Met Gala Bongo inawezekana tukifanya haya

Muktasari:

  • Tamasha hili linaandaliwa na Taasisi ya Mavazi ya Metropolitan Museum of Art huko Manhattan New York, Marekani.

Met Gala ni tamasha la mitindo ya mavazi linalofanyika kila mwaka likilenga kukusanya fedha kwa ajili ya Makumbusho ya Costume ya Metropolitan.

Tamasha hili linaandaliwa na Taasisi ya Mavazi ya Metropolitan Museum of Art huko Manhattan New York, Marekani.

Lililoanzishwa mwaka 1948, huwakutanisha watu maarufu duniani kutoka nyanja  mbalimbali zikiwemo muziki, filamu, michezo, mitandao ya kijamii na kawaida hufanyika kila Jumatatu ya kwanza ya mwezi Mei.

Kila mwaka tamasha hili huwa linabeba ujumbe tofauti. Kwa mwaka huu ujumbe ulikuwa "The Garden Of Time" ikimaanisha bustani ya wakati, ndio maana nguo nyingi zilizooneshwa zilitawaliwa na maua.

Baadhi ya mastaa waliohudhuria tamasha hilo kwa mwaka huu ni pamoja na Nicki Minaj, Cardi B, Ariana Grande, Kim Kardashian, Gigi Hadid, Tyla na wengine wengi.

Hata hivyo, zikiwa zimepita siku chache tangu kufanyika kwa hafla hiyo nchini Marekeni, hapa nchini kuna waliojaribu kufanya namna hiyo licha ya kuwa haikuwa katika maandalizi yanayotakiwa.

Katika sherehe hiyo, ilitumika kuonesha mavazi kwa wanawake waliofanikiwa katika nyanja mbalimbali ambayo ilipewa jina la Extra Vaganza au Mwanamke Nangai.

Mwananchi ilifanya mahojiano na baadhi ya wabunifu wa mavazi nchini kujua nini kifanyike ili Tanzania kuwe na hafla ya kuendana na Met Gala.

Martin Kadinda mmoja wa wabunifu mavazi, anasema wazo la Extra Vaganza yeye ni mmoja wa watu waliolitoa na kueleza kuwa mpango ni kuja kuwa na onesho la namna hiyo kwa ukubwa.

“Hata sisi wakati tunafanya shughuli ile hatukujua kama itakuwa kubwa kiasi kile, hivyo tumeona kuna haja ya kujipanga kuja na onesho la aina hiyo hata kama halitafikia lile la Met Gala,” anasema Kadinda.

Amesema watu takribani 200 walihudhuria katika hafla hiyo ya Extra Vaganza, lakini katika upande wa kuwa na hafla kama Met Gala itatakiwa kukutanisha walau watu 3000.

Amesema anaamini kukiwa na hafla kama hiyo wabunifu wa mavazi wataweza kuonesha kazi zao na kuwa moja ya eneo ambalo wataweza kufanya biashara katika sekta ya mavazi.

Ili kufanikisha hilo, ameiomba serikali kuanza kuangazia watu wasiokuwa na elimu, kwani nao wanavipaji lakini wameweza kuajiri wasomi.

"Kuna watu wengi mtaani hawajaenda shule lakini wana vipaji vikubwa ni wakati wa serikali kuwageukia kuona namna gani wanawasaidia, ninaimani wakiangaliwa kwa jicho lingine wanaweza kuifanyia nchi mambo makubwa sana," anasema Kadinda.

Naye Mkurugenzi wa Umoja wa Wabunifu Mavazi Nchini, Kemi Kalikawe, anasema  kuna maonesho ya mavazi kama   Swahili Fashion Week, Stara na mengineyo bado hufanyika kila mwaka.

Hata hivyo, kwa upande wa kuwa na Met Gala Tanzania, Kemi anasema inahitaji uwekezaji mkubwa.

“Kwa mfano ilipofanyikia Met Gala kuna mpaka ngazi ambazo mtu kama kavaa nguo ya kujimwaga sana ni rahisi kuiona hadi mwisho wake,  kumbi ambazo sisi hapa kwetu hatuna.

“Nadhani ifike mahali nchi tuwe serious na sekta hii ya mavazi kuanzia serikali ambayo yenyewe inaweza kutenga siku moja vazi flani likavaliwa kama sare. Wabunifu wengi wanajiendeleza wenyewe tena kwa kwenda kusomea nje ya nchi.

"Vyuo vinavyofundisha fashion vingi vimejikita kwenye upande wa viwandani lakini siyo kama wakina sisi ambao tunabuni mavazi hayo kwa mikono yetu, kuna kitu hapa hakipo sawa tunapaswa kuwa na shule zetu za kuwafundisha wabunifu badala ya kusubiri wabunifu wachache waliopo ndiyo wawainue,”anasema  Kemi.

Amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia kuondokana na kuiga nguo za wabunifu wa nje kwa kuwa yote hii ni kutokuwa  na elimu ya ubunifu .

Ilichosema Serikali

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ukuzaji na Maendeleo ya Sanaa (Basata), Edward Buganga, amesema serikali imeliona hilo katika bajeti ijayo ya fedha inayoanza Julai mwaka huu wameliwekea mikakati.

Kuhusu vyuo vya kutoa elimu, alisema vyuo vikuu vinatoa elimu hiyo ya ubunifu wa mavazi.

"Siyo kweli kwamba hatuna vyuo  vinavyofundisha mambo ya ubunifu wa mavazi, sema tu kwa kuwa ni option kwa mwanafunzi ndiyo maana kama watu wanaona hayapo,” anasema.