Taylor Swift kukunja Sh260 bilioni kupitia mauzo ya Spotify 2023
Muktasari:
Kwa mujibu wa Variety, Taylor Swift nyimbo zake zimesikilizwa (streams) zaidi ya mara bilioni 26.1 tangu Januari, 2023 na iwapo ataendelea kusikilizwa kwa kasi hiyo hadi mwishoni mwa Desemba, basi huenda akapata Dola 130 milioni.
Mwimbaji wa Marekani, Taylor Swift anatarajia kupokea kitita cha Dola104 milioni, wastani wa Sh261 bilioni kutokana na mauzo ya muziki wake katika mtandao wa Spotify kwa mwaka 2023.
Kwa mujibu wa Variety, Taylor Swift nyimbo zake zimesikilizwa (streams) zaidi ya mara bilioni 26.1 tangu Januari, 2023 na iwapo ataendelea kusikilizwa kwa kasi hiyo hadi mwishoni mwa Desemba, basi huenda akapata Dola 130 milioni.
Utakumbuka mtandao wa Spotify ulianzishwa mwaka 2006, una watumiaji zaidi ya milioni 489 kila mwezi, huku watumiaji milioni 205 wakiwa kwenye huduma ya malipo, data hizo ni hadi kufikia Desemba 2022.
Jumatano wiki hii Spotify ilifichua kwamba Taylor Swift ndiye msanii aliyefanya vizuri zaidi katika jukwaa lao kwa mwaka huu. Wasanii wengine bora ni pamoja na Bad Bunny, The Weeknd, Drake na Peso Pluma.
Nyimbo mbili za Taylor Swift ambazo ni 'Cruel Summer' na 'Anti-Hero' pia zimejumuishwa kwenye orodha ya nyimbo 10 bora ulimwenguni 2023, huku albamu yake 'Lover' ikishika namba saba mwaka huu.
Mafanikio hayo ya Taylor Swift yanakuja baada ya Oktoba mwaka huu uchunguzi wa Bloomberg News, kubaini kuwa mwimbaji huyo amefikia hadhi ya ubilionea kufuatia mafanikio makubwa ya ziara yake ya 'The Eras Tour' duniani.
Kwa mujibu wa Bloomberg News, Taylor Swift amefikia utajiri wa Dola1.1 bilioni, tangu alipoanza ziara zake za muziki kimataifa mapema mwaka huu.
Hata hivyo, Washington Post wanaripoti kuwa ziara za mwimbaji huyo zipo mbioni kukusanya Dola 4.1 bilioni. Kiasi hicho kitaifanya ziara hiyo kuandika rekodi kama iliyoingiza fedha nyingi zaidi katika historia.
Mbali na ziara hiyo na mauzo ya Spotify, mwimbaji huyo wa wimbo 'New Romantics' anatazamiwa kutengeneza fedha zaidi kupitia filamu yake ‘Eras Tour’, iliyoanza kuonyeshwa kwenye kumbi za sinema tangu Oktoba 13 mwaka huu.
Inaripotiwa na Variety kuwa tayari filamu hiyo imeingiza Dola 250 milioni ulimwenguni baada ya wiki zake saba sokoni.
Mpaka sasa Taylor Swift ameuza rekodi zaidi ya milioni 200 duniani na ndiye mwanamuziki wa kike anayesikilizwa zaidi Spotify, pia ana rekodi 92 za dunia za Guinness, ameshinda tuzo 12 za Grammy, tuzo 40 za America Music, tuzo 20 na Billboard Music n.k.