Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shakira anavyoitumia Afrika kuishagaza dunia!

Muktasari:

  • Shakira, mshindi wa tuzo 15 za Latin Grammy, tayari ametoa nyimbo tatu maalum za michuano hiyo huku mbili kati ya hizo akishirikiana na wanamuziki kutokea Afrika, kitu ambacho ni bahati kwa timu ya taifa ya Hispania huku kikiibua mambo mengine ya kushangaza

Marekani. Mwimbaji wa miondoko ya Pop na Rock ambaye pia ni Malkia wa Latin Music, Shakira, 49, ameendelea kujizoelea sifa na umaarufu mkubwa kutokana na kile ambacho amekifanya katika fainali za Kombe la Dunia tangu mwaka 2006 nchini Ujerumani.

Shakira, mshindi wa tuzo 15 za Latin Grammy, tayari ametoa nyimbo tatu maalum za michuano hiyo huku mbili kati ya hizo akishirikiana na wanamuziki kutokea Afrika, kitu ambacho ni bahati kwa timu ya taifa ya Hispania huku kikiibua mambo mengine ya kushangaza.

Mzaliwa huyo wa Colombia, msimu huu ametumbuiza katika ufunguzi wa Kombe la Dunia la FIFA 2026 katika uwanja wa Mexico City, na vilevile amefanya hivyo katika fainali iliyopigwa uwanja wa MetLife nchini Marekani.

Kwa ujumla Shakira ametumbuiza katika fainali nne za Kombe la Dunia akiwa ndiye mwanamuziki pekee mwenye rekodi hiyo. Alitumbuiza fainali zilizofanyika Ujerumani 2006, Afrika Kusini 2010, Brazil 2014, na hizi zilizomalizika ambazo zimefanyika Marekani, Canada & Mexico 2026.

Huko Ujerumani alitoa burudani katika mchezo wa fainali uliokutanisha Ufaransa dhidi ya Italia walioibuka mabingwa, mbele ya umati mkubwa uliojitokeza katika uwanja wa Olympic jijini Berlin, Shakira aliimba wimbo wake, Hips Don't Lie (2006).

Alitumbuiza pamoja na Wyclef Jean kutokea Haiti ambaye ameshirikishwa katika wimbo huo ulioshika nafasi ya kwanza katika nchi 18 ikiwemo Marekani kupitia Billboard Hot 100, huku ukijumuishwa katika albamu yake ya saba Shakira, Oral Fixation, Vol. 2 (2005).

Mwaka 2010, Shakira alitoa wimbo wake wa kwanza rasmi wa Kombe la Dunia ambao ulitumika katika michuano hiyo ambayo ilifanyika nchini Afrika Kusini.

Wimbo huo, Waka Waka (This Time for Africa) (2010), alishirikiana na bendi ya Freshlyground ya nchini humo, na hadi sasa ndio wimbo wa Shakira wenye mafanikio makubwa zaidi katika Kombe la Dunia na YouTube ambapo video yake imeshatazamwa (views) mara bilioni 4.6.

Shakira alitumbuiza na bendi hiyo katika mchezo wa ufunguzi na ule wa fainali ambao ulipigwa uwanja wa Soccer City ukiwakutanisha Uholanzi na Hispania walioibuka mabingwa kwa ushindi wa goli 1-0, ikiwa ni mara yao ya kwanza kushinda taji hilo.

Jambo kama hilo limekuja kujirudia tena mwaka 2026, ambapo Shakira ametumbuiza katika ufunguzi wa Kombe la Dunia na mechi ya fainali iliyowakutanisha Argentina dhidi ya Hispania ambao wameibua mabingwa kwa ushindi wa goli 1-0.

Vilevile wimbo aliyotumbuiza Shakira, Dai Dai (2026), ameshirikiana na mwanamuziki kutokea Afrika ambaye ni Burna Boy wa Nigeria, na katikati show hiyo ya mwisho pia alishirikiana na kundi la watoto wenye vipaji vya dansi kutokea Uganda, Ghetto Kids.

