Safari ya Domokaya na Mandojo kwenye muziki

Mwanamuziki Domokaya akizungumza na mwandishi wa makala hii, Emmanuel Msabaha nje nyumbani kwake Sinza jijini Dar es Salaam. Picha na Imani Makongolo

Walitamba na staili yao ya gitaa, kolabo ya Domokaya na Mandojo iliteka soko la muziki wa Bongofleva nchini mwanzoni mwa miaka ya 2000, hivi sasa Mandojo amejikita kwenye biashara, mwenzake amegeukia kilimo.

Hata hivyo, bado kombinesheni yao kwenye muziki imeendelea kuimarika kwa mwaka wa 22 sasa, kila mmoja akiwa na historia ya kusisimua, kufundisha, kusikitisha na kufurahisha, wiki iliyopita Mandojo alifunguka kuhusu maisha yake na safari yake ya muziki hadi kujikita kwenye biashara.

Leo Domokaya katika mahojiano maalumu na Mwananchi, ameeleza namna muziki ulivyosababisha atimuliwe shuleni, visa na mikasa aliyopitia akitaka kutimiza ndoto yake kwenye muziki hadi kuwa staa.

Mwanamuziki huyo ambaye jina lake halisi ni Precious Juma Nkoma anasema waliposikia wimbo wao wa ‘Nikupe’ umetoka, walishauriana na Mandojo waende Dar es Salaam wakiamini huko ndipo kuna pesa.

“Hatukuwa na kitu Arusha, maisha yalikuwa magumu tukasema tunakaaje hatuna hata mia wakati Dar es Salaam ngoma yetu inapigwa, twende huko huko kuna pesa yetu,” anaanza kusimulia Domokaya.

Anasema ngoma yao ilipotoka hawakuwa wanafahamu, waliambiwa baada ya kwenda hotelini walipofikia wasanii waliokuwa wamekwenda kufanya tamasha Arusha.

“Kama kawaida yetu, tulikuwa tukisikia wasanii wako Arusha, tunawaibukia (watembelea) na gitaa letu, siku hiyo kulikuwa na shoo, alikuja Profesa Jay, Mwana FA, Juma Nature na wasanii wengine, tukawaibukia.

Anasema rafiki yao huyo alikuwa ni msanii lakini wa injili ambaye alikuwa akifahamiana na Mandojo tangu wakiwa Manyoni, Singida wakati huo naye akiimba injili.

“Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kuja Dar es Salaam, awali ni ile tuliitwa na P Funky kuja kurekodi wimbo wa Nikupe, tukafikia kwa baba mdogo Kiki (RIP), Vingunguti ambako tuliibiwa kila kitu.

“Mara ya pili tulifikia kwa mshikaji (rafiki) anaitwa James Farijala, alikuwa anatukubali, aliona bora alale chini kutupisha sisi, tuliishi kule eneo moja panaitwa bonde la Sukita, tukawa tukienda kushinda kwa kina Albert Mangwea, Kijitonyama, huko ndipo tulipata konekisheni zaidi.”

Anasema wakati huo ngoma yao ya Nikupe ilikuwa inabamba mjini, lakini wao hawana kitu, wakawa wanapanda daladala la Buguruni-Mwananyamala, wanashuka kwa Mama Zacharia na kukatisha chocho za Makumbusho kwa miguu hadi wanaibukia Kijitonyama kwa kina Mangwea.

“Tulikuwa wataalamu wa chocho zote za Kijitonyama, hadi kufika kwa kina Mangwea kwenda kushinda kule ambako tulikutana na wasanii mbalimbali, ikawa rahisi kuunganishwa na wadau wengine, lakini hatukuwa na mawasiliano hivyo tukanunua simu moja tukawa tunashea (shirikiana) kuitumia.

Huku akicheka, Domokaya anasema: “Simu ilikuwa inatunzwa na mkubwa (Mandojo), yeye ndiye alikuwa anakaa nayo, mimi niliona sawa tu, kwanza nilikuwa ni mdogo wake.

