Rekodi za Diamond Afrika zapuputishwa na Burna Boy, Tyla
Muktasari:
- Tangu Diamond alipotoa wimbo wake, My Number One (2014) akiwa na Davido wa Nigeria nyota yake kimuziki upande wa kimataifa ilianza kung'aa na kuweka rekodi nyingi Afrika ila sasa zinamponyoka moja baada ya nyingine.
Dar es Salaam. Mwimbaji wa Bongofleva, Diamond Platnumz alikuwa anashikilia rekodi kadhaa Afrika lakini mbili kubwa kati ya hizo zimefikiwa na hata kuvunjwa na Burna Boy na Tyla ambao kwa sasa wanaliwakilisha vizuri bara hili kila kona ya dunia.
Tangu Diamond alipotoa wimbo wake, My Number One (2014) akiwa na Davido wa Nigeria nyota yake kimuziki upande wa kimataifa ilianza kung'aa na kuweka rekodi nyingi Afrika ila sasa zinamponyoka moja baada ya nyingine.
Rekodi alizokuwa anajivunia ni kuwa namba kubwa YouTube akitazamwa (views) zaidi ya mara bilioni 2, pia kuwa msanii aliyeshinda tuzo nyingi za MTV Europe Music Awards (EMAs) ila sasa Burna Boy na Tyla wamepita nazo.
Utakumbuka Diamond, mshindi wa tuzo 22 za muziki Tanzania (TMA) tangu 2010 hadi 2024, ameshirikiana na wasanii wengine wa kimataifa kama P-Square, Ne-Yo, Kofi Olomide, Tiwa Savage, Rick Ross, Fally Ipupa, Alicia Keys, Jason Derulo n.k.
Burna Boy - Nigeria
Mnamo Agosti 2023 Burna Boy, mshindi wa Grammy 2021 alikwea hadi nafasi ya kwanza kama mwanamuziki aliyetazamwa zaidi (most viewed) YouTube ukanda wa kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika akimpiku Diamond.
Hiyo ilikuja baada ya Burna Boy kutazamwa mara bilioni 2.241 YouTube na kumpiku Diamond ambaye alikuwa na bilioni 2.240, ila licha ya kupoteza rekodi hiyo Diamond ameendelea kusalia kuwa kinara ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Hadi sasa Burna Boy bado anaongoza akiwa ametazamwa mara bilioni 3.06, Diamond bilioni 2.79, huku nafasi ya tatu ikienda kwa Wizkid mwenye bilioni 2.11, kisha Rema bilioni 1.86, Davido bilioni 1.78, Ckay bilioni 1.52 na Mr. Flavour bilioni 1.35.
Hata hivyo, bado Diamond, Mkurugenzi Mtendaji wa WCB Wasafi anaendelea kuongoza kwa wafuasi (subscribers) YouTube kusini mwa Jangwa la Sahara akiwa nao milioni 954, huku Burna Boy akiwa na milioni 5.06.
Ni wazi Burna Boy amekuwa na ukuaji wa kasi zaidi YouTube kuliko Diamond, hiyo ni kutokana alijiunga na mtandao huo Januari 13, 2018 wakati Diamond alijiunga Juni 12, 2011, hivyo wamepishana miaka saba ila sasa ndiye namba moja.
Licha ya Diamond kutangulia miaka saba mbele, amepitwa kutokana na kushindwa kutengeneza video nyingi za muziki zenye namba kubwa, badala yake amekuwa na video nyingi za matukio mbalimbali hadi matangazo ambazo ndizo hasa zilikuwa zinambeba.
Ikumbukwe Burna Boy alianza kuvuma Afrika baada ya kuachia ngoma yake, Like to Party (2012), albamu yake ya tano, Twice As Tall (2020) ilishinda tuzo ya Grammy huku akiweka rekodi kama msanii kwanza Nigeria kuwania Grammy mara mbili mfululizo.
Tyla - Afrika Kusini
Katika tuzo za MTV EMAs 2024 zilizofanyika Novemba iliyopita huko Manchester, Uingereza, Tyla alishinda vipengele vitatu, navyo ni Best Afrobeats Act akiwabwaga Asake, Ayra Starr, Burna Boy na Tems wote kutokea Nigeria.
Pia kuna Best African Act mbele ya Ayra Starr, DBN Gogo, Diamond na TitoM & Yuppe, na kali zaidi akashinda Best R&B akiwabwaga wakali wa dunia kama Kehlani, SZA, Tinashe, Usher na Victoria Monet wote kutokea Marekani.
Hivyo, Tyla akafikisha tuzo tatu za MTV EMAs sawa na Diamond aliyekuwa anaongoza kwa wasanii wa Afrika baada ya kushinda mbili 2015 na moja 2023 ila rekodi ya Tyla ina mvuto zaidi maana amefanya hivyo ndani ya msimu mmoja.
Na baada ya Tyla na Diamond, wasanii wengine Afrika walioshinda mara nyingi MTV EMAs, ni Burna Boy, Davido, Wizkid na D'banj, hawa wote kutokea Nigeria ambapo kila mmoja ameshinda tuzo mbili.
Tyla aliyevuma na kibao chake, Water (2023), pia aliweka rekodi kama msanii wa kwanza kike Afrika kunyakua tuzo tatu za MTV EMAs na wa pili kushinda kipengele cha Best African Act baada ya Tiwa Savage kutokea Nigeria kufanya hivyo 2018.
Ni mwafika wa kwanza kushinda Best R&B huku akiwa mwanamke wa pili duniani asiyetokea Marekani kufanya hivyo baada ya Rihanna, na kwa ujumla Tyla anaungana na Whitney Houston, Jennifer Lopez, Alicia Keys, Beyonce na Chloe.
Ikumbukwe Tyala akiwa na miaka minne tu katika muziki ameshinda tuzo 20 zikiwemo nne za South Africa Music Awards (SAMA), tatu za MTV EMAs, mbili za BET, Grammy, MTV Video Music Awards (VMAs) na Billboard ambazo ametajwa tena kuwania vipengele nane!.