Mtunzi wa ‘Nikupe Nini Mungu Wangu’ afariki dunia
Muktasari:
- Lukando amefariki na kuacha alama ndani ya Kanisa Katoliki na nje kutoakana na utunzi wake uliowavutia wengi.
Dar es Salaam. Mtunzi maarufu wa nyimbo za Kanisa Katoliki, Basili Lukando, amefariki dunia jana Machi 24, 2026 na kuzikwa leo Machi 25, 2026 mkoani Morogoro katika makaburi ya Kihonda Maghorofani.
Lukando, ambaye enzi za uhai wake alikuwa pia mwalimu wa kwaya, anakumbukwa kwa kutunga nyimbo nyingi zilizopata umaarufu mkubwa ndani ya Kanisa Katoliki, zikiwamo Nikupe Nini Mungu Wangu, Sasa Wakati Umefika, Lala Kitoto na nyinginezo.
Akizungumza na Mwananchi leo, Mratibu wa Utume wa Kwaya Katoliki Tanzania (UKWAKATA), Bernard Mukasa, amethibitisha kifo hicho akieleza kuwa msanii huyo alifariki baada ya kuugua homa.
“Ni kweli amefariki jana nyumbani kwake Morogoro. Aliugua kwa kipindi fulani, akapata nafuu, kisha akapata matatizo ya kifua, akatibiwa na kuimarika. Hata hivyo, hivi karibuni alipata homa kali kwa siku kadhaa hali iliyosababisha umauti wake,” amesema Mukasa.
Amesema marehemu ameacha alama kubwa kupitia kazi zake, akibainisha kuwa nyimbo zake zilijulikana zaidi kuliko hata jina lake.
“Alitunga nyimbo nyingi zilizopendwa sana na waumini. Watu wengi wanazijua nyimbo kama Nikupe Nini Mungu Wangu, Sasa Wakati Umefika na Familia Takatifu, lakini hawakumfahamu kwa karibu mtunzi wake,” amesema.
Akizungumzia maisha yake, Mukasa amesema Lukando alikuwa mtu wa utulivu na mbunifu mkubwa, aliyependelea kufanya kazi zake kimyakimya.
“Alikuwa mkimya lakini mwenye kipaji kikubwa. Alifanya kazi zake kwa utulivu mkubwa na mara nyingi matokeo yake yalikuwa ya kushangaza kwa ubora,” amesema.
Katika uhai wake, Lukando aliwahi kufundisha kwaya mbalimbali, zikiwamo za Mtakatifu Michael Malaika Mkuu Parokia ya Kawe jijini Dar es Salaam, Kanisa Kuu la Mtakatifu Patrick Jimbo la Morogoro, pamoja na kwaya ya Benki ya NBC enzi za mashirika ya umma kabla ya mageuzi yaliyozaa benki ya NMB.
Mukasa amesema baadhi ya nyimbo zake maarufu zilitungwa kati ya mwaka 1990 na 1993, kipindi ambacho alitoa kazi kadhaa kwa wakati mmoja na kupokelewa vizuri na waumini.
“Katika kipindi hicho alitoa nyimbo kadhaa za matoleo kwa pamoja na zote zilifanya vizuri sana,” amesema.
Nyimbo nyingine za Lukando
- Siku Hii
- Tuimbe Bwana Amejifufua
- Asante Mungu Mwenyezi
- Misa Ya Mt. Consolatha
- Furaha Yangu Ni Kubwa Sana
- Ni Usiku Wa Manane
- Siku Hii Ndiyo Aliyoifanya Bwana
- Sekwensia Ya Pasaka
- Hakuna Aliye Sawa Naye Mungu