Diamond, Ziiki hapatoshi, wadau washauri

Muktasari:

  • Diamond acharuka awatuhumu ziiki kuwahujumu katika tasnia ya muziki kwa kukataa kutoa wimbo wa msanii wa kebo yake, Ziiki yakanusha yadai utaratibu haujafuatwa

Dar es Salaam. Hali haikuwa shwari katika kiwanda cha burudani, leo Ijumaa Aprili 19, 2024 baada ya msanii Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz kuituhumu kampuni ya usambazaji muziki ya Ziiki kuzuia utolewaji wa wimbo mpya wa msanii wa lebo hiyo. 

Diamond ametoa lawama hizo kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram katika kipengele cha insta story akiituhumu kampuni hiyo kuzuia utolewaji wa wimbo mpya wa msanii wa lebo yake ya Wasafi, Lavalava ambayo baadaye ilijibu.


                       

Diamond ameandika "Ni masikitiko kuona kampuni ya Ziiki inauzuia wimbo wa Lavalava Kibango, kutoka siku ya leo na kulazimisha kutoa tarehe wanayotaka wao tena mwezi ujao pasipo sababu ya msingi.

"Ziiki wameahidi kwamba endapo leo tutapandisha wimbo wa Lavalava Kibango wataushusha kila platform na kuhakikisha watu hawaupati popote," ameandika Diamond.

Saa chache tangu Diamond aandike tuhuma hizo, kampuni hiyo kupitia ukurasa wake wa Instagram ilitoa taarifa ya kufafanua kilichoelezwa na msanii huyo huku wakidai tatizo ni lebo hiyo imekiuka masharti ya kuwasilisha wimbo mpya.

“Taarifa ya kuachiwa kwa wimbo huo tumeipokea tofauti na tulivyokubaliana ambapo kimkataba msanii anapaswa kuwasilisha wimbo walau wiki tatu kabla ya wimbo kutoka au kukiwa na sababu zilizo nje ya uwezo wao tunaweza kumpatia walau siku saba iuli wimbo uweze kutoka.

“Wimbo unaolalamikiwa wa Kibango uliwasilishwa siku ya tarehe Aprili 16, 2024, na kutaka kutolewa siku ya Aprili 19 ambapo kwa hali ya kawaida ipo nje kabisa na utaratibu uliokuwa umepangwa,”imeeleza taarifa hiyo.

Pia wameeleza kila mara wamekuwa wakiwaelewesha wasanii wengi hasa kutoka Tanzania juu ya utoaji kazi kwenye Digital Platforms zote. Hivyo basi wamekanusha taarifa za kuzuia wimbo huo kama ilivyoelezwa na msanii huyo.

Wadau waeleza tatizo
Akizungumzia suala hilo Jacob Mhina ‘Dj Cobo’ amesema kuwa kwa ulimwengu wa sasa wa teknolojia ili kuepusha lawama hizo hakuna ulazima wowote wa msanii kutegemea kampuni za usambazaji muziki.

"Sio lazima kuna wasanii wengi tu wanasambaza wenyewe bila kutegemea kampuni na kazi zinakwenda". Amesema Dj Cobo

Pia kwa upande wake Happy Ibrahim ambaye pia ni mdau wa muziki amesema siyo lazima wasanii wategemee kwa wasambazaji muziki .

“Binafsi yangu naona kwamba wasanii wanaweza kuishi bila kutegemea wasambazaji muziki lakini matokeo yake hayawezi kuwa kama wanavyopata kwa wasambazaji.

“Kama unaweza kuuza pekeyako ina maana unachopata una kula mwenyewe ila kwa wasambazaji utachopata utagawana faida iliyopo. Kwa wasambazaji ni kwamba wana nguvu kubwa ya matangazo na kila kitu, ukiwa pekeyako ni ngumu kuwa na matangazo,” amesema Happy

Aidha mdau mwingine, Peter Minja amesema wasanii waache uvivu wa kutegemea jukwaa za kuuza na kusambaza muziki bali wabuni mbinu mpya na binafsi zinazoweza kuwasaidia kusambaza kazi zao kwa uhakika lakini pia kuwanufaisha kwa kile wanachowekeza kwenye kazi zao. 

“Hadi msanii unatambua kuwa anaibiwa asilimia za malipo yake tayari anauelewa na anafahamu baadhi ya taratibu zinazofanyika kwenye kuuza na kusambaza muziki wake, hivyo anapaswa kutafuta watu wake ili awape kazi ya kusambaza kazi zake kwa uhakika maana kampuni ambazo tayari zina majina makubwa lazima zitakuwa zinaangalia zaidi faida kwao kwenye uendeshaji kuliko kumnufaisha mwanamuziki,”amesema Minja.

Mbali na Diamond, mwaka 2023, Harmonize pia amewahi kuwatuhumu Ziiki kutomlipa fedha zake jambo lililopelekea aombe msaada wa kupata haki serikalini, pia Agosti 2022 mwanamuziki Vanessa Mdee kupitia ukurasa wake wa Instagram aliitolea uvivu Ziiki kwa kutaka alipwe fedha zake.

Ziiki waliwahi kujibu tuhuma
Kutokana na lawama kutoka kwa Harmonize, Meneja wa kampuni ya Ziiki, Camilla Owora alikanusha kutomlipa msanii huyo fedha zake na kueleza kila msanii ana kiasi cha fedha ambacho anatakiwa kufikisha kwa mwezi ndiyo alipwe kwa hiyo kwa upande wa Harmonize amekuwa akiitwa kila mwezi na alikataa kusaini invoice.