Frida aweka historia kwenye Kongamano la Kimataifa la Vijana na Hip-hop

Muktasari:

  • Kongamano lililoleta pamoja vijana kutoka kote ulimwenguni lilifanyika Jumamosi, Mei 18, 2024.

Rapa na mtangazaji, Frida Amani ameweka historia ya kuwa msanii wa kwanza kushiriki katika mkutano maarufu wa kimataifa wa NEXT, ulioandaliwa na kituo cha utangazaji cha Uturuki, ‘Turkey Radio na Televisheni (TRT)’.

Kongamano lililoleta pamoja vijana kutoka kote ulimwenguni lilifanyika Jumamosi, Mei 18, 2024.

Akizungumza kuhisiana na mchango wake kwenye tasnia ya muziki Frida Amani anaeleza, “Hip-hop imenipa jukwaa la kufikisha kile ninachotaka kuwasiliana na jamii, bila kujali kama kinapendwa au laaa!, kilicho muhimu zaidi ni kuhakikisha ujumbe unakuwa na matokeo.”

Pia aliangazia jinsi muziki wa hip-hop unavyoweza kuchochea mabadiliko ya jamii na kuhamasisha watu wenye talanta kuongeza uwezo wao kwa mabadiliko chanya, pamoja na kuvunja vizuizi vya kitamaduni.

“Kushiriki katika kongamano hili la vijana kumekuwa chachu ya kunitajirisha, kwani nimepata maarifa na maarifa ya thamani nina imani kwamba nitatumia yale niliyojifunza kwa manufaa ya vijana wa Tanzania, kuleta mabadiliko chanya katika jamii yetu.”

Katika jukwaa hilo liliwakilishwa na nchi mbalimbali za Afrika, zikiwemo Tanzania, Somalia, Nigeria na Afrika Kusini, kwa lengo la msingi la kukuza maono ya pamoja ya kile kilicho mbele na majukumu ya vijana katika kila nyanja.

Mbali na Frida Amani kulikuwa na mcheshi kutoka Nigeria Maryam Apaokagi-Greene, anayejulikana zaidi kama Taaooma, na msanii wa Palestina Malak Mattar.

Watatu hao walichangia mjadala kuhusu jinsi Sanaa na Utamaduni unavyoweza kuleta mabadiliko katika jamii.