Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Njia za Hamisa Mobetto kwenye Sanaa

Muktasari:

  • Hata hivyo, kwa sasa ukimtafuta Hamisa katika vitu hivyo huoni ushiriki wake hata kwa asilimia 50, ni kama sanaa ameipa kisogo na kuendelea na mambo mengine yanayofanya maisha yake kuendelea kusimama

Dar es Salaam. Kwa miaka Hamisa Mobetto anajulikana na wengi kutokana na ushiriki wake katika kiwanda cha urembo, mitindo, muziki na filamu ambapo kazi yake imemtambulisha na kumpatia mamilioni ya mashabiki.

Hata hivyo, kwa sasa ukimtafuta Hamisa katika vitu hivyo huoni ushiriki wake hata kwa asilimia 50, ni kama sanaa ameipa kisogo na kuendelea na mambo mengine yanayofanya maisha yake kuendelea kusimama.

Akiwa bado kijana mdogo, Hamisa alimtazama na kuvutiwa sana na Miss Tanzania namba tatu 2006, Lisa Jensen kutokana na kufanya vizuri upande wa mitindo na uigizaji hasa kipindi cha nyuma.

Nyota ya Hamisa ilianza kung’aa aliposhinda taji la Miss XXL After School Bash 2010, na baadaye kuibuka mshindi wa pili Miss Dar Indian Ocean 2011, nusu fainali ya Miss Tanzania 2011 na 10 bora ya Miss University Africa 2012.

Umaarufu na uzoefu alioupata katika majukwaa ya ulimbwende, ndio alioutumia kuingia katika ulimwengu wa mitindo ambapo alifanya vizuri hadi kushinda tuzo mbalimbali za ndani na kimataifa.

Baadhi ya tuzo hizo ni Swahili fashion Week Awards (Tanzania), Abryanz Style Fashion (Uganda), Starqt Awards (Afrika Kusini), Scream Awards (Nigeria), Young C.E.O Round Table (Tanzania), EAEA (Kenya) n.k.

Kutokana na umahiri wa kazi yake kama mwanamitindo, baadhi ya wasanii wa Bongofleva wakaanza kumtumia Hamisa katika video za nyimbo zao na kweli kwa kazi chache alizozifanya alizitendea haki.

Miongoni mwa waliofanya kazi na Hamisa kama video vixen ni Abdukiba, Hatuna Habari Nao (2012), Barnaba, Magubegube (2012), Diamond, Mawazo (2012), Quick Rocka, My Baby (2013), Diamond, Salome (2016), Alikiba, Dodo (2020) n.k.

Watayarishaji filamu nao wakaona kipaji chake, kati yao ni Steps Entertainment ambao walimpa nafasi katika filamu, Vocha (2014) ambayo Hamisa alicheza pamoja na waigizaji wengine kama Rammy Galis, Hemedy PhD n.k.

Kutokana na kuwa karibu na wanamuziki, naye akapata kiu ya kuimba, basi akaingia studio na kwa mara ya kwanza alisikika rasmi kupitia wimbo wake, Madam Hero (2018), kisha ikafuata Extended Playlist (EP), Yours Truly (2022).

Licha ya hayo yote, Hamisa kwa sasa ameamua kukaa kimya kama sio kuupa kisogo upande huo wa sanaa, haonekani kwenye shughuli za mitindo, hatokei katika video za muziki, hachezi filamu wala hatoi tena nyimbo zake.

Ni miaka mitano imepita tangu alipotokea katika video ya muziki ambayo ni Dodo (2020) yake Alikiba kutokea Kings Music, tangu wakati huo Hamisa hajafanya tena kazi na sidhani kama hahitajiki, bali inaweza kuwa ni mipango yake tu.

Dodo ni video iliyozua gumzo kutokana na historia ya Hamisa na Diamond ambaye ni hasimu wa Alikiba kimuziki. Ila Alikiba alidai hadi anafika Zanzibar kwa ajili ya kushuti hakujua kama Hamisa atatokea kwenye video hiyo, ni jambo lililopangwa na uongozi wake.  

Kwa mujibu wa Hamisa, kwa sasa ili aweze kutokea kwenye video ya msanii ni lazima yeye ndiye awe muhusika mkuu (main character) katika kazi hiyo ingawa haikuwa hivyo katika video ya Diamond, Mawazo (2012).

Tukija kwenye filamu ambapo alidumu kwa muda mfupi, kazi yake ya mwisho ilitoka miaka saba iliyopita, nayo ni Zero Player (2017) ambayo ilifanyika Afrika Kusini.

Upande wa muziki, huku amekaa kimya zaidi ya miaka mitatu sasa, tangu alipotoa EP yake, Yours Truly (2022), Hamisa hajatoa wimbo wowote ule kwa mashabiki wake waliompokea kwa nguvu kubwa.

Hamisa ameukimbia muziki wakati alikuwa ndio anaanza kupata mafanikio, mathalani video ya wimbo wake, Ex Wangu Remix (2021) akishirikiana na Seneta Kilaka, imeshatazamwa YouTube zaidi ya mara milioni 12.

Utakumbuka Hamisa ni video vixen na mwigizaji mwingine aliyejaribu bahati yake kwenye Bongofleva kama ilivyo kwa kina Gigy Money, Amber Lulu, Lyyn, Nai, Caren Simba, Snura, Shilole, Rose Ndauka n.k.  

Kwa sasa akiwa ameipa kisogo sanaa, Hamisa amejikita katika kazi ya ushawishi wa chapa akiwa balozi wa kampuni, taasisi, kampeni na miradi mbambali ambapo kwa sehemu kubwa anatumia mitandao ya kijamii kufanya kazi hiyo.

Huyu ni miongoni mwa mastaa wenye nguvu kubwa ya ushawishi mtandaoni akiwa na wafuasi zaidi ya milioni 12.3 Instagram akishika nafasi ya pili katika orodha ya wasanii Bongo nyuma ya Diamond mwenye milioni 18.7.