Isarito afichua chimbo wanalotokea waigizaji wakali

Muktasari:

  • Isarito ambaye kwa sasa anatamba kupitia tamthilia mbalimbali ikiwemo ya Jua Kali ambayo anaigiza kama Luka, ameiambia Mwananchi kuwa alianza kuigiza kanisani akiwa mdogo.

Church boy anayekimbiza kwenye Bongo Movie, hivi ndivyo tunaweza kumuita mwigizaji Isarito Mwakalindile ambaye safari yake kwenye tasnia ya uigizaji ilianzia kanisani katika matamasha ya sikukuu mbalimbali.

Isarito ambaye kwa sasa anatamba kupitia tamthilia mbalimbali ikiwemo ya Jua Kali ambayo anaigiza kama Luka, ameiambia Mwananchi kuwa alianza kuigiza kanisani akiwa mdogo.

“Mimi nilianza kufanya maigizo kanisani wakati nilipokuwa mdogo katika kipindi cha ‘Sunday School’ hasa katika wakati wa sikukuu za Chrismas na Pasaka nilikuwa naandaa maigizo kwa kutoa ujumbe wowote uliopo kwenye biblia.

“Lakini mwaka 2017 nilianza kuingia kwenye makundi ya sanaa ya maigizo kipindi hicho nilikuwa naishi Mbagala Kilungule kwa hiyo sehemu niliyokuwa naishi kulikuwa na makundi mengi ya maigizo ilikuwa rahisi mimi kuwa serious na ninachofanya” anasema Isarito.

Hata hivyo mwigizaji huyu anaamini kuwa kupitia makundi ya sanaa ya maigizo ndiko wanakotoka waigizaji wazuri wa baadaye kwa sababu wanakuwa wamezoea, tofauti na waigizaji ambao hawajapitia kikundi chochote.

“Naamini mwigizaji kupitia kwenye makundi ya sanaa kwa sababu ndiyo yanamkomaza na kumpatia elimu ya sanaa upande mwingine makundi yanamsaidia mwigizaji kuwa na nidhamu kwenye kazi na morali ya kupenda kitu ambacho anakifanya.“ anasema Isarito.

Hata hivyo msanii huyu amewataka watazamaji wa Bongo movie kutofikiria sana kuhusu movie za nje kwani anaamini kuna wasanii wazuri nchini ambao wanaweza kufanya kitu kizuri kuliko wa nje.

“Mimi nawaambia watazamaji wasiegemee sana katika upande wa kuangalia kazi za sanaa kutoka nje kwa sababu naamini kuna wasanii wazuri wanaoweza kufanya vizuri kuliko wasanii wa nje.

“Hivyo vijana wasikate tamaa, kupitia sanaa ya uigizaji waamini ni kama kazi nyingine kwani wapo watu ambao wanaweza kufanya vizuri na kuwapa motisha wasioamini kwamba ugizaji unaweza kuendesha maisha” anasema Isarito.

Aidha amefunguka kuhusiana na wahusika kubadilishwa katikati ya tamthilia akidai kuwa uigizaji ni kama kazi nyingine ambayo mtu anaweza kutolewa kampuni fulani kwa sababu zilizo nje ya uwezo na kuwekwa mfanyakazi mwingine.

“ Kitu ambacho watu wanatakiwa wajue kwamba uigizaji ni kama kazi nyingine kama mtu akizingua kazini basi anatolewa analetwa mwingine au umepata matatizo ambayo ameona yatachukua muda mrefu kuwa sawa basi mtu mwingine anakava nafasi yake” anasema.

Pia kutokana na tetesi zinazomuhusisha mwigizaji huyu kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwigizaji mwenziye Femi, Isarito amekanusha tetesi hizo .

 “Ukaribu wangu mimi na Femi ni kazi tu hatupo kwenye mahusiano na tulikutana katika tamthilia ya Jua Kali, unajua kazi zetu za series ni kitu ambacho tuna-shoot muda mrefu kwa hiyo lazima watu wahisi hivyo kwa sababu wanatuona kila mahali pamoja” anasema

Filamu ambazo mwigizaji huyu amewahi kufanya ni Bunji, Jua Kali, Mpango Mbaya, Mlinzi, Sheikh Issa, Obambo ambayo iliweza kumpatia  tuzo za Africa Magic Viewers Choice mwaka 2022 na nyingine nyingi.