Anasema ile simu iliwarahisishia na kuanza kupata kazi mbili tatu zilizowapa pesa, na kushauriana na Mandojo wakapange vyumba vyao ili waanze kujitegemea na kumpunguzia mzigo rafiki yao aliyewapokea na kukubali waishi kwake.

“Tulipanga vyumba viwili na sebule, tukapata pesa na kununua vitu vya ndani, hadi ikafikia hatua tukamudu sasa kupanga nyumba nzima.”

Wiki iliyopita, Mandojo alieleza namna Ruge alivyowapa shoo ya kwanza wakaingiza kila mmoja Sh600,000 ambayo ilikuwa ni pesa nyingi kwao wakati huo na kununua vitu sare, Domokaya anasema hadi nguo walikuwa wakivaa saresare.

“Tulikuwa tukishauriana kabla ya kufanya kitu chochote, kwangu Mandojo ni bro (kaka) amenipita miaka mitano, lakini aliniheshimu na kunisikiliza.

“Tangu tumekutana Arusha mwanzoni mwa mwaka 2000 tumeishi katika misingi ya kuheshimiana na kusikilizana, sio kama hatutofautiani, la hasha kuna wakati tunapishana kauli, lakini hilo halitutoi kwenye msingi wa kufanya kazi,” anasema.

Aliyewaunganisha Mandojo, Domokaya huyu hapa

Akiwa mwanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya Sekondari Sekei, jijini Arusha ndipo Domokaya alikutana na Mandojo.

“Mandojo alikuwa akiishi kwa kaka yake, ambaye alipanga nyumba moja na rafiki yangu aliitwa Furaha Haleluya ambaye huyu ndiye alikuwa kiungo cha mimi kufahamiana na Dojo (Mandojo).

“Nilipokuwa nikienda kwao kumpitia twende shule namkuta Mandojo anapiga gitaa, nilipenda, lakini wakati huo tayari nilikuwa nimeingia kwenye harakati za muziki muda mrefu kidogo, lakini sikuwa najulikana,” anasema.

Anasema alianza kujifunza muziki mwanzoni mwa miaka ya 1990, wakati huo akisoma Shule ya msingi Hananasif, Kinondoni, Dar es Salaam.

“Hadi nahitimu darasa la saba nilikuwa nachana (ana rap), lakini kisirisiri, nilijifunza kwa kaka yangu, David Nkoma aliyekuwa mwanamuziki ingawa sasa ni produza yuko Arusha.

“Kipindi hicho kaka yangu alikuwa kwenye kundi na TID na Digo Jango linaitwa Black Gangstars, mazoezi walifanyia nyumbani, wakijirekodi wanapomaliza na kuondoka mimi nachukua daftari la kaka na kuanza kukariri mistari bila kuonekana.

“Wakati huo wanachana kwa lugha ya Kiingereza, nilikuwa nakariri mistari hata lugha siifahamu, mwaka 1998 mama alipata kazi Arusha, tukahamia kule nikaenda kuanza kidato cha kwanza, kaka yangu alibaki Dar es Salaam.

“Siku amekuja Arusha, alinikuta tayari nimeiva, alikuja kugundua siku hiyo alipokuwa akichana, kila akipiga nipo naye akabaki anashangaa, hakuwahi kujua kama nachana, nikampa na mashahiri yangu ambayo nimeandika mwenyewe.”

Chanzo cha jina la Domokaya

Mwenyewe anajiita Domo, akifupisha jina lake la utani la Domokaya ambalo anasema alipoulizwa na kaka yake katika fani yake ya usanii anajiita nani, hakupepesa macho na kumwambia yeye ni Domokaya.

“Bro (kaka) alicheka akaniambia hilo jina baadaye utakuja ulikatae, lakini wakati ananiambia hivyo, tayari Arusha wengi walinifahamu kwa jina hilo na nilishaanza kuimba kwenye matamasha ya kule.

