Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ndani ya Boksi: 2025 tutoke mitandaoni sasa

Tunaishi mitandaoni kwa kila kitu. Kama matapeli, wachunga kondoo. Na hata mashekhe wana vijiwe vyao huko. Wanasiasa na wasanii huko ndiko kwenye makazi yao rasmi.

Siye watu wa mapokeo, tumepokea kila kitu. Bahati mbaya tunaenda mbali zaidi. Kiasi cha kuondoa hata maana ya tulivyovipokea. Tunavuka lengo la waanzilishi au wabunifu wa mambo yenyewe.

Kama ni dini siye tunafika mbali kuliko wa Mashariki ya Kati. Kisiasa waliotuletea wanaishia kushangaa. Kibaya zaidi tunaanza kuwalilia hao hao tena ili watusuluhishe. Ila kwao maisha yanaendelea.

Mitandao tumeipokea kama dini na siasa. Lakini lengo la waanzilishi wa hii mitandao ni tofauti na kile kinachofanywa na sisi huku kwetu. Inatuvurugia kila kitu katika ustawi wa jamii. Tunapotoka kama jamii.

Ni maumivu makali kwa jamii yetu. Wizi, utapeli, uzinzi, mauaji na kila jambo baya. Wauza miili wamejaa mitandaoni kwa sasa, tofauti na nia ya waanzilishi. Wao mitandao ni njia kurahisisha maendeleo.

Familia zimesambaratika sababu ya mitandao. Ndoa hazijafungwa kisa mitandao. Watu wamefukuzwa au kuacha kazi kisa ni mitandaoni. Mitandao imegeuka ibilisi kamili na inatutafuna haswa.

Kila mtumiaji wa mtandao huu ni mwandishi wa habari. Mpiga picha. Mjuaji wa mambo ya watu. Anajua wa kila jambo, na zaidi kila mtu wa mtandaoni ni mtakatifu. Yaani kazi ni kukosoa wengine.

Kosa lako likasambaa mitandaoni. Kila mtu atakuongelea vibaya. Na wewe utaamini kwamba ni wewe pekee mwenye dhambi duniani. Na treni la peponi litakuacha, kumbe ni bwege tu analewa na ‘kukomenti’.

Utakuta anayekushambulia muda huo, naye yuko utupu ‘gesti’ na mke au mume wa mtu. Kwa sababu tu ana bando, ‘anakomenti’ kukuua. Kisha yeye anaendelea kutenda dhambi ya uzinzi wake.

Unaumizwa na ‘komenti’ ya pimbi mmoja. Ambaye kamaliza ungwe ya kwanza ya ngono zembe zake. Ondoka mitandaoni mwaka huu. Kuna namna nyingi za kusepa zako mitandaoni.

Mitandaoni kila mtu amekamilika. Anamtegemea Mungu. Ana sura nzuri. Ana gari zuri. Shepu nzuri. Kazi nzuri. Ndoa imara. Unaweza kuhisi ni wewe pekee uliyekosea maisha na Mungu kakutenga.

Wakati polisi wakikimbizana na makahaba wanaojiuza barabarani. Hii biashara sasa imehamia huko mitandao. Wa barabarani ni ‘pati gazeti’ nenda mjini insta, nenda na telegram.

Zamani walijiuza vibarazani. Katika maeneo maarufu, sasa wapo wazi mitandaoni. Ukahaba utahalalishwa tu siku si nyingi. Kuna kodi hupotea bure wakati wateja ni wengi zaidi kuliko bidhaa.

Tumekuwa watumwa wa mitandao kiasi cha kuanza kuwa fyatu fyatu. Wakute kina dada kwenye vyoo vya Mlimani City na pande kama hizo. Wapo ‘bize’ kupiga picha na macho matatu zao.

Kajibinua kimguu. Simu imeficha uso. Lengo lake uone yale macho matatu ya simu na siyo sura yake. Mwenye akili unajiuliza huyu yupo sawa sawa kichwani? Maisha ya mitandao inatoa akili.

Mtu anasali lakini ‘anashea’ picha mitandaoni. Unajiuliza yule mpiga picha ni malaika aliyeshuka katikati ya maombi yake? Kumbe ni mjinga mmoja kaambiwa ampige wakati wa tukio la kusali.

Mbona hampigi picha mkiwa kwa waganga kuku nyie? Mbona huna picha ukiwa kitaani ambako ndio kwenye ukweli wa kweli ya maisha yako? Kwa hiyo wewe huli chakula ‘homu’? Hii ni kwa jinsi zote.

Kuna watu wengine ‘eji goo’. Kitu pekee anachosubiri ni wajukuu wa binti yake. Lakini kila akikutana na staa yeyote anapiga picha na kuposti. Huu ni ugonjwa kama kaswende, pepopunda na tetekuwanga.

Huu mwaka tuutumie kutoka huko mitandaoni. Njoo kwenye uhalisia wenu. Tuishi tunavyostahili, maisha ya insta na kwingineko yanatilia ‘stresi’. Kuna namna ‘yanakudraivu’ uishi ili ‘upruvu’ ujinga tu.

Tuache utumwa wa mitandao kwa mwaka huu. Siyo kwamba ‘mdiliti’ peji zenu. Hapana, endelea lakini anza kuishi kiuhalisia usiendeshwe na mtandao, wewe ndio uendeshe mtandao.