Queen Latifah: Afya yangu ni muhimu kuliko kazi yangu 

Muktasari:

  • Queen Latifah, 54, ambaye ni muigizaji pia, kwa miaka mingi amecheza uhusika wa namna mbalimbali katika filamu nyingi na muonekano wake umekuwa kielelezo chanya kutokana na kucheza nafasi sahihi kwake.

Mkongwe wa Hip Hop Marekani, Queen Latifah amesema hawezi kuruhusu maisha yasiyofaa na hatari kwa afya yake haswa linapokuja suala la kazi.

Queen Latifah, 54, ambaye ni muigizaji pia, kwa miaka mingi amecheza uhusika wa namna mbalimbali katika filamu nyingi na muonekano wake umekuwa kielelezo chanya kutokana na kucheza nafasi sahihi kwake.

Ikumbukwe akiwa na umri wa miaka 19, Queen Latifah alitoa albamu yake ya kwanza, All Hail the Queen (1989), huku mwaka 2006 akiandika rekodi kama msanii wa kwanza wa Hip Hop kupokea nyota ya heshima kutoka Hollywood Walk of Fame.
Katika mahojiano yake na People hivi karibuni, Latifah amesema katika kazi zake hasa uingizaji mara zote amekuwa anahakikisha anachukua majukumu ambayo hayahatarishi afya yake.

“Afya ni muhimu zaidi kwangu, siyo tu kuhusu kupunguza uzito au kuongezeka. Ninapotaka kupunguza uzito au kunenepa, najua jinsi ya kufanya hivyo kwa kufuata njia sahihi za kiafya.” anasema na kuongeza.

“Hivyo ikiwa ni lazima nifanye hivyo, kitu ambacho kitakuwa kibaya kabisa kwangu, basi hiyo siyo kazi yangu. Mtu mwingine ambaye tayari yupo hivyo, anapaswa kuchukua kazi hiyo. Hivyo.., ninasema hapana!.” anasema Queen Latifah.

Hata hivyo, anakiri kuwa kusema hapana siyo rahisi kila wakati, kama wanawake, huwa na tabia ya kutaka kumfurahisha kila mtu na hivyo kujikuta wakisema ndiyo hata kwa mambo ambayo walipaswa kusema hapana. Lakini ana suluhisho la changamoto hiyo baada ya majaribio mengi.

“Ninajifunza kusema hapana. Ninaenda kwenye kioo changu na kusema, hapana, hapana, hapana, hapana, kama mara 20.” anasema nyota huyo wa The Equalizer.

“Nahitaji kuwa sawa na mimi, ikiwa niko sawa basi ninahisi kama ninaweza kufanya chochote ila ikiwa siko sawa, lazima niseme kitu, kama ni wakati wa kupumzika, kuacha au kukataa hiyo kazi.” anasema Queen Latifah.
 
Latifah ambaye jina lake halisi ni Dana Owens, mzaliwa wa New Jersey, anasema amejitolea kudumisha maisha yenye afya na anajitanguliza yeye mbele kuliko kitu kingine kile anachofanya.

“Nadhani kujistahi ni sawa na kutunza gari. Huwezi kununua gari na kufikiria kuwa hautalazimika kulihudumia kwa kununua mafuta na kulifanyia marekebisho kama kubadilisha matairi. Unajua ni lazima kufanya hivyo.

“Na afya iko hivyo, lazima ujihudumie wewe mwenyewe. Unahitaji kurekebisha, unahitaji kubadilisha mafuta, lazima ujihusishe na wewe mwenyewe. Ni lazima nifanye mambo ambayo yanamsaidia sana Dana Owens.” anasema Queen Latifah.
Ikumbukwe katika muziki, Queen Latifah alivuma zaidi na kibao chake ‘U.N.I.T.Y’ 

kutoka katika albamu yake ya tatu, Black Reign (1993). Wimbo huo uliolenga kupinga unyanyasaji wa wanawake weusi nchini Marekani, ulifika 40 bora kwenye chati za Billboard Hot 100 na kushinda tuzo mbalimbali ikiwemo ya Grammy.