Siri ya vituko vya waalikwa harusini
Muktasari:
- Video hizo ambazo huchapishwa katika kurasa mbalimbali za washereheshaji zimeendelea kuzua mijadala kwa baadhi ya watu kutopendezwa nazo na kwani huwafanya wasiwe huru kusherehekea kwa kuhofia kusambazwa mitandaoni.
Dar es Salaam. Si ajabu kukutana na picha ama video za wageni waalikwa kwenye sherehe zikiwa zinasambaa kwenye mitandao ya kijamii. Huku baadhi zikiwa na maudhui ya kudhalilisha na nyingine kuchekesha.
Video hizo ambazo huchapishwa katika kurasa mbalimbali za washereheshaji zimeendelea kuzua mijadala kwa baadhi ya watu kutopendezwa nazo na kwani huwafanya wasiwe huru kusherehekea kwa kuhofia kusambazwa mitandaoni.
Akizungumza na Mwananchi MC Big Chriss kuhusiana na tabia hiyo inadaiwa kutumiwa kama njia ya kutafuta like, comment na followers anasema huo ni ukosefu wa weledi kwa baadhi ya washereheshaji.
MC Big anasema katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la watu wanaojiingiza kwenye kazi ya ushereheshaji bila kufahamu misingi ya taaluma hiyo, jambo linalochangia baadhi yao kufanya makosa yanayoweza kuwaingiza kwenye migogoro ya kisheria.
“Wapo wenye weledi na wasio na weledi. Wengine wameingia kwenye kazi hii bila kujua masharti na maadili yake.
“Unakuta mtu amekwenda kwenye sherehe ya ndugu au rafiki yake, amefurahia, amekunywa na kucheza kwa uhuru, halafu mtu mwingine anachukua video hiyo na kuisambaza mtandaoni. Hilo si jambo sahihi,” anasema.
Alisema kupitia vyama vya washereheshaji vinavyotambuliwa nchini, ikiwamo KIKIMA cha Mafanikio na SAA, Ma-MC wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya mara kwa mara kutoka kwa wataalamu mbalimbali, yakiwamo mafunzo kuhusu sheria, maadili na namna ya kuendesha shughuli za kijamii kwa kuzingatia haki za wahusika.
Kwa mujibu wa MC Big, moja ya mambo muhimu anayoyazingatia kabla ya kuchapisha picha au video za shughuli anazosimamia ni kupata ridhaa ya wahusika husika.
“Mimi kabla ya kuingia ukumbini huwa nazungumza na wenye shughuli. Nauliza kama wanaruhusu picha na video zao kuwekwa kwenye mitandao ya kijamii. Wapo ambao hawapendi kabisa maisha ya mitandao, hivyo ni lazima kuheshimu uamuzi wao,” anasema.
Aliongeza kuwa licha ya watu wengi kupenda kuonekana kwenye mitandao ya kijamii, ni muhimu kuhakikisha maudhui yanayochapishwa yanazingatia maadili na hayawezi kumkwaza mhusika baadaye.
Akizungumzia madai kuwa baadhi yao hutumia picha na video za wageni kutafuta umaarufu au kuongeza idadi ya watazamaji kwenye kurasa zao, MC Big anasema tabia hiyo ipo na imekuwa ikikemewa mara kwa mara ndani ya vyama vya washereheshaji.
“Wapo wanaorusha picha za aibu wakiamini zitapata maoni mengi zaidi. Hiyo si sahihi na huwa tunawakumbusha mara kwa mara kuwa vitendo hivyo vinaweza kuwaingiza kwenye matatizo makubwa ya kisheria,” anasema.
Kwa upande wake, MC Big alisema hajawahi kupokea malalamiko kutoka kwa wateja wake kutokana na maudhui anayochapisha kwa kuwa amekuwa akifuata sheria na miongozo anayopatiwa kwenye semina mbalimbali.
Alionya kuwa MC atakayechapisha picha au video ya mtu bila ridhaa yake anaweza kujikuta akikabiliwa na hatua za kisheria, huku akisisitiza umuhimu wa washereheshaji kujiunga na vyama vyao ili kupata elimu na taarifa za mara kwa mara kutoka serikalini na taasisi husika.
Kwa upande wake, MC Luvanda kutoka Mbeya anasema watu wengi wanaohudhuria sherehe huenda kwa lengo la kufurahi na wakati mwingine mazingira ya sherehe yanaweza kusababisha mtu kufanya jambo ambalo asingependa lionekane hadharani.
“Unaweza kukuta mtu amecheza sana, akaanguka, akateleza au hata nguo ikaleta changamoto fulani. Ukichukua picha au video ya aina hiyo na kuiweka mtandaoni unakuwa umemvua nguo mbele ya jamii,” anasema.
Anasema madhara ya kitendo hicho yanaweza kuwa makubwa kwa mhusika, hasa ikiwa ni mtu mwenye nafasi ya uongozi, mfanyabiashara au mtumishi wa umma anayeheshimika katika jamii.