“Niliona mwanzoni nilijiita majina ya kiulaya ulaya lakini hayakuwa na nguvu, ila la Domokaya ilikuwa ni rahisi mtu yeyote kulizoea.

“Domokaya ni neno nilijifunza darasani nikiwa sekondari, kwenye somo la Kiswahili, tulifundishwa kuwa ni mtu mwenye maneno mengi, nililipenda, kuanzia pale nikaanza kujiita hivi maneno mengi, nikakutana nalo, domo ni mtu anayeongea sana, nililichukua kama lilivyo.”

Anasema wakati huo, familia nyingi hazikuamini katika muziki, hasa wa Bongofleva, kila aliyeingia huko alionekana mtukutu.

“Kilikuwa ni kipindi kigumu, kwa wazazi wengi kuwaruhusu watoto wao kufanya muziki, nilipitia vikwazo vingi, shuleni na hata nyumbani, lakini niliamini huko ndiko kuna mafanikio yangu.

“Sikutaka kikwazo chochote kikatishe ndoto zangu, mama hakutaka kunisikia kabisa kwenye muziki, ila nilipata ujasiri nikamwambia muziki ni ndoto yangu hivyo wewe nisapoti tu.

“Unapokutana na chalenji zinakuwa ni zako peke yako, lakini unapofanikiwa mafanikio yanakuwa ni ya wengi, mimi nakumbuka nilipokuwa maarufu bi mkubwa (mama yake) alikuwa akinitambulisha kila sehemu.

“Hadi kanisani tukienda anawambia watu, huyu mwanangu anaitwa Domokaya yuko na mwenzake Mandojo, hadi stendi wakati mwingine anataka kukutambulisha, wakati mwingine hadi namwambia kausha basi,” anasema.

Domokaya anasema akiwa Arusha anaishi kwa uhuru zaidi tofauti na Dar es Salaam ambako alizaliwa mwanzoni mwa miaka ya 1980. Anasema katika maisha ukijua unahitaji nini au kuwa nani na ukaweka nia kila kitu kinafunguka.

“Nakumbuka nilikuwa napewa adhabu, ikafikia hatua nikazoea kwamba nikirudi nyumbani nitachapwa, basi, lakini mimi muziki siachi, ikafikia hatua nikawa sipigwi tena, ila naambiwa ikifika saa 5 usiku hujarudi tunafunga mlango.

“Wakati mwingine unakwenda kwenye tamasha, unakwama kupata usafiri wa kurudi nyumbani nalazimika kulala kwa kina Mandojo, nikirudi nyumbani ni kesi, unasemwa, lakini wala sikuchukulia kama hilo ni tatizo la kunitoa kwenye reli ya muziki.

“Nitasemwa leo, kesho likitokea tamasha jingine nakwenda, unachosukuru Mungu tu ni kwamba unarudi salama.”

Anasema alitaka kuwa hivyo alivyo, aliacha kila kitu kwa ajili ya muziki, akiamini akifanya wimbo mmoja tu kila mtu atajua uwezo wake.

“Nikiwa sekondari nilikuwa nawaambia wanafunzi wenzangu shuleni, mimi nitakwenda Dar, huko nitapiga wimbo mmoja mkali na hapo kila mtu atanijua.

Anasema akiwa kidato cha tatu kuna mwanafunzi mwenzake wa kike alikuwa na sauti kama Celine Dion, mara nyingi walipenda kuimba pamoja.

“Ilikuwa tukianza kuimba hadi darasa linasimama, kifupi tulikuwa na vipaji, nikawa na ndoto kubwa sana kwenye muziki, kuna wakati tulionekana kama tunawapotosha wanafunzi wale wapole ambao walikuwa na vipaji na kutaka kujiunga na sisi kwenye muziki,” anasema.

 Itaendelea kesho, Domokaya akieleza namna alivyofukuzwa shule sababu ya muziki na alivyokomaa nao hadi ukamtoa.