Kabla ya kutusua Bruno Fernandes alilelewa na Ana
Muktasari:
- Ana amekuwa na mchango mkubwa katika safari ya Fernandes kufikia ndoto ya kuwa mchezaji wa kulipwa akimsaidia katika nyakati ngumu mwanzoni mwa taaluma yake.
Dar es Salaam. Safari ya kufikia umaarufu na mafanikio ya kisoka kwa Bruno Fernandes imeambatana kwa karibu na msaada mkubwa kutoka kwa mkewe Ana Pinho ambaye tangu mwanzo alionyesha imani kubwa kwa kiungo huyo wa Manchester United.
Ana amekuwa na mchango mkubwa katika safari ya Fernandes kufikia ndoto ya kuwa mchezaji wa kulipwa akimsaidia katika nyakati ngumu mwanzoni mwa taaluma yake.
Kabla Fernandes hajaanza kupata kipato kidogo hata kikubwa kama mchezaji, Ana ndiye aliyekuwa analipia gharama za miadi yao lakini sasa hayo yote ni historia inayoacha funzo kubwa la maisha.
Je, Ana Pinho ni nani hasa? Mrembo huyu alizaliwa na kukulia katika mji wa Maia huko Ureno, baadaye alisoma katika shule ya sekondari ya Boavista ambako alikutana Fernandes kwa mara ya kwanza wakati huo akiwa na umri wa miaka 17.
“Tulikuwa na miaka 16/17. Tulikutana shuleni. Wakati huo nilikuwa Boavista, hivyo tukajikuta tuko darasa moja. Alijaribu mara kadhaa kunibusu lakini nilikuwa namkatalia kila mara, kisha baadaye nikakubali,” alisema Ana.
Walidumu katika uhusiano kwa takribani miaka minane na ndani ya kipindi hicho Fernandes alianza kucheza soka katika klabu ndogo kama Sampdoria, Novara na Udinese.
Fernandes alipohamia Italia kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 18 ili kujiunga na klabu ya Novara, aliandamana na Ana ingawa alirejea Ureno kuendelea na mambo yake mengine.
Mwaka 2015, wawili hao waliamua kufunga ndoa, harusi yao ilihudhuriwa na watu takribani 350. Katika miaka ya mwanzoni ya ndoa yao, Ana alilazimika kusafiri mara kwa mara kati ya Ureno na Italia ili kuwa karibu na mumewe.
Walijaliwa kupata mtoto wa kike aitwaye Matilde hapo Januari 2017, na Ana aliamua kubaki Ureno ili kumlea. Mwaka 2020, Fernandes aliposaini Man United, Ana pia alihamia Uingereza, kitendo kilichobadilisha maisha ya Fernandes akajithibitisha kama kiungo bora duniani.
Akiwa kama mama wa watoto wawili kwa sasa, Ana kupitia ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi 123,000, mara kadhaa huonyesha maisha ya familia yao na shabiki wengi wameonyesha upendo kwao.
Kabla ya fainali ya Kombe la FA 2023/24 dhidi ya Manchester City kwenye Uwanja Wembley, Fernandes alitoa ujumbe wa kipekee kuhusu Ana akisema yeye ndiye aliyekuwa analimpia tiketi za kwenda kutazama sinema kwa sababu hakuwa na fedha!
“Alikuwa na kazi nzuri kama mwamuzi wa futsal kila mwishoni mwa wiki. Alikuwa akichezesha mechi tatu au nne kwa siku za Jumamosi, kisha Jumapili tulikuwa tunaenda sinema,” alisema Fernandes.
Fernandes alisema alikumbana na changamoto kubwa wakati akiichezea Udinese ya Italia. Hawezi kusahau tulio la kocha wake aliposema hana nafasi katika kikosi chake wakati wakipata chakula kama timu.
Hata hivyo, wakati ndoto yake ya kufikia mafanikio makubwa katika soka ikionekana kama jambo lisilowezekana, Ana alikuwapo pembeni yake akimsisitiza kusonga mbele.
“Unakumbuka nilipokuwa nalia hotelini? Unakumbuka uliniambia nini? ‘Endelea. Hii ndio ndoto yako. Angalia tulipo sasa… Nyakati ngumu hazijawahi kutuvunja moyo na kuturudisha nyuma,” Fernandes alikumbushia.
Hatimaye Man United ilishinda taji hilo la FA mbele ya Man City kwa ushindi wa mabao 2-1, Fernandes ambaye pia ni mshindi wa Euro 2024, leo hii anaishi ndoto yake huku Ana akiwa kando yake.
Mnamo Juni, Fernandes alifichua kuwa mkewe Ana ndiye mshawishi kukataa dili la kutimkia Saudi Arabia kuichezea Al-Hilal, na matokeo yake akaamua kusalia Man United ambayo msimu huu chini ya Ruben Amorim imeanza vibaya.
Nahodha huyo wa United alilipwa mshahara wa Pauni 200 milioni kwa kipindi cha miaka mitatu, huku Al-Hilal ikijitolea kulipa ada ya uhamisho ya Pauni 100 milioni ili kumnasa lakini aliamua kubaki kwenye Ligi Kuu England (EPL).
“Ilikuwa ofa yenye malengo makubwa sana. Rais wao alikuwa mtu wa kipekee. Hatukuwahi hata kujadili kiasi cha fedha, wakala wangu ndiye aliyejua. Kisha nikazungumza na mke wangu na familia yangu, na yeye akaniuliza malengo yangu binafsi kwenye kazi yangu ni yapi?” Alisema.
“Ana siku zote amenisaidia sana, hivyo ilikuwa ni hatua rahisi kuchukua uamuzi. Kwa sasa nataka kuimarisha uchezaji wangu katika kiwango cha juu nikicheza mashindano makubwa. Na nahisi bado nina uwezo huo,” alisema Fernandes.
Mara kadhaa Ana na watoto wake wamedhuria mechi za Fernandes pale OT.