Rais Samia awapongeza Ramadhani Brothers kwa ushindi

Muktasari:
- Fadhili Ramadhani na Ibrahim Job, waliwashinda washindani wengine tisa waliofika fainali
Watanzania wawili maarufu kama The Ramadhani Brothers, wameibuka washindi katika shindano la kusaka vipaji la America’s Got Talent (AGT) Fantasy-Legue na kujinyakulia kitita cha dola 250,000 (Sh637 milioni), huku Rais Samia Suluhu Hassan akiwapongeza.
Kupitia ukurasa rasmi wa Rais Samia wa mtandao wa Instagram, ameonyesha kufurahishwa na ushindi wa vijana hao na kuandika: Pongezi kwa vijana wetu Fadhili na Ibrahim (The Ramadhani Brothers), kwa kuibuka washindi katika mashindano ya sanaa na burudani ya AGT: Fantasy League.
Safari yenu inaendelea kudhiirisha kuwa juhudi, nidhamu, kujituma na kujiamini ni nguzo muhimu kufikia mafanikio, mnaitangaza vyema nchi yetu na kuweka mfano kwa wengine."
Ndugu hao, Fadhili Ramadhani na Ibrahim Job, waliwashinda washindani wengine tisa waliofika fainali, wawili kati yao walikuwa wakichuana na timu ya Howie na waliobaki kwenye timu za majaji Simon Cowell, Mel B na Heidi Klum.
"Kushinda AGT ni hisia ya kushangaza zaidi ambayo hatuwezi kuelezea!" alisema Fadhili baada ya kutangazwa washindi.
"Tumekuwa katika mashindano mengine ya Got Talent duniani kote na tumefika kila fainali, lakini hatujawahi kushinda. Kushinda dhidi ya washindi wa zamani wa AGT ni baadhi ya vitendo bora zaidi kwenye sayari."
Ndugu hao ambao hutumia balansi ya mikono na kichwa, kwa mara ya kwanza walishiriki AGT msimu wa 18 mwaka wa 2023, lakini walimaliza katika nafasi ya tano licha ya matendo yao ya kusisimua na kusifiwa duniani kote.