Juma Nature atema cheche kwa wasanii
Muktasari:
- Nature ameliambia Mwananchi, hizi stori za bifu la msanii na msanii halihitaji maelezo mengi, inabidi kubadilika kuwa kama mashabiki wa mpira wa miguu wasiwagawe mashabiki kwasababu zao binafsi.
Dar es Salaam. Msanii wa muziki wa bongofleva, Juma Nature amesema wasanii wa tasnia hiyo wasilete mambo meusi na kusababisha bifu kutawala kwenye soko la muziki Tanzania kuliko kazi zao na kuwa gumzo kwa mashabiki wao wakajaa upande wao.
Nature ameliambia Mwananchi, hizi stori za bifu la msanii na msanii halihitaji maelezo mengi, inabidi kubadilika kuwa kama mashabiki wa mpira wa miguu wasiwagawe mashabiki kwasababu zao binafsi.
Alisema wakati ambao mashabiki wa mpira wa miguu wanatamani msimu mpya wa Ligi Kuu uanze hata leo wasanii wa muziki pia wanapaswa kuwa na shauku ya kuwaletea kitu kizuri mashabiki wao na sio wao kuwaletea bifu zao za kiki na kuwa gumzo kwao.
“Katika tasnia ya burudani, ni muhimu kwa mashabiki wa nchi fulani kuwa mstari wa mbele kuwatetea na kuwaunga mkono wasanii wao hata pale ambapo kuna changamoto zinazohitaji kurekebishwa, lakini sisi wasanii ndio tunakuwa tunawagawa mashabiki kwa kutumia mbinu za bifu kwa ajili ya manufaa yetu.
" Hili ni jambo ambalo mataifa kama Nigeria wamefanikiwa kulifanya kwa ustadi mkubwa, tofauti na Watanzania ambao mara nyingi sisi wenyewe tunakuwa wa kwanza kuwachanganya mashabiki wetu na matokeo yake wanatupa maneno makali na dhihaka mitandaoni, "amesema
Nature amesema yeye ni shabiki wa Yanga kindakindaki, lakini huwezi kukuta mchezaji wa Yanga anatengeneza bifu na mchezaji mwenzake ili wawe gumzo kwa mashabiki wao.
" Wao wanachofanya ni kufanya kazi yao ya mpira vyema wakiwa uwanjani na wanazungumziwa kama kawaida, nimetolea mfano wa timu ya Yanga sababu ndio ninayoishabikia na ndio yenye kufanya vizuri kwasasa na hata msimu ujao itafanya vizuri kupitia wachezaji waliosajiliwa.
"Sasa wasanii ambao huleta mambo yao ya kutengeneza bifu na chuki ili wazungumziwe waachane na hayo mambo, sisi tushafanya sana huko kipindi cha nyuma lakini matokeo yake hakuna zaidi ya hivi sasa mnavyotuona, yaani zile ni sifa na pesa za hapo hapo ila hazina maendeleo kwenye muziki wetu,” amesema Nature.
Aidha, Nature aliongeza kusema; “Wapo mashabiki ambao wataendelea kusapoti drama hizo zitakazoendelea na wapo ambao watajiengua sababu ya kuchoka, na wapo mashabiki wapya watakaokuja na wasiwaelewe kazi zao bali wataelewa bifu zao.”
Nature ambaye ni msanii mkongwe wa muziki wa Bongofleva, amewahi kutamba na nyimbo kama Ugali, Mtoto Iddi, Imeniuma Sana na nyingine nyingi. Pia ni mmoja wa kundi la TMK Wanaume, lililokuwa linaundwa na wasanii kama Temba, Chege, KR, Doro na wengine wengi.