Taylor Swift awapigia saluti mashabiki wake
Muktasari:
- Tuzo hizo za 12 zilitolewa jijini Los Angeles wikiendi iliyopita ambapo Taylor Swift aliwabwaga mastaa kibao kama Drake, Jelly Roll, Luke Combs, Miley Cyrus, Morgan Wallen, Olivia Rodrigo, Shakira, SZA na Usher.
Mwimbaji wa Pop Marekani, Taylor Swift, 34, amewashukuru mashabiki wake kwa kumpigia kura na kumwezesha kushinda tuzo ya iHeartRadio Music Awards 2024 kama Msanii Bora wa Mwaka.
Tuzo hizo za 12 zilitolewa jijini Los Angeles wikiendi iliyopita ambapo Taylor Swift aliwabwaga mastaa kibao kama Drake, Jelly Roll, Luke Combs, Miley Cyrus, Morgan Wallen, Olivia Rodrigo, Shakira, SZA na Usher.
Akizungumza mapema wiki hii katika video yake aliyoiweka YouTube, Taylor ambaye hakuhudhuria hafla ya utolewaji wa tuzo hizo, vilevile aliwashukuru waandaaji kwa kumuunga mkono katika kazi yake ya muziki.
“Hey! nilitaka kusema asante kwa yeyote aliyepiga kura kwa tuzo hii. Kwa hivyo, asanteni kwa kunipigia kura kwa heshima hii ya ajabu.” Mshindi huyo wa Grammy aliyekuwa amevaa top ya blue na mkufu wa dhahabu alisema kwenye video hiyo.
“iHeart, pia mmekuwa mkiniunga mkono sana katika kipindi chote cha kazi yangu, lakini hasa mwaka huu umekuwa wa kuvutia sana. Ninashukuru kwa hilo.” anasema Taylor Swift.
Ikumbukwe Taylor Swift alikuwa amechanguliwa kuwania vipengele nane vya iHeartRadio Music Awards 2024 na kushinda vitano kikiwemo pia cha Msanii Bora wa Pop.
Ushindi huo unakuja baada ya Februari mwaka huu Taylor Swift kushinda tuzo za 66 za Grammy katika kipengele cha Albamu Bora ya Pop kupitia albamu yake, Midnights (2022) ukiwa ni ushindi wake wa nne katika kipengele hicho.
Mbali na kuwashukuru mashabiki kwa ushindi huo, Taylor Swift alidokeza ujio wa mambo mengi mazuri kutoka kwake ikiwa ni pamoja na albamu yake ya 11, The Tortured Poets Department itakayoachiwa hivi karibuni.
“Tuna mambo mengi ya kusisimua mbele yetu. Ninaendelea na ziara na muhimu zaidi nina albamu mpya kabisa inayoitwa ‘The Tortured Poets Department’ ambayo itatoka Aprili 19 mwaka huu. Sipati picha tutakavyoipokea.” alisema Taylor Swift.
Utakumbuka Taylor Swift ameuza rekodi zaidi ya milioni 200 duniani, huku akiwa ameshinda tuzo 14 za Grammy, tuzo 14 za Primetime Emmy, tuzo 40 za America Music, tuzo 39 za Billboard Music.
Ndiye msanii wa 7 kwanza kuwa bilionea kutokana na muziki pekee ambapo kwa sasa utajiri wake unafikia Dola 1.1 bilioni kwa mujibu wa Forbes. Oktoba 2023 ndipo alitangazwa rasmi kuwa bilionea baada ya mafanikio makubwa ya ziara yake, Taylor Swift: The Eras Tour.
Anaongoza kwa kusikilizwa zaidi Spotify, Desemba 2023 Variety waliripoti kuwa alipokea Dola 104 milioni kutokana na mauzo ya muziki wake katika mtandao huo. .(streams) zaidi ya mara bilioni 26.1 kwa mwaka huo.