Billnass awatupia jiwe wasanii wanaoogopa ndoa
Muktasari:
- Hayo ameyasema wakati akizungumza na Mwananchi na kuongezea kuwa msanii kuoa siyo kikwazo cha kushindwa kufanya vizuri kwenye muziki
Dar es Salaam. Mwanamuziki William Lyimo 'Billnass' ambaye anatamba na wimbo wa 'Magetoni' amesema ameamua kutoka kwenye Amapiano na kurudi kwenye aina ya muziki uliomtambulisha kwa mashabiki.
Hayo ameyasema wakati akizungumza na Mwananchi na kuongezea kuwa msanii kuoa siyo kikwazo cha kushindwa kufanya vizuri kwenye muziki
"Kwangu sidhani kama kuna haja ya kuwa muoga kwenye hili, sababu hilo jambo ni wajibu kulitimiza, sasa hayo mambo ya kuoa ndiyo mwisho wa muziki, sio kweli ni vile tu mtu atakavyojiwekea mikakati yake,"amesema.
Amesema mkewe hayupo kama watu wengi wanavyodai kwenye mitandao kuwa ni mkorofi.
"Tatizo wanaosema hivyo hawajawahi kukaa naye na wengine hawamjui zaidi ya kumuona mitandaoni, ila ni kwamba Nandy ni mwanamke ambaye hapendi mambo ya ugomvi kabisa.
"Sijawahi kumpiga na hata sitawahi kumpiga Nandy na kitu ambacho nimeumbwa ni kutogombana na mwanamke au kumpiga mwanamke, nawaheshimu sana wanawake,"amesema Nenga.
Amesema wao kufanya kazi zinazofanana hakuwapi ugumu wowote kwani tayari wamewekeana misingi hivyo ni rahisi kwao kufanya mambo mengi bila tatizo.
Hata hivyo, mwanamuziki huyo amesema kuna muda ukifika ataachana na muziki na kuwekeza nguvu zaidi kwenye biashara.