Mambo mawili Marioo akija na EP mpya
Muktasari:
- Marioo, mwanzilishi wa Bad Nation Records Label, tayari ameweka wazi jina la EP hiyo kuwa ni "MMMCXII" huku akiwataka mashabiki wake kuwa tayari kupokea muziki mzuri kutoka kwake.
Dar es Salaam. Mwimbaji wa Bongofleva, Marioo yupo mbioni kuachia Extended Playlist (EP) ya kwanza tangu ameanza muziki, hatua inayoibua mambo mawili kuhusu safari yake ya muziki akisaka mafanikio ya juu zaidi.
Marioo, mwanzilishi wa Bad Nation Records Label, tayari ameweka wazi jina la EP hiyo kuwa ni "MMMCXII" huku akiwataka mashabiki wake kuwa tayari kupokea muziki mzuri kutoka kwake.
EP hujumuisha nyimbo kuanzia nne hadi nane ambazo kwa ujumla huwa dakika kati ya 10 hadi 30, wakati albamu huwa na nyimbo kuanzia nane ambazo kwa ujumla zinakuwa na dakika kati ya 30 hadi 80.
Marioo anakuja na EP ili kupata 'hit' nyingine kufuatia mafanikio ya albamu yake ya pili, The God Son (2024) iliyotoka ikiwa na nyimbo 17, huku ikishirikisha mastaa kama Alikiba, Aslay, Bien, na Patoranking.
Albamu hiyo ilitoa wimbo wake maarufu 'Nairobi' uliotayarishwa na Kaniba Creator huku akimshirkisha mwimbaji wa kundi la Sauti Sol kutokea Kenya, Bien.
Wimbo huo alioutumbuiza katika hafla ya tuzo za Trace 2024 zilizofanyika Zanzibar, hadi sasa video yake imetazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 55 ikiwa ni ya pili kwake kufanyika vizuri zaidi katika mtandao huo.
Kubwa zaidi, ulikuwa miongoni mwa nyimbo zilizoingia katika mchakato wa kupata kazi chache kwa ajili ya tuzo za 68 za Grammy 2026, ikiwa ni wimbo wake wa kwanza kufanya hivyo akijitosa kipengele cha Best African Music Performance.
Hata hivyo, haukufanikiwa kuchaguliwa badala yake waliopata nafasi ni Burna Boy (Love), Davido (With You), Eddy Kenzo (Hope & Love), Ayra Starr (Gimme Dat) na Tyla (Push 2 Start) aliyeibuka mshindi.
Mbali na kusaka 'hit' nyingine, tunaweza kusema Marioo anakuja EP ili kuendana na kile ambacho majina makubwa yamekuwa yakifanya katika Bongofleva kwa sasa, yaani kuachia EP baada ya albamu kadhaa.
Alikiba, Diamond Platnumz, Jux, Nandy, Rayvanny, wote wamefanyaje hivyo kwa nyakati tofauti, na sasa ni zam ya Marioo
Alikiba kutokea Kings Music baada ya kuachaia albamu zake tatu; Cinderella (2007), Ali K4Real (2009) na Only One King (2021), ikafuata EP, Starter (2024) yenye nyimbo saba huku akiwashirikisha Jay Melody, Marioo na Nandy.
Diamond kutokea WCB Wasafi baada ya kutoa albamu tatu; Kamwambie (2010), Lala Salama (2012), na A Boy From Tandale (2018), ikafuata EP, First of All (2022) yenye nyimbo 10 akishirikiana na wasanii wengi wakiwemo Zuchu na Mbosso.
Naye Jux baada ya kutoa albamu mbili; The Love Album (2019) na King of Hearts (2022), akaja na EP, A Day To Remember (2025) yenye nyimbo saba ikiwa na lengo la kufurahia ndoa yake na mkewe Priscilla kutokea Nigeria.
Nandy baada ya kuachia albamu yake ya kwanza, The African Princess (2018), zikafuata EP tatu, Wanibariki (2021), Taste (2021) na Maturity (2022) yenye nyimbo tano huku akiwashirikisha Lody Music, Dulla Makabila na Oxlade kutokea Nigeria.
Rayvanny kutokea Next Level Music (NLM) ambaye ana albamu mbili; Sound From Africa (2021) na The Big One (2024), tayari ametoa EP nne, Flowers (2020), New Chui (2021), Flowers II (2022) na Unplugged Session (2022).
Kwa muktadha huo, Marioo ambaye ana albamu mbili, The Kid You Know (2022) na The God Son (2024), ni wazi naye anataka kufanana na wenzake wanaofanya vizuri kwa wakati huu ndani ya Bongofleva.
Marioo, mshindi mara nne wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), alitoka kimuziki na ngoma yake, Dar Kugumu (2018) iliyotayarishwa na Abbah ambaye pia ndiye alikuwa mtayarishaji kuu wa albamu yake ya kwanza