Tuzo za Muziki (TMA) kutolewa Juni 15

Muktasari:

  • Akizungumza na waandishi wa habari katibu mtendaji wa baraza hilo  Dk. Kedmon Mapana, amesema TMA chini ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Damas Daniel Ndumbaro (Mb), imefanya uteuzi wa kamati ya wajumbe ambao watahusika na mchakao wa tuzo hizo ambao ni David Minja, Mwenyekiti wa Kamati, Christine ‘Seven’ Mosha Makamu 

Baraza la Sanaa Taifa (Basata), limetangaza kuwa Tuzo za Muziki Tanzania ‘Tanzania Music Awards’ (TMA), 2023/2024, zinatarajiwa kufanyika Juni 15 mwaka huu, huku kauli mbiu ikiwa ni "Kubadilisha tasnia ya Tuzo za Muziki Tanzania na Afrika kwa namna ambavyo haijawahi kutokea". 

Akizungumza na waandishi wa habari katibu mtendaji wa baraza hilo  Dk. Kedmon Mapana, amesema TMA chini ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Damas Daniel Ndumbaro (Mb), imefanya uteuzi wa kamati ya wajumbe ambao watahusika na mchakao wa tuzo hizo ambao ni David Minja, Mwenyekiti wa Kamati, Christine ‘Seven’ Mosha Makamu 

Mwenyekiti, Mtumwa Mrisho akiwa pia katibu, pia wamo  wajumbe Chris Torline, Natasha Stambuli, Paul Matthysse (P-Funk Majani), Jandre Louw, Lloyd Leslie na Kelvin Msangi. 
Ili kuzifanya tuzo hizo kuwa za kimataifa zaidi, TMA itaandaa usiku wa ‘TMA prelude’ ambao utafanyika Juni 14, ikiwa ni siku moja kabla ya usiku wa tuzo kwa lengo la kuheshimisha mashujaa wa tasnia ya muziki.

Katika kuzingatia kupata washindi wanaostahili, kamati hiyo italenga  zaidi kupata maoni na ushauri wa wadau wa muziki Tanzania na Afrika kwa ujumla, huku tuzo hizo zikitarajiwa kutolewa  kwa wasanii ambao wametoa ngoma kati ya Januari 1 hadi Desemba 31, mwaka 2023.

Ambapo kazi hizo zitazingatia vigezo maalumu vinavyostahiki huku wasanii wakitakiwa kuwasilisha kazi zao kuanzia Machi 26, hadi Aprili 20.
Aidha mashabiki wataruhusiwa kupiga kura kuanzia Aprili 29 hadi Mei 29, ujumlishwaji wa kura hizo utafanyika Juni 7, huku matokeo yakitangazwa  katika tukio rasmi la utoaji tuzo kati ya Juni 14 au 15.

Hata hivyo, makamu mwenyekiti kwenye kamati hiyo, Christine ‘Seven’ Mosha ameweka wazi kuwa tuzo za msimu huu wasanii watakaoshinda hawatatoka mikono mitupu kwa kuna fungu limeandaliwa.

Ugawaji wa Tuzo za TMA unatarushwa Mubashara kupitia vituo vya BET na MTV Base vinavyomilikiwa na  Kampuni ya ‘Paramount Africa’ ambayo imeingia mkataba na waandaaji.