Pia zingatia kuwa mechi ya ufunguzi wa Kombe la Dunia 2010 ambapo Shakira alitumbuiza, iliwakutanisha Afrika Kusini dhidi ya Mexico, halafu bingwa akaja kuwa Hispania. Na ufunguzi wa Kombe la Dunia 2026 ambapo pia Shakira alitumbuiza iliwakutanisha Afrika Kusini na Mexico, na bingwa akawa Hispania.

Hivyo hadi sasa kila ambapo Shakira ametoa wimbo wa Kombe la Dunia na kuwashirikisha wanamuziki kutokea Afrika, basi timu ya taifa ya Hispania imefika fainali na kupata ushindi wa goli 1-0, huku mwanamuziki huyo akiwaburudisha.

Ikumbukwe kipindi anatayarisha video ya wimbo wake, Waka Waka (This Time for Africa) (2010), ndipo Shakira alikutana na kupendana na mchezaji wa zamani wa Hispania, Gerard Pique ambaye alikuwepo katika kikosi kilichoshinda Kombe la Dunia 2010.

Uhusiano wa Shakira na Pique ulidumu kwa takribani miaka 10 ambapo walijaliwa kupata watoto wawili wa kiume, Milan (2013) na Sasha (2015).

Hii ya juzi ilikuwa mara ya tatu kwa Shakira kutumbuiza fainali ya Kombe la Dunia kupitia wimbo wake rasmi wa michuano hiyo, mara ya kwanza alifanya hivyo nchini Afrika Kusini.

Mara ya pili alifanya hivyo nchini Brazil kupitia wimbo wake, La La La (2014) ambao alimshirikisha mwanamuziki maarufu kutokea nchini humo, Carlinhos Brown.

Shakira, mshindi wa Grammy mara nne, alitumbuiza wimbo huo mbele ya mashabiki 74,738 uliojitokeza katika uwanja wa Maracana jijini Rio de Janeiro kushuhudia fainali kati ya Argentina na Ujerumani walioibuka mabingwa kwa ushindi wa goli 1-0.

Hapa pia yanaibuka mambo mawili ya kushangaza, mosi: fainali zote tatu za Kombe la Dunia ambazo Shakira ametumbuiza kupitia nyimbo zake rasmi za michuano hiyo zimemalizika kwa matokeo ya 1-0, vilevile Argentina imepoteza fainali zote mbili ambazo Shakira alitumbuiza!.

Kwa sasa Shakira anaendelea kuvuma na kolabo yake na Burna Boy, Dai Dai (2026) ambayo imekuwa wimbo wa nne rasmi wa Kombe la Dunia kuingia kwenye chati ya Billboard Hot 100.

Nyimbo rasmi za Kombe la Dunia zilizoingia Billboard Hot 100, ni The Cup of Life (1998) wake Ricky Martin, Waka Waka (This Time for Africa) (2010) wake Shakira na Freshlyground, We Are One (Ole Ola) (2014) wake Pitbull, Jennifer Lopez na Claudia Leitte, na sasa Dai Dai (2026) wake Shakira na Burna Boy.

Hapo Juni 18, Shakira aliwashukuru mashabiki baada ya video ya wimbo 'Dai Dai' kufikia rekodi ya kutazamwa (views) zaidi ya mara milioni 100 YouTube, na sasa umefikia milioni 504. Video hiyo imewaonyesha wachezaji maarufu kama Lionel Messi, Kylian Mbappe na Erling Haaland.

Ikumbukwe 'Dai Dai' ni wimbo unaohimiza umoja duniani kote kupitia soka ukiwa umeandikwa kwa lugha tano ambazo ni Kiingereza, Kihispania, Kiitaliano, Kifaransa na Kijapani, huku ukichanganya ladha mbalimbali za muziki kama, Dance Pop, Reggaeton na Afrobeats, muziki unaowakilisha bara la Afrika.