Mandojo alivyotumia fursa ya machinga kuondolewa barabarani

Mwandishi wa gazeti hili, Imani Makongolo akifanya mahojiano na msanii Mandojo

Katika muendelezo wa makala hii, Mandojo ameeleza namna alivyopitia changamoto za hapa na pale, lakini ndoto yake kubwa ya kufanya biashara haikuwahi kufa.

"Kama nilivyosema, ndoto yangu tangu zamani ilikuwa biashara, miaka 10 iliyopita nilianzisha ya maduka pale Kariakoo.

"Nilianza kufanya mwenyewe kisha nikaajiri vijana wanne wa kunisaidia ambao nao walikuwa wakipata riziki na kuhudumia familia zao kupitia biashara ile," anasema.

Katika kipindi hicho, Mandojo alikuwa na maduka mtaa wa Narung'ombe na mtaa wa Congo, akiuza kwa jumla na rejareja vitu mbalimbali, vikiwamo viatu.

"Nilianza kufuata mwenyewe mzigo China, kwa mwaka nilikuwa nakwenda mara nne nikapata uzoefu na sasa China imekuwa kama nyumbani, nikiwa kule ni kama niko Dar es Salaam tu, nimejifunza tabia zao, wanafanikiwa vipi na mambo mengine ya asili ya Taifa hilo.

"Hapa nyumbani kuna fursa nyingi lakini tunashindwa kuzitumia kwa sababu mbalimbali kama za kutokuwa na elimu, lakini ukitembea unapata na mambo mengine kama hayo.

"Tuna vitu vingi, lakini cha kusikitisha utakuta vijana wapo maskani tu wengine wanasubiri hadi waajiriwe ofisini, ingawa fursa zipo nyingi kama tukiamua," anasema Mandojo, ambaye shuleni alikuwa akichukua mchepuo wa sanaa.

"Nimesoma HGK, nilipohitimu kidato cha sita nikaingia kwenye muziki na biashara, wakati wetu tunafanya muziki shule ilikuwa ni lazima, hata vipaji vyetu viligundulika kuanzia shule, nakumbuka tulikuwa tunatoroka tunakwenda mlimani kujifunza kuimba.”

Anasema muziki ulimpa chaneli ya biashara, na baadhi ya wateja walienda kwenye maduka yake mtaa wa Congo na Narung’ombe kwa sababu ya kumuona Mandojo ambaye walimfahamu kwenye muziki.

"Mwaka jana ndiyo nimeifunga biashara ya Kariakoo na kuanzisha huu mradi hapa Kisewe," anasema.

Kuingiza Sh4,800 kila baada ya saa moja

Mradi huo ambao unafahamika kama Kwa Mandojo Soko la Wajasiriamali na mitumba Kisewe, linawafanyabiashara mbalimbali.

"Hapa kuna vizimba 100 na fremu 10, mradi umekamilika kwa asilimia 85, na baadhi ya wafanyabiashara wameanza shughuli zao.

"Kwenye kizimba kodi kwa siku kwenye kila kibanda ni Sh1000 na fremu moja kwa mwezi ni Sh50,000," anasema Mandojo.

Kwa uwekezaji huo, kama utakamilika na vizimba na fremu zote kufanya kazi, Mandojo sasa atakuwa na uhakika wa kuingiza zaidi ya Sh115,000 kila siku au kila saa Sh4,800 hata akiwa nyumbani amelala.

"Huu mradi naona utawasaidia vijana watakaofanya biashara katika mazingira rafiki hapa kwa gharama ndogo, lakini pia Serikali itapata mapato na mimi siku zijazo nitapata kile ninachokifikiria kupitia hapa," anasema.

Alivyoamua kuwekeza

Mandojo anasema alipata wazo hilo baada ya wafanyabiashara kuamuriwa kutoka barabarani na kwenda kwenye maeneo rasmi.

"Mkakati huo ndio ulikuwa chanzo cha kupatikana kwa eneo hili, Rais alitaka kila wenyeviti wa Serikali za mitaa wawatafutie watu maeneo ya masoko kwa ajili ya kufanya biashara katika maeneo salama na rafiki.

"Hili lilikuwa ni eneo mojawapo lililotafutwa na Serikali ya Kisewe, wafanyabiashara walikuwa ni wengi barabarani, tulikutana na mwenyekiti wetu kwa ajili ya kupata eneo.

"Serikali ya mtaa ikamuomba Anorld ambaye ndiye mwenye eneo, akakubali, watu wakagawiwa, wengi walitaka hii fursa lakini baadhi hawakuwa na mtaji wa kuwawezesha kuanza biashara na kujenga vizimba.

"Ilienda hivyo, soko likawa linayumba, mimi nikaongea na Serikali ya mtaa na mwenye eneo kwamba niko tayari kujenga soko, kulipa ushuru wa Serikali na kwa mwenye ardhi, kisha mimi nitapangisha ili iwe rahisi kwa vijana wengine sasa kufanya biashara.

"Niliwarahisishia, hivyo ikawa kama mtu ana mtaji wa Sh300,000, atakuwa na uwezo wa kuja kupanga kizimba na kuanza biashara akilipa Sh1,000 kwa siku kwa kizimba, akifanya biashara katika mazingira mazuri na rafiki yenye umeme na huduma nyingine muhimu," anasema.

Anasema aliiona hiyo fursa kwa kuwa amefanya biashara ndogondogo hadi za kati anafahamu changamoto zake na namna vijana wanavyohangaika kupata maeneo ya kufanyia biashara hadi kuingia barabarani.

"Niliona niwasaidie vijana wenzangu, lakini pia kujisaidia hata mimi, tayari ujenzi umekamilika kwa asilimia 85, bado kuna maeneo madogo madogo hayajakamilika, nimewekeza Sh100 milioni, ni pesa nyingi, japo naamini mambo yakienda vizuri huu mradi utanilipa hivyo naendelea kupambana.

"Ikitokea nikapata sapoti ya Serikali kukamilisha hiyo asilimia 15 ya ujenzi iliyobaki nitashukuru mno," anasema Mandojo, akionyesha eneo hilo lenye ukubwa wa ekari mbili ambalo limejengwa vizimba zaidi ya 100, fremu 10 na kila moja ina mita yake ya umeme, soko likiwa limejengwa kisasa na kuwekewa huduma zote muhimu kwa binadamu, huku kwenye baadhi ya fremu na vizimba kukiwa na biashara zinaendelea.

"Kuna stoo pia imejengwa kwa ajili ya soko, naendelea kufanya maboresho, nimewekeza pesa nyingi hapa, litakapokamilika na vizimba vyote kufanya kazi jasho langu litaanza kurudi, huu ni mwaka wa pili sasa unaenda tangu kuanza kwa mradi huu, natumia nguvu yangu mwenyewe, natamani Serikali inisapoti kwani nahitaji kujenga soko la mfano lenye mazingira bora ambalo wateja wakija wanapata huduma nzuri katika mazingira bora.

Anasema kila baya lina zuri ndani yake, ukitazama kwa jicho la fursa na ndicho kilichotokea kwake.

“Wamachinga walipokuwa wanaondolewa barabarani nilichukulia kama changamoto kwa sababu najua biashara ndogondogo na za kati zilivyo. Ila nikaangalia upande mwingine wa fursa, ndiyo nikaja na hili wazo, hivyo ni kujifunza kubadili changamoto kuwa fursa kila mahali unapotafuta maisha utafanikiwa, kuliko kulalamika.

itaendelea kesho