Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

G Nako kuanzia Nako2Nako, Weusi hadi WCB Wasafi

Muktasari:

  • Alitambulika na wengi kupitia kundi la hip hop kutokea Arusha, Nako 2 Nako Soldiers. Baadaye akaibuka na Weusi na sasa anaachia mapini tu akishirikiana na baadhi ya wasanii wa WCB Wasafi - moja ya chapa kubwa katika muziki Tanzania.

Dar es Salaam. Kati  ya wanamuziki Bongo wanaojua kubadilika kuendana na wakati, basi ni huyu G Nako a.k.a Warawara, The Kankara, The Finest of AR. mwamba anajua kipi mashabiki wanataka kwa wakati gani na mwisho wa siku itakuwa na faida gani kwake.

Alitambulika na wengi kupitia kundi la hip hop kutokea Arusha, Nako 2 Nako Soldiers. Baadaye akaibuka na Weusi na sasa anaachia mapini tu akishirikiana na baadhi ya wasanii wa WCB Wasafi - moja ya chapa kubwa katika muziki Tanzania.

Ni wiki hii tu G Nako ameachia wimbo mpya, Hapo (2025) akimshirikisha Zuchu, mwanamuziki wa saba na wa pili wa kike kusainiwa na WCB Wasafi - rekodi lebo ya Diamond Platnumz ambayo ilianza kazi miaka 10 iliyopita.

Kolabo hii na Zuchu - mshindi mara saba wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), ni mwendelezo wa G Nako kuubadilisha muziki na chapa yake kwa ujumla ili kuzidi kuwepo masikioni mwa mashabiki wengi, lakini ebu tutazame safari yake kabla ya kufikia hapa.


Warawara & Nako 2 Nako Soldiers

Kundi hilo liliundwa na wasanii wengi, ila wale waliowakilisha zaidi ni wanne ambao ni G Nako, Bou Nako, Ibra Da Hustler na Lord Eyes au Eyez Nako, huku wakitoa albamu moja - Hawahemi Streets Hustler (2007).

Hata hivyo, kabla ya Warawara (G Nako) kujiunga na Nako 2 Nako, yeye na mwenzake Bou Nako walikuwa na kundi lao - Chronic Mob - ambalo walilianzisha kipindi wanasoma Nangwa Technical Manyara ingawa kazi zao hazikupata kusikika.

Kipindi cha mwanzo katika muziki, G Nako bado alikuwa anafanya kazi ya kuongoza watalii katika mbuga za wanyama, hivyo alikuwa anasubiri hadi likizo ndio aungane na wenzake kurekodi au kufanya shoo kabla ya kuacha kazi hiyo na kujikita rasmi katika muziki.

Wakiwa kama kundi, Nako 2 Nako walifanya vizuri kupitia nyimbo zao nyingi - baadhi ya hizo ni Ndio Zetu Kuwakilisha (2005), Bang (2008), Mchizi Wangu (2008) na Hawatuwezi (2008) uliotengenezwa Bongo Records na P-Funk Majani, mshindi wa TMA mara tatu.


Warawara & Weusi

Kufuatia kuvunjika kundi la Nako 2 Nako Soldiers, G Nako na Lord Eyes walijiunga na Joh Makini, Bonta na Nikki wa Pili kutokea kundi la River Camp, kisha kuanzisha kundi la Weusi ambalo hadi sasa limetoa albamu moja, Air Weusi (2021) yenye nyimbo 14.

Wimbo wa kwanza kuwapatia mafanikio Weusi ni Gere (2013) uliojumuisha wasanii watatu, G Nako, Nikki wa Pili na Joh Makini, ni wimbo uliowafanya kushinda tuzo mbili za TMA 2014 kama Wimbo Bora wa Hip Hop na Kundi Bora la Mwaka.

Hata hivyo, mtayarishaji wa wimbo huo kutoka studio za The Industry, Nahreel hakuamini iwapo G Nako anaweza kufanya vizuri kwenye 'Gere' wakati wakirekodi kutokana na aina yake ya muziki ila ulipotoka tu, ukawapatia mafanikio makubwa ambayo hadi wanajivunia.

Wakiwa wamefanya kazi pamoja kwa miaka zaidi ya 10 sasa, kwa kipindi chote ni wasanii wawili tu ambao hawajawahi kukosekana kwenye wimbo wowote wa kundi la Weusi, nao ni G Nako na Joh Makini, rapa aliyetoka na albamu yake, Zamu Yangu (2007) chini ya Madungu Digital - Dunga.


Warawara & WCB Wasafi

Baada ya kutamba sana na Hip Hop na aina nyingine za muziki kama Afrobeats, G Nako naye aliamua kugeukiwa upepo wa Amapiano, muziki ulioanzia huko Soweto, Johannesburg na Pretoria nchini Afrika Kusini katikati mwa miaka ya 2010.

Ngoma ya Amapiano kutoka kwa G Nako iliyofanya vizuri zaidi hadi sasa ni ile aliyomshirikisha Mkurugenzi Mtendaji wa WCB Wasafi, Diamond Platnumz, Komando (2023) ambayo video yake imeshatazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 10 ikiwa ni ya kwanza kwa Warawara kufanya hivyo.

Wimbo huo uliotengenezwa na S2kizzy kutokea studio za Pluto Republic, ulifanya vizuri kiasi kwamba staa wa Nigeria na mwanamuziki wa kwanza wa kike Afrika kushinda MTV EMAs, Tiwa Savage alionyesha kukoshwa nao na kuuliza nani kaimba, kumbe ni Warawara.

Hivyo pia tutarajie wimbo huu mpya na Zuchu, Hapa (2025), nao utaongeza kitu katika safari ya G Nako ila kuna wasiwasi sehemu, nao ni tabia ya Zuchu kutofanya video za wasanii wanaomshirikisha kutoka nje ya WCB Wasafi, hilo limejionyesha katika kolabo zake na Jux (Nidhibiti - 2022 ), Darassa (Romeo - 2024) na Whozu (Attention - 2024).