Riyama: Wasanii hawana shukrani
Muktasari:
- Riyama ana historia ndefu katika sanaa hiyo ambapo amewahi kutamba na tamthilia nyingi, huku aina ya uigizaji wake unaobeba hisia za kipekee ukiwa kivutio kwa watazamaji.
Dar es Salaam. Tasnia ya filamu nchini ina waigizaji wengi na kila mmoja ana mvuto wake, lakini Riyama Ally ambaye ni mkongwe kwa sasa ni mtu na nusu!
Riyama ana historia ndefu katika sanaa hiyo ambapo amewahi kutamba na tamthilia nyingi, huku aina ya uigizaji wake unaobeba hisia za kipekee ukiwa kivutio kwa watazamaji.
Lakini, nyuma ya hilo, msanii huyo amepitia mengi. Katika mahojiano aliyofanya na mwandishi wa makala haya amesema tasnia bado inamdai
“Sanaa inanidai, Watanzania wananidai lazima nilipe deni la watu. Licha ya kufanya kazi nyingi wadau bado wana kiu, hivyo lazima nirudi kufanya kazi.
“Nilimuomba Mungu nisibadilike niwe Riyama yuleyule wala nisivae koti la umaarufu. Nawashukuru Watanzania wanapenda kazi zangu na wananisapoti sana,” amesema
Hii ni sehemu ya maneno ya mwigizaji huyo wa filamu ambaye hajaonekana kwa muda kwenye tasnia hiyo na kalithibitishia Mwananchi kwamba anatarajia kurudi hivi karibuni.
KUKODIWA KUCHAMBA
Ukiondoa uigizaji anaoufanya mwanadada huyo ni miongoni mwa wasanii ambao wana maneno na vijambo jumbe vya kimafumbo na hapa anaeleza sababu.
“Kwanza mimi ni Mzanzibari na Mzaramo. Sasa hao watu si unajua ni watu wa Pwani ambao wana nahau na ucheshi, na maneno mengi nakumbuka kipindi nina umri mdogo nilikuwa nakodiwa,” anasema na kuongeza:
“Watu wakigombana na nilivyo mfupi nikienda kuchambana naruka kama kitenesi, baada ya hapo napewa fedha naenda kununua pipi na mama akisikia ananipiga, lakini mimi nilikuwa najibizana tu na watu kutokana na namna mazungumzo yanaenda.”
Anasema kuna muda hata kwenye mitandao ya kijamii watu wanamchokoza ili tu awachambe, akikaa kimya wanamfuata hadi ‘DM’ ili awachambe wanamtia upepo ili tu wasikie maneno yake.
KITI KIPO WAZI
Sanaa ya uigizaji inakua siku hadi siku na sasa mambo ya kutoa filamu yanapotea. Huu ni wakati wa tamthilia ambazo zinarushwa katika vipindi mbalimbali vya TV tofauti, lakini kipindi kile Riyama alitamba kwa sana. Bado anadai kuwa licha ya kuwa nje kwa muda nafasi yake ipo wazi.
“Kila mmoja na aina yake ya uigizaji, kuna wasanii wengi bora ambao wanafanya vizuri hao ni wao na kuna mimi Riyama Ally sina mpinzani na hakuna kama mimi,” anasema mwanadada huyo ambaye anadai anarudi kwenye ‘nafasi yake’.
“Narudi kwenye kiti changu bado kipo wazi, hakuna aliyekikalia mashabiki wa kazi zangu na hata wale washindani zangu wajiandae ndio narudi hivyo, na najua hakuna atakayeweza kushindana na mimi, nitashindana na kivuli changu.”
Riyama pia amewazungumzia baadhi ya wasanii wasivyo na shukrani hata wanapotendewa wema.
“Siwezi kuwataja kwa sababu wasanii wengi wa Kibongo hawana shukrani, unaweza ukamtaja huyu kapita mikononi mwangu akakukataa unajikuta unaaibika,” anasema.
“Watu wanaojua wataendelea kujua hivyo, lakini siku zote sitaacha kumtaja Mohammed Zubery ‘Niva’ hajapita kwenye mikono yangu lakini nilifanya kazi yake inaitwa ‘Tabia Kuoneana’ nilimfanyia bure kabisa kipindi hicho nimekuwa maarufu sana.”
Anasema anajivunia huyo kwani hata yeye mwenyewe amekuwa akizungumza kwa kile ambacho alimfanyia huku akieleza kuwa kipindi hicho alikuwa ni maarufu na kila kazi alikuwa anaonekana.
KURUDI DARASANI
Karibuni Riyama alikuwa akitangaza redioni, lakini masuala ya kitaaluma yakamuondoa na hapa anasema hajakata tamaa, bali huko pia anarudi.
“Ithibati (ya uandishi wa habari) imeniondoa katika kipindi (alichokuwa anafanya redioni) na imenipa chachu ya kusoma, kwani natakiwa kuongeza ujuzi wa elimu. Nina mpango wa kwenda kusoma ili nirudi kazini.
“Kwa sasa nimesimama kwa kutii sheria bila shuruti, nimepokea kwa mikono miwili kwa sababu kila mtu na mipaka yake kwenye kazi hasa usipojua sheria za utangazaji wa habari,” anasema msanii huyo.
Anasema kusimama kwake kumempa chachu ya kurudi darasani ukiwa ni mpango wa kwenda kuongeza elimu kwani tayari alishajitengenezea wasikilizaji wengi.
