Siku ya kifo cha Sokoine
Muktasari:
- Tulikuta meneja wetu Mzee Masumbuko, aliyekuwa katangulia alikwishatutafutia vyumba vya kulala katika nyumba ya kulala moja kubwa Katikati ya jiji la Shinyanga. Tulitegemea kuanza onyesho letu la kwanza siku ile ile, kulikuwa na kila dalili kuwa mambo yangekuwa mazuri kwa siku ile.
Dar es Salaam. Tarehe 12 April 1984, kundi zima la Orchestra Mambo Bado lilitua katika mji wa Shinyanga likitokea Dar es Salaam kwa treni. Nia ya safari hiyo ilikuwa kuzunguka wilaya zote za Kanda ya Ziwa kuporomosha muziki ili kupata riziki. Mimi nilikuwa mmoja wapo wa wanamuziki wa bendi hiyo.
Tulikuta meneja wetu Mzee Masumbuko, aliyekuwa katangulia alikwishatutafutia vyumba vya kulala katika nyumba ya kulala moja kubwa Katikati ya jiji la Shinyanga. Tulitegemea kuanza onyesho letu la kwanza siku ile ile, kulikuwa na kila dalili kuwa mambo yangekuwa mazuri kwa siku ile.
Matangazo yalikuwa yamebandikwa kwenye kuta na nguzo za umeme sehemu mbalimbali za mji wa Shinyanga, na hali ya kuonyesha kuwa watu walikuwa na taarifa ya ujio wetu ilikuwa dhahiri.
Wakati huo Orchestra Mambo Bado, ilikuwa ikiongozwa na Tchimanga Kalala Assossa jina lake la umaarufu lilikuwa Mtoto Mzuri. Bendi yetu ilikuwa ni moja ya bendi zilizokuwa pendwa wakati huo, mtindo wetu ulikuwa ni Bomoa.
Neno hili lilitokana na wimbo wa Bomoa Tutajenga Kesho, wimbo ambao baadaye kwa sababu ambazo mpaka leo sizijui, ulikuja kupigwa marufuku kupigwa redioni na Umoja wa Vijana wa Mkoa wa Dar es Salaam wakati ule. Tukawa tunaupiga dansini tu.
Orchestra Mambo Bado ilikuwa na watu ishirini hivi, Tchimanga Assossa kiongozi na mwimbaji. George Mzee muimbaji, Lucas Faustin muimbaji, Jenipher Ndesile muimbaji, Athumani Cholilo muimbaji, John Kitime muimbaji, Likisi Matola mpiga gitaa la bezi na katibu wa bendi, Andre Milongo akipiga gitaa la second solo, Huluka Uvuruge na Kazembe wa Kazembe wapiga gitaa la solo, William Maselenge akiwa kwenye gitaa la rhythm, Sadi Mnala alikuwa akizikung’uta drums. Kulikuweko na wacheza show wanne, mafundi mitambo watatu na mweka hazina mmoja na meneja wa bendi.
Ilikuwa ni muda wa saa kumi hivi habari zilipoanza kuzagaa kuwa imetangazwa radioni kuwa nchi imepata msiba mkubwa sana. Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine amefariki katika ajali ya gari jirani na Morogoro.
Kwanza ilikuwa ni mshtuko, halafu akili ilipotulia tulijua kuwa na sisi kama bendi tunaingia kwenye tatizo kubwa sana, enzi hizo hakukuwa na wadhamini, hivyo tulikuwa tumeweza kukusanya nauli ya kuja tu mpaka Shinyanga, na fedha ya kula ya siku moja tu, tulikuwa tunategemea kupiga dansi ili kuweza kulipa malazi ya siku hiyo na kupata fedha ya kula na kuendelea na safari kesho yake, hivyo kwa tangazo la msiba ule mkubwa, tulijua mambo yote yamebadilika.
Kwanza tulirudisha vyumba vyote vya kulala mara moja na kubaki na viwili tu kimoja walipewa wasichana tulioambatana nao, sisi wengine wote ikalazimu tuhamishie mizigo yetu chumba kilichobaki.
Tulimtafuta Afisa Utamaduni na kutafakari kama dansi lingewezekana kupigwa siku ile, na kama halitapigwa nini hatima ya waanamuziki hawa 20 wageni kutoka Dar es Salaam?
Kukosekana kwa mawasiliano bora enzi hizo kulisaidia kutoa uamuzi kuwa kwa siku ile dansi lipigwe kwani kulikuwa hakujafika taarifa ya amri yoyote kuzuia burudani, Afisa Utamaduni akaruhusu tupige dansi ili tuweze kupata nauli ya kurudi Dar es Salaam.
Tulipiga dansi ambalo lilipata umati mkubwa tukaweza, kulipa gharama za malazi usiku ule na kupata nauli ya kurudi Dar es Salaam. Maombolezo yalichukua siku ishirini na mmoja, na kwa kuwa burudani zilizuiliwa kwa siku hizo, kilikuwa kipindi cha njaa kubwa kwa wanamuziki.
Amri za kuzuiwa kwa burudani zimeshawahi kutolewa tena baada ya kufariki kwa Baba wa Taifa mwaka 1999, tena zuio hilo lilikuwa refu zaidi, lilikuwa miezi mitatu.
Pamoja na hali hiyo, wanamuziki walitunga nyimbo nyingi za kuomboleza msiba huo na kuzirekodi, wafanyabiashara walipata faida kubwa kwa kuuza kanda za nyimbo hizo, lakini ulikuwa wakati mgumu kwa wanamuziki ambao njia yao pekee ya kuishi na familia zao ni kwa kufanya maonyesho. Kuna kumbukumbu za kampuni iliyopata shilingi 250,000,000/- kwa kuuza kanda za nyimbo za kumuaga Mwalimu.
Katika kipindi hicho cha maombelezo, muziki uliendelea kusikika, vyombo vya utangazaji vilipiga muziki, na muziki uliendelea kusikika katika mabaa na kumbi mbalimbali za starehe na kwenye vyombo vya usafiri wa umma, michezo imeendelea kufanyika, wanamuziki peke yao ndio waliozuiwa kufanya maonyesho!
Hakika lilikuwa jambo la kufikirisha.