Hii ndiyo rekodi ya Michael Jackson isiyozungumziwa
Muktasari:
- Kwa mujibu wa ‘Guinness World Record’ MJ ndiye msanii wa pop aliyeunga mkono mashirika mengi zaidi, akitajwa kusaidia mashirika 39 kwa njia mbalimbali ambapo hadi anafariki mwaka 2009 ripoti zinaonyesha alikuwa ametoa zaidi ya dola milioni 500 ikiwa ni zaidi ya Sh1.3 Trillioni.
Marekani. Ni wazi kuwa zipo rekodi nyingi ambazo watu wanazifahamu kuhusu marehemu Mfalme wa Pop, Michael Jackson. Lakini inaelezwa kuwa moja ya rekodi yake ambayo haizungumzwi sana ni kuwa msanii wa kwanza ambaye ametoa misaada katika mashirika zaidi ya 39.
Kwa mujibu wa ‘Guinness World Record’ MJ ndiye msanii wa pop aliyeunga mkono mashirika mengi zaidi, akitajwa kusaidia mashirika 39 kwa njia mbalimbali ambapo hadi anafariki mwaka 2009 ripoti zinaonyesha alikuwa ametoa zaidi ya dola milioni 500 ikiwa ni zaidi ya Sh1.3 Trillioni.
Misaada hiyo ilihusisha huduma za afya, elimu na kusaidia watoto waliokuwa katika mazingira magumu. Huku mara chache akijitokeza katika vituo vya afya, vituo vya kulelea watoto akitoa misaada ya vitu na fedha taslimu.
Kutokana na juhudi hizo MJ alianzisha taasisi yake ya Heal the World Foundation, taasisi ambayo ilianzisha kampeni ya kusaidia watoto waliokumbwa na matatizo ya kiafya na wale walioathirika na majanga ya asili huku wimbo wake wa ‘Heal the World’ akiutumia kwenye kampeni hizo.
Aidha mpaka kufikia sasa hakuna msanii ambaye amewahi kuifikia rekodi hiyo ya Michael Jackson ya ‘Most charities supported by a pop star’ licha ya kuwepo kwa wasanii kadhaa ambao walitumia gharama nyingi katika kusaidia watu akiwemo Elton John, George Michael, Prince, Taylor Swift na wengineo.
Mbali na rekodi ya kusaidia mashirika 39 duniani. Michael Jackson ana rekodi nyingi kubwa ambazo zinamfanya kuendelea kutajwa hadi leo. Akianza na albamu yake ya Thriller ikiwa ndiyo iliyouzwa zaidi duniani kwa nakala zaidi ya milioni 66, huku video yake ya wimbo huo ikitajwa kuwa maarufu zaidi katika historia ya muziki.
Lakini pia mwaka 1984, alishinda tuzo za Grammy 8 kwa usiku mmoja kupitia albamu hiyo, jambo lililomuweka kwenye vitabu vya historia.
Aidha anatambuliwa na Guinness kama msanii aliyeuza zaidi ya nakala milioni 350 duniani na msanii mwenye tuzo nyingi zaidi duniani. Akiwa na tuzo zaidi ya 400. Lakini pia ndiye msanii wa kwanza wa pop kuingiza mapato ya zaidi ya dola 1bilioni kupitia kazi zake za muziki.
Huku onyesho lake la Super Bowl la mwaka 1993 lilivunja rekodi ya watazamaji, na limeendelea kuwa kipimo cha burudani katika hafla hiyo kubwa ya michezo.
Michael Jackson alizaliwa August 29, 1958 na alifariki dunia Juni 25, 2009 akiwa na umri wa miaka 50 huku sababu ya kifo chake ikitajwa kuwa ni overdose ya dawa za usingizi (propofol na benzodiazepines), dawa ambazo alipewa nyumbani kwake Los Angeles na daktari wake binafsi.