Hamisa Mobetto hapoi, wala haboi mtandoani!

Muktasari:
- Kati ya watu bilioni 2.4, milioni 11.5 ni mashabiki wa Hamisa Mobetto
Kama ilivyotarajiwa, hatimaye Hamisa Mobetto amempiku Wema Sepetu katika orodha ya mastaa wa kike Bongo wenye wafuasi wengi Instagram ikiwa ni miaka 12 tangu alipojiunga na mtandaoni huo wa kijamii.
Wakati watumiaji wa Instagram wakifikia bilioni 2.4 duniani, Hamisa anasema kuweka machapisho kila mara katika mtandao huo pamoja na kusafiri nchi mbalimbali na kujuana na watu wengi, kumemfanya kuwa kinara.
Ikumbukwe hadi kufikia Aprili 2024 watumiaji wa mtandao walifikia bilioni 5.44 ikiwa ni sawa na asilimia 67.1 ya watu duniani kote, kati ya hao, bilioni 5.07 ni watumiaji wa mitandao ya kijamii kama Instagram, Facebook, X, TikTok, YouTube, WhatsApp n.k.
Hamisa, Miss XXL After School Bash 2012 na mshindi wa pili Miss Dar Indian Ocean 2011 amefikisha jumla ya wafuasi milioni 11.6, huku Wema, Miss Tanzania 2006 akisalia na wafuasi wake milioni 11.5.
Mwaka 2012 ndipo wawili hao walijiunga na mtandao huo ulioanzishwa Oktoba 2010 na Kevin Systrom na Mike Krieger, kufika Aprili 2012 ukanunuliwa na Meta Platforms, kampuni ya teknolojia ambayo awali ilijulikana kama Facebook Inc.
Hamisa na Wema wanafuatiwa na Shilole mwenye wafuasi milioni 10.5, kisha Jacqueline Wolper - milioni 10.1, Nandy - milioni 9.8, Aunty Ezekiel - milioni 9.1, Vanessa Mdee - milioni 8.9, Linah - milioni 6.9, Gigy Money - milioni 6.7 na Zuchu - milioni 6.1.
Duniani staa wa kike anayeongoza Instagram ni Selena Gomez, mwimbaji, muigizaji na mfanyabiashara wa Marekani ambaye alianza kazi yake ya uigizaji kwenye kipindi cha runinga cha watoto, Barney & Friends mwaka 2002 hadi 2004.
Selena aliyepata umaarufu kwenye kipindi cha Disney Channel, Wizards of Waverly Place, ana wafuasi milioni 426, akifuatiwa na Kylie Jenner - milioni 399, Ariana Grande - milioni 378, Kim Kardashian - milioni 362 na Beyonce - milioni 318.
Kwa matokeo hayo, Hamisa Mobetto anapanda hadi nafasi ya pili katika orodha ya mastaa wa kike wanaofuatiliwa zaidi Instagram Afrika Mashariki nyuma ya Zari The Bosslady kutokea Uganda ambaye ana wafuasi milioni 12.1.
Utakumbuka Hamisa na Zari wote wamezaa na staa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz ambaye kwa ujumla ndiye kinara Instagram ukanda huo akiwa na wafuasi milioni 17.6 tangu ajiunge na mtandao hapo Julai 2012.
Hadi Desemba 2015, Diamond alikuwa ndiye msanii mwenye wafuasi wengi Instagram barani Afrika akiwa nao milioni 1.5, ila kufikia Septemba 2016 akashushwa na Davido wa Nigeria aliyefikisha wafuasi milioni 2.9 kwa wakati huo ila sasa ana milioni 29.5.
Chapa ya Hamisa inazidi kukua na kuvutia wafuasi wengi Instagram baada ya kufanya mambo mawili katika tasnia ya burudani Bongo kwa zaidi ya miaka 14.
Mosi, urembo na mitindo, Hamisa ameshinda taji moja la urembo na kufika hatua nzuri katika mashindano ya ulimbwende kama kuingia nusu fainali ya Miss Tanzania 2011 na 10 bora ya Miss University Africa 2012.
Upande wa mitindo amefanya vizuri na kushinda tuzo kama Abryanz Style Fashion 2016 (Uganda), Starqt Awards 2017 (Afrika Kusini), Swahili fashion Week Awards 2018 (Tanzania), Scream Awards 2021 (Nigeria), Young C.E.O Round Table 2022 (Tanzania) n.k.
Pili, muziki na filamu, mwaka 2018 ndipo Hamisa aliachia wimbo wake wa kwanza 'Madam Hero' uliotengenezwa na C 9, hiyo ni baada ya kuonekana katika video za wasanii kama Quick Rocka, My Baby (2013) na Diamond Platnumz, Salome (2016).
Tayari ametoa EP moja,Yours Truly (2022) ikiwa na nyimbo sita, huku akishirikiana na wasanii kama Diamond, Christian Bella, Seneta Kilaka na Whozu, pia kuna Otile Brown wa Kenya, pamoja na Korede Bello na Singah wote kutokea Nigeria.
Na katika filamu ambapo haonekana kwa sasa kutokana na kile alichodai ni kuzidiwa na majukumu mengine licha ya kuombwa sana kurejea katika uigizaji, Hamisa amecheza filamu kama Endless Love, Vocha n.k.
Akizungumzia mafanikio yake Instagram, Hamisa amesema amekuwa akihakikisha muda wote anakuwepo katika mtandao huo kitu kinachofanya kujadiliwa kila mara, hivyo watu wengi kupenda kumfuatilia.
"Nadhani kila siku ukiingia Instagram utanikuta tu kwa namna moja au nyingine, ukiwa sana kwenye midomo ya watu wanakuwa na kiu ya kutaka kukujua zaidi." alisema Hamisa na kuongeza.
"Pia mimi nimepata bahati ya kwenda nchi mbalimbali na kujumuika na mastaa mbalimbali wa huko, hivyo nao kunifuata (follow), nadhani inasadia kuvuta wafuasi wengi zaidi." alisema mama huyo wa watoto wawili.
Ikumbukwe Hamisa aliyetamba zaidi katika Bongo Fleva kupitia wimbo wake, Ex wangu Remix (2021) akiwa na Seneta Kilaka, tayari ametembelea nchi kama Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Nigeria, Falme za Kiarabu (UAE), China, Marekani n.k.