Anko Kitime: Nyimbo za asili za watoto zinapotea
Muktasari:
- Mijini na vijijini kulikuwa na nyimbo maalumu za watoto kuanzia watoto wachanga, mpaka wakubwa. Kulikuwa na nyimbo ambazo kina mama walikuwa na wakiwaimbia watoto wao wachanga ili kuwatuliza kama walikuwa wakilia au kuonekana kuwa na wasiwasi fulani.
Dar es Salaam. Kama makala zilizopita zilivyoeleza muziki una mambo mengi sana ndani yake, leo niongelee aina nyingine ya muziki. Kuna aina hii ya muziki ambayo itapotea moja kwa moja ikiwa hatua za makusudi zisipochukuliwa. Huu ni muziki asili wa watoto.
Mijini na vijijini kulikuwa na nyimbo maalumu za watoto kuanzia watoto wachanga, mpaka wakubwa. Kulikuwa na nyimbo ambazo kina mama walikuwa na wakiwaimbia watoto wao wachanga ili kuwatuliza kama walikuwa wakilia au kuonekana kuwa na wasiwasi fulani.
Siku hizi kazi hiyo hufanywa na nyimbo kutoka kwenye simu janja. Watoto huwekewa nyimbo za Kiingereza kama vile Baa Baa Black Sheep au Twinle twinkle little star na nyingine za aina yake ili huwabembeleza na hatimae kulala usingizi. Mtoto anaanza kujengewa upenzi wa utamaduni mwingine wakati akili yake inaanza kukua.
Nyimbo ambazo watoto walikuwa wakiimba huku wakicheza kwenye mwanga wa mbalamwezi, nyimbo kama Ukuti Ukuti, zinapotea taratibu. Si ajabu kabisa kuhudhuria mahafali ya shule za chekechea na kukuta watoto wakiimba vizuri sana nyimbo za watoto za mataifa mengine huku wakishangiliwa na wazazi wao wakifurahia na kuona hiyo ndio elimu bora.
Katika vipindi vya redio na luninga ambavo ni maalumu kwa watoto si ajabu kabisa watoto wadogo wakawa wanashindanishwa kuimba nyimbo za wasanii maarufu wakubwa, nyimbo ambazo hazikutungwa kwa ajili ya watoto wadogo.
Miaka kadhaa iliyopita, kulikuwa na biashara ya kukaribisha vikundi vya ngoma kutoka Botswana vikiwa na mtindo wao ulioitwa Amakirikiri. Ghafla ikawa ngoma ya Makirikiri inafundishwa hata kwenye vituo vya watoto wadogo. Kama vile kukubali kuwa hakuna ngoma za asili za nchi yetu au kukubali kuwa ngoma za asili za nchi nyingine ni bora kuliko ngoma yoyote ya asili ya nchini kwetu.
Kila kabila lina nyimbo za watoto, hata watoto waliozaliwa na kukulia mijini pia walikuwa na nyimbo zao nyingi tu.
Kilimanjaro Band waliwahi kuurekodi wimbo ulioitwa Ndembele, wimbo huu ni wimbo wa Kinyamwezi ambao ulikuwa ukitumika kuwaimbia watoto, Mr Nice aliwahi kufanya kazi nzuri ya kuchukua nyimbo za watoto na kuzibadili kuwa za Bongofleva.
Album yake yenye wimbo ‘Kuku kapanda baiskeli’ ni kati ya mkusanyiko wa nyimbo za watoto uliokuja kupata umaarufu kila kona nchini na hata katika nchi jirani.
Sitasahau mwanzo mwa miaka ya 2000 nilipohudhuria mashindano ya urembo katika mji wa Blantyre huko Malawi, na kuusikia wimbo wa Kuku kapanda baiskeli ukiwa kama wimbo wa kuwaongoza walimbwende kupita mbele ya majaji.
Nyimbo za asili za watoto, wenye umri mkubwa kidogo zilikuwa ni burudani kwa watoto lakini wakati huohuo zikawa zinajenga watoto kujitambua wao ni akina nani. Nyimbo hizi mara nyingine zilikuwa ni hadithi au mara nyingine ni nyimbo zilizokuwa zikisindikiza hadithi. Nyingi zilikuwa na mafunzo makubwa ndani yake. Kikubwa zaidi nyimbo hizi zilijenga misingi ya utamaduni na maadili yao.
Katika nchi ambazo mfumo wa kulinda utamaduni umewekwa kuanzia utotoni, matokeo yake utayaona. Tungo za wanamuziki hawa, mizizi ya muziki wao wa kibiashara una utambulisho wa kwao. Hata namna ya uchezaji wa nyimbo zao hutokana na uchezaji wa asili wa ngoma za kwao.
Matokeo ya kukosekana kwa mizizi ya muziki asili, yanaonekana kwa wanamuziki wetu. Wanamuziki wetu wenye vipaji vikubwa sana, wanalazimika kutunga nyimbo zao kwa kuiga mitindo ya nyimbo za asili za kutoka nchi nyingine.
Tuna wanamuziki wazuri sana ambao kama aungekuwa hujui Kiswahili ungedhani ni wanamuziki wa Afrika ya Kusini wakiimba na kupiga muziki wa kikwao, na vivyo hivyo kwa wanamuziki wanaoiga muziki kutoka Nigeria au Kongo.
Tatizo hilo si kwanamuziki pekee, hata wapenzi wa muziki ambao hawajawahi kupata malezi ya kusikia muziki asili wa kwao, nao hufurahia muziki huo wa kigeni bila kuona ukakasi wowote.
Utamaduni si jambo la kulichukulia kirahisi hasa katika zama hizi ambazo hutambuliwa kama ‘dunia ni kijiji’.
Taifa lisilolinda kwa nguvu utamaduni wake teknolojia itaingiza utamaduni mpya tena kwa nguvu kubwa. Kuna kila sababu ya kurudisha masomo ya sanaa kwa nguvu sana katika shule za awali na msingi. Masomo yaliuyopangiliwa vizuri yatakomaza uzalendo na kutengeneza wasanii wazuri watakaolinda Utanzania.