Harusi ya Taylor Swift kufanyika kwa vificho
Muktasari:
- Inaelezwa harusi hiyo inafanywa kwa siri kiasi kwamba kufikia hatua ya kuweka alama maalumu kwenye kadi za mwaliko ili kuzuia taarifa kuvuja kwa vyombo vya habari.
Marekani. Macho na masikio ya mashabiki yataelekezwa jijini New York Marekani ambapo staa wa muziki Taylor Swift na mchezaji wa NFL, Travis Kelce wanatarajia kufunga ndoa.
Inaelezwa harusi hiyo inafanywa kwa siri kiasi kwamba kufikia hatua ya kuweka alama maalumu kwenye kadi za mwaliko ili kuzuia taarifa kuvuja kwa vyombo vya habari.
Hata kwa upande wa wageni waalikwa inaelezwa ni watu wachache watakaohudhuria harusi hiyo, hadi sasa mwanamuziki Ed Sheeran, ambaye ni rafiki wa muda mrefu wa Taylor amethibitisha kuwepo.
Na huenda Ed Sheeran akatumbuiza katika harusi hiyo baada ya Taylor kudokeza kuwa hawezi kumzuia kuimba endapo kutakuwa na jukwaa.
Ndugu wa Travis Kelce, Jason Kelce, pamoja na mkewe Kylie Kelce, pia wamethibitisha kuwapo kwenye sherehe hiyo. Jason amesema ana furaha kubwa kushuhudia ndugu yake akifunga ndoa na anasubiri kwa hamu kusherehekea siku hiyo muhimu.
Mwimbaji Suki Waterhouse naye amethibitisha kuhudhuria harusi hiyo na huenda akaongozana na mchumba wake, muigizaji Robert Pattinson. Suki amesema anatarajia kupata mawazo mapya ya maandalizi ya harusi yake mwenyewe kupitia hafla hiyo.
Wengine ni muigizaji Zoë Kravitz pia amealikwa kwenye harusi hiyo, ingawa haijafahamika kama mchumba wake, Harry Styles, atahudhuria kutokana na kuwa na ratiba ya tamasha siku hiyo.
Mbali na waliothibitisha, mastaa wengine kama Selena Gomez, dada wa Haim na Sabrina Carpenter wanatajwa kuwa miongoni mwa wageni wanaotarajiwa kuhudhuria, jambo linalofanya harusi hiyo kutajwa kuwa moja ya matukio makubwa zaidi ya burudani mwaka huu.
Uhusiano wa wawili hao ulianza mwaka 2023 baada ya Kelce kueleza hadharani kuwa alitaka kukutana na Swift kufuatia tamasha lake la Eras Tour.
Wawili hao walianza kuwasiliana kwa siri kabla ya kuthibitisha uhusiano wao Septemba 2023, walipotokea pamoja kwenye mchezo wa Kansas City Chiefs.
Baada ya kuwa pamoja kwa takribani miaka miwili, Agosti 2025 walitangaza uchumba na kuvishana pete na Julai 03 wanatarajia kuwa wanandoa wapya.