Jumba la J.Lo na Ben Affleck ladoda sokoni

Muktasari:
- Wawili hao waliocheza pamoja filamu kama Gigli (2003) na Jersey Girl (2004), wamefanya uamuzi huo muhimu baada ya kushindwa kumpata mnunuzi wa jumba hilo la Beverly Hills tangu walipoanza kuliuza kimya kimya Juni 2024.
Marekani. Hatimaye Jennifer Lopez, 55, na mtalaka wake, Ben Affleck, 52, wamefikia uamuzi wa pamoja wa kuliondoa sokoni jumba lao la kifahari lenye thamani ya Dola68 milioni lililopo Los Angeles baada ya kukamilisha talaka yao tangu Januari mwaka huu.
Wawili hao waliocheza pamoja filamu kama Gigli (2003) na Jersey Girl (2004), wamefanya uamuzi huo muhimu baada ya kushindwa kumpata mnunuzi wa jumba hilo la Beverly Hills tangu walipoanza kuliuza kimya kimya Juni 2024.
Jumatano hii chanzo kimoja kimeliambia jarida la People kuwa ingawa tangu mwanzo walikuwa na matumaini makubwa ya kuuza nyumba hiyo, pia walikuwa na wasiwasi wa kupata hasara kubwa mbeleni.
"Walipunguza bei ili kuvutia wanunuzi zaidi, lakini walipoona hakuna mabadiliko, walipewa ushauri wa kuiondoa sokoni. Ulikuwa ni uamuzi wa kibiashara walioufanya pamoja," chanzo hicho kilidokeza.

Mtaalamu huyo wa masuala ya mali isiyohamishika, aliendelea kwa kusema kuwa soko la sasa ni gumu kwa wauzaji, hasa kwa mali za bei ya juu kama hiyo, hivyo kuisitisha kwa sasa hadi mazingira ya soko yawe rafiki kwa wauzaji ni uamuzi wa busara zaidi.
Ikumbukwe Lopez na Affleck walijaribu kuuza nyumba hiyo bila kuitangaza hadharani mnamo Juni 2024 kabla ya kuiweka wazi sokoni Julai mwaka huo, licha ya kuishusha bei kutoka Dola68 milioni hadi Dola59.95 milioni bado imekosa mteja.
Jumba hilo lenye vyumba 12 vya kulala, bafu 24, majiko 15, eneo la kuegesha magari 15, ukumbi wa sinema, bwawa la kuogelea, saluni, viwanja vya michezo n.k, lilinunuliwa na mastaa hao kwa bei ya Dola61.8 milioni ikiwa ni takribani mwaka mmoja wa ndoa yao