Rose Mhando alivyoweka alama kwenye kipaji cha Charugamba

Muktasari:
- Miongoni mwa wasanii hao ni Ussy Charugamba (48), anayefahamika zaidi kama Profesa Charugamba, ambaye ni msanii chipukizi wa muziki wa injili mwenye ndoto ya kuifikia dunia kupitia neno la Mungu.
Morogoro. Katika upeo wa muziki wa injili nchini, jina la Rose Mhando limeendelea kuwa alama ya ujasiri, kipaji na wito wa kipekee kwa miaka mingi. Sauti yake yenye mvuto na ujumbe wa kiroho umegeuka kuwa taa ya mwanga kwa wasanii wengi chipukizi wanaotamani kufikia kiwango chake.
Miongoni mwa wasanii hao ni Ussy Charugamba (48), anayefahamika zaidi kama Profesa Charugamba, ambaye ni msanii chipukizi wa muziki wa injili mwenye ndoto ya kuifikia dunia kupitia neno la Mungu.
Akizungumza na Mwananchi, Profesa Charugamba amesema Rose Mhando ni msanii anayemvutia na kumtia moyo kwa sababu ya kipaji chake kikubwa, unyenyekevu na moyo wa kusaidia wasanii wachanga.
“Nimewahi kuunganishwa naye katika wimbo wa Wema wa Mungu, na nilishangazwa na utu wake. Rose ni msanii wa kipekee, hana majivuno kama baadhi ya wasanii maarufu ambao hujisikia wakuu wasanii wachanga wanapowakaribia,” amesema Profesa Charugamba.
Anasema fursa hiyo ya kufanya kolabo na Rose ilikuja baada ya kuunganishwa na Katibu wa Chama cha Wanamuziki wa Injili Tanzania (Chamuita), Stella Joe. Kupitia wimbo huo, ameona mafanikio makubwa na mwitikio chanya kutoka kwa mashabiki.
“Wimbo wa Wema wa Mungu umepokelewa vizuri sana katika mitandao ya kijamii, ukiwa na watazamaji zaidi ya 36,000 kwenye YouTube, tofauti na nyimbo zangu za awali,” amesema.
Profesa Charugamba ambaye ana albamu 17, anasema yuko kwenye maandalizi ya albamu ya 18, ambapo ana mpango wa kumshirikisha tena Rose Mhando. Baadhi ya nyimbo zake zilizofanya vizuri ni Yatakuwa Sawa, Mtetezi Wangu Yu Hai, Namshukuru Mungu, Hatujawa na Tumpe Sifa.
Amesema tofauti na wasanii wengi, yeye hujitenga na mitindo ya kucheza sana kwenye video za nyimbo zake, kwa sababu anaamini kufanya hivyo kunapunguza usikivu wa ujumbe wa kiroho.
Alianza kuimba mwaka 1996 akiwa kidato cha pili katika Kanisa la EAGT Biharamulo, mkoani Kagera. Mbali na muziki, ana taaluma ya uwakili, ni mwandaaji wa filamu za kiroho, mwandishi wa vitabu, na mkufunzi wa kozi ya Ulimwengu wa Roho.
Amesema changamoto nyingi zimekuwa kikwazo katika kujitangaza zaidi licha ya kuwa na nidhamu, kipaji na juhudi, lakini kutokuwa na fedha za kutosha na ukosefu wa fursa ya kushirikiana na wasanii wakubwa kumemkwamisha.
“Wasanii chipukizi wengi wanakata tamaa mapema kwa sababu ya changamoto kama kutokuwa na fedha za studio, nidhamu mbovu, na hofu ya kuibiwa na wale wanaojitokeza kuwasaidia,” amesema.
Katika kazi zake, ameshirikiana na wasanii mbalimbali wa muziki wa injili akiwemo Faraja Mtoboba kutoka DRC, Marthin Mwanyamaki, Chacha Mussa, Prisila Lukindo na Lucy Patrick.
Kwa sasa, Profesa Charugamba anajiandaa kuzindua tuzo za Ubunifu na Ufumbuzi kwa Watoto – Mfalme Daudi 2025 zitakazohusisha watoto wa miaka 4 hadi 17 kutoka dini zote. Tuzo hizo zinalenga kukuza vipaji vya utunzi wa mashairi na ufahamu wa maadili ya kiroho kupitia Biblia na Qur'an.
“Tuzo hizi zitasaidia kuibua watoto wabunifu, waadilifu na viongozi bora wa baadaye kwa kuwaondoa kwenye hatari ya kukumbatia tabia potofu kama vile matumizi ya dawa za kulevya, ukahaba, ufisadi na wizi,” amesema.