“Heshima yake inaweza kuathirika kazini, kwenye familia na hata kwa watoto wake. Ndiyo maana kabla ya kuchapisha chochote ni lazima kujiuliza kama ungekuwa wewe ungependa maudhui hayo yawekwe hadharani,” alisema.
MC Luvanda anasisitiza kuwa si kila picha au video inayopatikana kwenye shughuli inapaswa kuwekwa mtandaoni, huku akiwataka washereheshaji kuzingatia utu na heshima ya watu badala ya kukimbilia kutafuta umaarufu wa muda mfupi.
Washereheshaji hao wamemaliza kwa kuwataka wenzao kuacha mara moja tabia ya kusambaza picha na video zinazoweza kuwavunjia heshima watu. Wakisisitiza kuwa kazi ya ushereheshaji inapaswa kwenda sambamba na kulinda utu, faragha na heshima ya wahudhuriaji wa shughuli mbalimbali.
Kauli za Wananchi
Asha Mrema, mkazi wa Dar es Salaam, alisema tabia ya kusambaza picha na video za watu bila idhini yao imekuwa chanzo cha usumbufu kwa baadhi ya wahudhuriaji wa sherehe mbalimbali.
Anasema si kila mtu anayehudhuria hafla anapenda maisha ya mitandao ya kijamii, hivyo ni muhimu kwa wanaorekodi na kusambaza maudhui hayo kuheshimu faragha za wengine.
“Wakati mwingine mtu anakuwa amekwenda kufurahi tu na ndugu au marafiki zake, lakini baadaye anakuta picha au video yake imesambazwa kwenye mitandao bila ridhaa yake. Hilo linaweza kumletea usumbufu mkubwa kwenye familia, kazi au hata kwenye jamii inayomzunguka,” anasema.
Kwa upande wake, Baraka Msuya, mkazi wa Morogoro, amewataka washereheshaji na wadau wengine wa burudani kuzingatia maadili wanapochapisha maudhui yanayotokana na shughuli wanazosimamia.
Anasema kukimbilia kutafuta umaarufu au watazamaji wengi kupitia picha za aibu za watu ni jambo linaloweza kuharibu heshima na taswira ya wahusika husika.
“Ni muhimu kila anayeshughulika na picha na video kutambua kuwa nyuma ya kila picha kuna maisha ya mtu, familia yake na hadhi yake katika jamii. Kabla ya kuposti chochote ni vyema kujiuliza kwanza kama maudhui hayo yatamjengea au yatamharibia mhusika,” anasema.
Kauli ya Basata
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bwana Edward Buganga alisema washereheshaji wanapaswa kuzingatia miongozo na maadili ya kazi zao, akisisitiza kuwa taasisi hiyo haitasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekiuka taratibu zilizowekwa na sheria.
Akizungumzia mjadala unaoendelea kuhusu uchapishaji wa picha na video zinazodaiwa kuwavunjia heshima baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii, Buganga anasema washereheshaji wana taratibu zao za utendaji huku akibainisha kuwa wapigapicha na watengeneza video nao wanasimamiwa na mamlaka nyingine husika katika sekta ya filamu.
Anasema kwa upande wa picha za kawaida na picha mnato, BASATA ina miongozo ya maadili iliyo wazi inayosisitiza kulindwa kwa utu na heshima ya kila mtu.
“Hairuhusiwi kumdhalilisha mtu, kumvunjia heshima au kutweza utu wake. Atakayefanya hivyo tutamchukulia hatua kwa mujibu wa sheria na taratibu za Baraza,” alisema.
Buganga alieleza kuwa kila MC anatakiwa kusajiliwa na BASATA na kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia maadili ya taaluma pamoja na haki za watu anaowahudumia.
Anasema pale ambapo MC anabainika kukiuka taratibu, BASATA huwaita kwa mazungumzo na wakati mwingine kuchukua hatua za kinidhamu ikiwemo kuwasimamisha kufanya shughuli zao.
Aidha, anasema wananchi wanaokumbana na changamoto zinazohusiana na maudhui yanayokiuka maadili wanaweza kuwasilisha malalamiko yao BASATA kwa ajili ya kufanyiwa kazi kupitia mifumo rasmi ya kisheria na kiutendaji.
Amesisitiza kuwa si kila shauri linalopelekwa BASATA huwekwa hadharani kwani baadhi hushughulikiwa kwa kuzingatia taratibu za kitaaluma na usiri unaohitajika.
Buganga alibainisha kuwa sheria inayosimamia masuala ya sanaa nchini ilitungwa mwaka 1984 na kufanyiwa maboresho mwaka 2019 kwa lengo la kuifanya sekta ya sanaa kuwa chanzo cha kipato kwa Watanzania huku ikijenga mazingira bora na salama ya utekelezaji wa shughuli za kisanaa.
Aliwataka washereheshaji na wadau wengine wa sanaa kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia miongozo iliyowekwa ili kulinda maadili na heshima ya jamii.