa kuna aina nyingi sana za muziki na asilimia kubwa ya wahusika wa aina hizo ni vijana wenye rika la kuanzia miaka 18 mpaka 35, muziki wa miaka ya nyuma shoo zake ambazo zilikuwa zikiandaliwa na wadau mbalimbali wa muziki walikuwa wakishirikiana na wasanii kwenye kuaandaa maudhui ya kupeleka kwa mashabiki wao ili shoo iwe nzuri jambo ambalo kwa sasa ni mara chache kutokea hilo.
SHOO ZA SASA
Mfano mzuri sasa hivi kuna matamasha mawili yanayotajwa kuwa makubwa kwa hapa nchini kwetu kutokana na ushindani uliopo kwenye muziki, matamasha hayo ni Fiesta pamoja na Wasafi Festival yanayoendeshwa na vyombo va habari vya Couds Media na Wasafi Media.
Kwa upande wa matamasha haya mawili tunaona ni jinsi gani kila mmoja anapambana kufanya sanaa yake ionekane bora zaidi hasa kwa matamasha haya yaliyofanyika mwaka 2024 ambapo kulikuwa na mvutano mkubwa wa nani atajaza kuliko mwenzake na nani atafanya shoo kali kuliko mwenzake, lakini mwisho wa siku wote walifanya shoo nzuri ambazo kila moja ilikuwa ikibebwa na vionjo vyake binafsi kuanzia mpangilio wa wasanii na mpaka vifaa vilivyotumika stejini. Kwa upande wa Fiesta waliamua kutumia vyombo zaidi tofauti na ilivyokuwa kwa Wasafi.
WASAFI 2019
Tamasha lilifanyika Jumamosi ya Novemba 9, likikusanya wasanii wa sasa na wa zamani ambao ni Profesa Jay, Ferooz, TMK Wanaume wakiongozwa na Mh.Temba, Juma Nature, Madee na Tiptop Conection, Z anto, Lava Lava, Mbosso, Rayvanny, Juma Jux, Inspekta Haroun, Mandojo na Domo Kaya na wengine kibao ambapo kulikuwa na wasanii wageni wane, wawili wakitokea nchini Nigeria ambao ni Wizkid na Tiwa Savage mmoja kutokea nchini Congo anayefahamika kama Inno’s B. Mwingine Meddy kutoka Rwanda
Tamasha hilo lilikwenda mpaka saa 10:15 alfajiri ambapo watu walionyesha kupendezwa na mpangilio mzuri wa wasanii na matukio mfano wakati wa Madee ambaye aliingia kisha kuwapandisha wasanii ambao wamekuwa kimya kwenye gemu kwa muda mrefu sasa ambao ni Pingu na Denso, Z. Anto ambao walisepa na kijiji kutokana na kuamsha hisia za mashabiki wengi sana jukwaani hapo mpaka wageni wenyewe waliona kuwa ni jinsi gani muziki wetu una thamani hasa pale walipokuwa wanapanda watu wa muziki wa zamani.
FIESTA 2019
Tamasha lilifanyika Jumapili ya Desemba 8 kuamkia Desemba 9, ambalo lilikusanya wasanii wa sasa na wa zamani ambao ni Harmonize, Ali Kiba, Profesa Jay, Chege, Dogo Janja, Juma Nature, Whozu, Maua Sama, Weusi, Mimi Mars, Mandojo na Domo Kaya na wengine kibao ambapo kulikuwa na shoo ya aina yake.
Tamasha hilo lilikwenda mpaka saa 12 asubuhi ambapo watu walionyesha kupendezwa na mpangilio mzuri wa wasanii waliofanya shoo kuanzia majira ya saa 5 usiku na kuendelea kusepa na kijiji kutokana na kuamsha hisia za mashabiki wengi sana jukwaani hapo.
Shoo ilianza kuvutia ilipofika saa 5:15 usiku baada ya kupanda Young Lunya huku akipafomu wimbo wake alioupa jina la Freestyle Session 2 kisha akawakaribisha wenzake ambao kwa pamoja wanafanya muziki wa aina ya New School Rap ambao ni Country Boy na Kachi ambapo walifuatiwa na Profesa Jay ambaye aliamsha umati kwa wimbo wake wa Zali la Mentali aliomshirikisha Juma Nature kisha akaimba wimbo wake alioupa jina la piga makofi ambapo aliweza kuwakumbusha watu enzi zile wakati muziki unaanza kuteka hisia za watu na kumaliza na wimbo wake wa Hapo Vipi.
Yalipofika majira ya saa 10 alfajiri alipanda Harmonize ambaye alikuwa akisubiriwa kwa hamu sana na watu kwani ni mara yake ya kwanza kupafomu kwenye jukwa la Fiesta tangu aanze kuwika kwenye soko la muziki ndani na nje ya Tanzania.
Ukiacha matamasha hayo makubwa mawili pia kuna baadhi ya Taasisi mbalimbali zimekuwa zikijitahidi kuandaa matamasha yao binafsi kwa kushirikiana na taasisi zingine ili kuweza kuleta ile ladha ya burudani kutoka majukwaani moja kwa moja tena mara nyingine wamekuwa wakienda mbali zaidi mpaka kualika wasanii wa mataifa mengine kuja kutumbuiza hapa nchini kwetu.
Mwaka 2024 ni moja kati ya miaka ambayo tulishuhudia wasanii mbalimbali wakija Tanzania kwa ajili ya matamasha hayo kama vile Uncle Waffles kutoka Afrika Kusini, Sean Paul (Jamaica), Daliwonga, Toss na Pcee kutoka (Afrika Kusini), Ruger kutoka Nigeria na wengine wengi.
Jambo hili linapelekea kuitangaza nchi yetu hasa kwenye upande wa burudani kwani taasisi kubwa za kimuziki duniani zinapoona juhudi kama hizo na mapokezi mazuri wanayopata wasanii hao wanapokuja nchini kwetu basi moja kwa moja zinaweza kuangalia ni namna gani wanaweza kujihusisha na matamasha hapa kwetu pia kuleta fursa kwa wanamuziki wetu wazawa kuonekana kimataifa zaidi.