Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miaka 10 drama za MTV EMAs kwa Alikiba!

Muktasari:

  • Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa Alikiba kupata ushindi huo kwani kulikuwa na sarakasi za hapa na pale kutoka kwa waandaaji, sarakasi tunazoweza kuziita drama kwa jinsi jambo hilo lilivyoanza hadi kuhitimishwa

Dar es Salaam. Kama utani vile inaenda kutimia miaka 10 tangu Alikiba alipong’aa MTV Europe Music Awards (EMAs), tuzo kubwa zaidi aliyowahi kushinda katika safari yake ya muziki ambayo ina miaka zaidi ya 23 tangu ilipoanza.

Hata hivyo, haikuwa rahisi kwa Alikiba kupata ushindi huo kwani kulikuwa na sarakasi za hapa na pale kutoka kwa waandaaji, sarakasi tunazoweza kuziita drama kwa jinsi jambo hilo lilivyoanza hadi kuhitimishwa.  

Alikiba, mwanzilishi wa Kings Music Label, alishinda tuzo ya MTV EMAs 2016 ikiwa ni mwaka mmoja baada ya mshindani wake katika Bongofleva, Diamond Platnumz kufanya hivyo katika hafla iliyofanyika Italia.

Tuzo za MTV EMAs hufanyika kila mwaka katika nchi tofauti barani Ulaya, na huandaliwa na kampuni ya Paramount International Networks kwa lengo la kutambua mchango wa wasanii na muziki katika utamaduni.

MTV EMAs zilikuja baada ya MTV Video Music Awards (VMAs) ambazo hutolewa Marekani ila hizi hutunza video za muziki pekee, hivyo lengo lingine la MTV EMAs lilikuwa kuwafikia wasanii wengi nje ya MTV VMAs.

Hafla ya kwanza ya MTV EMAs ilifanyika Novemba 24, 1994 katika ukumbi wa Brandenburg Gate huko Berlin nchini Ujerumani, na tangu 2007 mashabiki wamekuwa wakipiga kura mtandaoni kuwachagua washindi.  

Mkali wa Pop na R&B kutokea Canada, Justin Bieber, anashikilia rekodi kama mwanamuziki aliyewika zaidi tuzo za MTV EMAs kwa muda wote akiwa ameshinda mara 22, huku akifuatiwa na Taylor Swift.

Septemba 2016, Alikiba alitangazwa kuwania MTV EMA akiwekwa kipengele cha Msanii Bora Afrika huku washindani wake wakiwa ni Wizkid, Olamide (Nigeria), Cassper Nyovest na Black Coffee (Afrika Kusini).

Msimu huo hafla yake ilifanyika Novemba 6, 2016 katika jiji la Rotterdam nchini Uholanzi, huku Alikiba, mkali wa kibao, Mwana (2014), akiwa msanii pekee kutokea Afrika Mashariki aliyechaguliwa kuwania.

Alipata nafasi hiyo baada ya kufanya vizuri na wimbo wake, Aje (2016), ambao pia ni wa kwanza kutoka kwa msanii aliyesainiwa Sony Music Entertainment Africa kutazamwa zaidi ya mara milioni 5 YouTube.  

Mashabiki wengi walimpigia kura Alikiba kama ulivyo utaratibu wa MTV EMAs, kubwa zaidi ni pale Diamond alipojitokeza na kuhamasisha mashabiki wa pande zote kumuunga mkono kwa maslai ya nchi.  

“Akikosa tuzo hiyo itaonekana kabisa Watanzania wote tumekosa, kwa hiyo tuhakikishe tunampigia kura ili tuirudishe hiyo tuzo nyumbani,” alieleza Diamond, mshindi wa MTV EMAs mara tatu.

Hatimaye siku ya tukio lenyewe ikawadia na ndipo drama zikaanza, kivipi?, katika tovuti ya MTV EMAs, Alikiba ndiye aliyekuwa akiongoza kwa kura, hivyo wengi walikuwa wanatarajia ndiye atatangazwa mshindi.

Lakini mambo yakuwa hivyo, Wizkid ndiye akatangazwa mshindi, jambo ambalo liliacha maswali pamoja na malalamiko mengi kwa mashabiki ambao kupitia mitandao ya kijamii waliwajia juu waandaaji.

“Kiukweli hata mimi mwenyewe sijui ni kitu gani kimetokea... mashabiki wanataka kujua nini kimetokea ili kila mtu ajue ni vigezo gani wametumia kufanya nisishinde ile tuzo, hilo ndilo tunangojea,” alisema Alikiba.

Baadaye MTV EMAs walikiri makosa na kuomba radhi, huku wakitaja vigezo vilivyotumika kuwateua ni   kiwango cha video zao kuchezwa katika chaneli za MTV, redio na mtandaoni (streams) katika maeneo yao.

“Wizkid na Alikiba wote ni wasanii wakubwa na wanastahili kushinda katika MTV EMAs, na tunawapongeza kwa moyo wote kwa mafanikio hayo. Tunaomba radhi kwa kosa lililojitokeza,” taarifa ilieleza.

Hiyo ilikuwa habari mbaya kwa Wizkid, kibaya zaidi ni kitendo cha mashabiki kumzodoa vilivyo Instagram hadi akaamua kufuta posti zote ambazo aliweka akisheherekea ushindi wake ulikuja kubatilishwa.

Kwa upande wake Alikiba aliwashukuru mashabiki, wasanii wenzake, vyombo vya habari na menejimenti yake kwa kumuunga mkono bila kuchoka katika kazi zake hadi kufikia mafanikio hayo.

“Shukrani kwa MTV EMAs kwa heshima hii, nina furaha sana kwa ushindi huu, ni heshima kwangu na nchi yangu Tanzania pamoja na Afrika Mashariki kwa ujumla. Ushindi wangu ni wetu sote,” alieleza Alikiba.

Hata hivyo, alikuja kukabidhiwa rasmi tuzo yake mwaka uliofuatia nchini Afrika Kusini ambapo alikuwa na ziara yake huko, na kufikia Februari 28, 2017 akawasili nchini akiwa ameibeba tuzo hiyo.

Ikiwa inaelekea kutimia miaka 10 tangu hayo yamejiri, Alikiba hajafanikiwa kushinda tuzo nyingine ya MTV EMAs, na hadi sasa inaendelea kusalia kama tuzo ya juu zaidi aliyowahi kushinda.

Staa mwingine wa Bongofleva aliyeshinda MTV EMAs ni Diamond aliyebeba mbili 2015, na moja 2023, akiwa kinara kwa Afrika sawa na Tyla wa Afrika Kusini ambaye naye ameshinda tuzo tatu ila msimu mmoja.

Hadi sasa Diamond amechaguliwa mara tano kuwania MTV EMAs na kushinda mara hizo tatu akiwa ni mwanamuziki pekee kutokea Afrika Mashariki mwenye rekodi hiyo.

Mwimbaji wa Pop kutokea Marekani, Taylor Swift ndiye amechaguliwa kuwania tuzo hizo mara nyingi zaidi kwa muda wote. Mkali huyo wa kibao cha Blank Space (2014), amewania mara 65, huku akishinda mara 19.