TAARABU HADI KUIGIZA
Je unajua Riyama anajua kuimba na hasa taarabu? Msikie akizungumzia hilo. “Nilikuwa napenda kitu ambacho hakinihitaji. Nakumbuka nilikuwa Darajani na wenzangu tunaimba na kucheza.
“Naimba kwa taharuki kutokana na watu waliokuwa wananisema. Nikachagua kuachana na kuimba kwani nilikuwa nahofia kupigwa makopo jukwaani,” anasema Riyama ambaye anadai kuwa ni miongoni mwa wasanii walioonekana kwenye filamu nyingi hapa nchini.
Anasema anapenda taarabu na alikuwa anaimba hata akiwa anaoga, lakini enzi hizo mama alikuwa anamchapa kwani alikuwa akimwambia si vizuri kuimba, akimtaja Hadija Kopa kuwa ndiye msanii aliyekuwa anamvutia na nyimbo zake nyingi ndizo alikuwa akiziimba.
CHANZO UIGIZAJI
Mawazo mengi ilikuwa chanzo cha staa huyo kujiingiza kwenye uigizaji na hapa anasema: “Mwaka 2000 nilipata bahati ya kujifungua kwa kupasuliwa, lakini bahati mbaya nilimpoteza (mtoto), hivyo kutokana na upweke wa kukosa ndio ilikuwa sababu.
“Nilikuwa nakaa mwenyewe nikaona kama dunia inanielemea nikaamua kujichanganya na watu ili kuweza kupata faraja pengine nikisikia mitihani ya watu wengine nitarudi kwenye hali ya kawaida.”
Riyama anasema alikuwa anapitia changamoto ambayo ilimpa msongo wa mawazo, lakini huo ndio ulikuwa mwanzo wa kuingia kwenye tasnia ya filamu.
NSYUKA FILAMU ILIYOMTOA
Kwa Riyama ile filamu ya Nsyuka ndiyo iliyomtoa kisanii na kumfanya awe alivyo sasa.
“Nikiwa sehemu ya mafunzo uliletwa mwongozo wa filamu ya Nsyuka tukawa tunafanyia mazoezi na nakumbuka kupitia mwongozo huo nikapitishwa kuwa muigizaji,” anasema.
“Katika tafuta tafuta yangu nikahama tena kituo na kwenda Temeke Keko huko ndio nilikutana na Mussa Banzi katika maongezi nikataja mwongozo wa Nsyuka, akaniuliza naifahamia wapi nikamweleza kuwa ndio tulikuwa tunafanyia mazoezi, akaniambia yeye ndiye aliyeandika.”
Riyama anasema kipindi hicho Banzi alikuwa na kikundi cha Tamba kilichokuwa Magomeni, hivyo akawa anakwenda huko asubuhi Taswila na mchana Tamba hivyo akawa anazurura kuonyesha kipaji chake.
“Mambo yangu yalipoanza kufunguka nikiwa Tamba nilifanya filamu yangu ya kwanza ‘Fungu la Kukosa kwenye Riziki Hapakosi Fitina hii ni baada ya mambo kuanza kuwa mabaya licha ya kipindi cha mazoezi kutokuwa na shida,” anasema.
“Siku ndio tunaandaa filamu hiyo kiongozi akaniambia kuwa siku hizi naringa nawavimbia wenzangu na kuwa sitakuwa sehemu ya filamu, nafasi ikachukuliwa na wengine nikaishia kutoa chozi na kuondoka.” Anasema baada ya kushindwa kucheza filamu hiyo alipata wazo la kuandaa stori ambayo ilisaidia kufanikisha Fungu la Kukosa akicheza kama kichaa.
LICHA YA UCHIZI ALIVUTA LAKI
Pamoja na kucheza kama kichaa lakini aliambulia Sh100,000. “Elfu 50 niliwagawia wenzangu zilizobaki nilinunua mavazi ambayo nilikuwa naonekana nayo kwenye filamu yenyewe maana hayo hayakuwa yangu, mimi madera na buibui na kofia ambayo kwenye Fungu la Kukosa kuna kipande niliivaa nikawa namfukuza mtu,” anasema.
“Hivyo licha ya kufanya vizuri sana niliambulia kiasi hicho cha laki moja tu sikuwahi kuzungumzia hii taarifa na hata mwandaaji wa filamu alikuwa ananipongeza kuwa sikuwahi kulalamika juu ya kiasi kidogo cha fedha.”
Anasema hakujali kwani alifanya kazi ili atambulike auonyeshe umma kuwa ana uwezo wa kuigiza na anashukuru alifanikiwa.
HESHIMA SASA
Kwa wasanii wengi suala la kutoka huambatana na majivuno, lakini kwa Riyama kipaumbele ni heshima.
“Najivunia kutengeneza jina kubwa. Heshima imekuwa kubwa sana, nimepata nafasi ya ushehereshaji kutokana na kujulikana kwangu. Sio mtu wa mikopo tu lakini huu umaarufu nilionao nakopesheka,” anasema.
“Nimekuwa msanii mkubwa ukitaja wasanii waliofanya filamu nyingi na zilizokubalika, basi jina langu halikosekani. Ilifikia wakati kulikuwa na watu wanatumia picha zangu kwenye makava ya sinema ili zinunuliwe na mimi nikiwa sionekani kwenye kazi zenyewe.” Riyama anasema hakuwahi kujivunia umaarufu ndio maana hadi leo anaheshimiwa kwenye sanaa akijivunia kuwa ni mafanikio.