Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Nandy na jawabu kamili la Ruge 

Muktasari:

  • Watajinasibu kufahamiana sana na wadau. Kama msanii husika ni binti wataenda mbele zaidi. Bia, sifa na tantalila kibao. Hata kama havutii lakini akili ya pombe itafanya awe Beyonce ghafla.

Dar es Salaam, Kuna watu wapo kukupa moyo kwa maisha ya kipaji. Watakusifia kuwa unaweza na kila aina ya maneno ya faraja utapewa. Hao watu huishia kukusifia tu kwenye vikao vya baa au popote. 

Watajinasibu kufahamiana sana na wadau. Kama msanii husika ni binti wataenda mbele zaidi. Bia, sifa na tantalila kibao. Hata kama havutii lakini akili ya pombe itafanya awe Beyonce ghafla.

Hao hawana muendelezo zaidi wa kumsaidia baada ya hapo. Msanii atabaki kwenye ‘data bezi’ ya idadi ya madem zake. Ndo wanaowatia ndimu hata wasanii ambao tayari wana majina mjini. 

Kwamba wanatumiwa na wajanja, wao wakifa masikini na vipaji vyao. Msanii mpumbavu anaachana na watu wake sahihi anajiendea huko kusikojulikana. Mwisho anajifia na kipaji chake.

Kama hukumfahamu kabla Linnah. Kama hukuwahi kumuona Barnaba na Nandy. Inakuaje uje leo kusema anatumika kwa kumuona kwenye runinga na jukwaani? Unafahamu kafikaje hapo?

Na msanii unakubali vipi maneno ya shabiki? Ambaye kakuona baada ya uwekezaji wa watu kwenye kipaji chako? Na unaamini maneno yake na kumuona ni mtu sahihi sana kwako?

Sasa kuna watu humsikiliza msanii. Wanagundua kuna kipaji na namna gani wakitumie. Ili kipaji kile kiwe mfereji wa pesa. Msanii apate na muwezeshaji huyo pia afaidike. Hao ndiyo kama marehemu Ruge. 

Hao huwakuti baa wakisifia msanii na kumnunulia bia. Huku wakijinadi kufahamiana na wadau wa sanaa. Ila majina yao utayasikia huko huko uliko. Kama siyo kwa wasanii basi walevi wa baa.

                        

Jide na Ray C, walianzia utangazaji kabla ya muziki. Wengi hawakupita huko, walimsikia tu Ruge. Wakajipa imani siku moja ya kukutana naye. Ili kila kitu maishani mwao ‘kichenji’ kwa ghafla. 

Wanakuwa na hasira ya umaarufu kabla ya mafanikio. Akili ya pesa hutengwa na akili ya ustaa tu. Tena wanakuwa tayari kwa lolote ilimradi wajulikane. 

Yaani jina likiwa kubwa kuliko viatu vyake. Akitazamwa zaidi kiumbile kuliko kusikilizwa sauti yake. Yaani ustaa ukiwa mkubwa kuliko lile wigi alilobandika kichwani kwake. Basi akili zinamruka ghafla.

Wakati kabla aliwaza umaarufu tu. Ghafla anaanza kuwaza kutajirika. Ndinga, pamba na gheto la ukweli. Hapo neno subira hugeuka ni adui yake namba wa moja kuliko yule shetani. Wanakuwa wakali na msimamo.

Neno ‘unaibiwa’ kwako linakuwa ni kipaumbele kuliko sala ya kula na kulala. Pesa ya shoo huonekana haitoshi kukidhi mavazi ya kistaa. Bata kila wikiendi na ‘auting’ na shost zake. 

Anaanza kuona hastahili maisha yale. Macho na sifa za mashabiki. Msanii anaanza kujiona mawinguni. Nidhamu hutoweka taratibu kama nywele kwenye utosi wa meneja wa Diamond. Anakuwa mwehu mwehu.

Nani wa kuendelea kuishi na msanii wa hivyo? Atakaa kando ataletwa mwingine. Kwenye foleni ya kutoka, wasanii ni wengi kuliko walioingia. Akishikwa mkono mwingine yeye angeondoka kwenye ramani.

Kutoka kutaka umaarufu tu. Baada ya ustaa, akataka pesa zaidi. Baada ya vyote kuja na kupita na anabaki yule yule wa mwanzo. Mwisho ni kujenga upendo na neno kama vile, ‘nabaniwa’. 

Ruby kabla ya kukutana na Ruge kila aliyemsikia alisema huyu balaa. Ni zaidi ya fulani na fulani na fulani. Nakumbuka baada ya kumsikiliza tu, nilisema huyu mtoto ni zaidi ya Rose Muhando. 

Sisi wengine tuliishia kumsifia tu. 

Lakini Ruge akaifanya Tanzania yote itambue uwepo wa kipaji hiki. Alimfungulia dunia na kuwa kile anachotaka. Ruby akapitiliza geti na kuwa asichotaka.

Akasonga na muziki kivyake. Ndipo akashikwa mkono binti wa Kipare. Tusiyoyajua ya nyuma tukaanza na maneno yetu. Waliotuambia Ruby anabaniwa ili Nandy awe juu yake. Tukakubaliana nao.

Kweli tukisikiliza ubora wa Ruby. Na tulishamzoea, tukaaminishana. Ni kweli Nandy ‘anakopi na kupesti’ kwa Ruby. Stori ni Ruby anabaniwa na Ruge ili kumuinua Nandy wake. Stori za ‘tauni’ tena.

Hii leo Ruge hayupo. Ruby yupo na Nandy yupo. Na siye wanoko tupo. Wa kushushuka tunashushuka na kuumbuka tunaumbuka. Kwamba suala siyo kubebwa kwa Nandy na kubaniwa kwa Ruby. 

Hii leo Nandy anabebwa na nani? Kwanini Nandy yupo pale alipo na mwenzake yuko kule aliko? Hapa ndipo unaelewa kwamba kipaji ni mosi. Kujiongoza na kujisimamia ni jambo mtambuka. 

Nandy anatupa jawabu sahihi juu ya Ruge. Stori za wanabania hawa na kubeba wale. Zilikuwa tantalila tupu kama tantalila zingine.