Wanamuziki wa dansi wanavyoishi kwa posho
Muktasari:
- Tofauti na wasanii wa kizazi kipya wanaopata fedha kutokana na mikataba na majukwaa ya kidijitali, wanamuziki wa dansi hulipwa kutokana na kila onyesho.
Dar es Salaam. Wanamuziki wa muziki wa dansi Tanzania wameendelea kuendesha maisha yao kwa kutegemea mfumo wa malipo ya posho kila wanapopanda jukwaani kupiga shoo.
Tofauti na wasanii wa kizazi kipya wanaopata fedha kutokana na mikataba na majukwaa ya kidijitali, wanamuziki wa dansi hulipwa kutokana na kila onyesho.
Katika mfumo huu, bendi nyingi hulipa wanamuziki wao kati ya Sh15,000 hadi Sh50,000 kwa shoo moja, kutegemea hadhi ya bendi, uzoefu wa msanii na ukubwa wa tukio.
Bendi kubwa zenye jina huweza kulipa zaidi, huku zile ndogo zikiishia kutoa kiwango cha chini.
“Ukishapanda jukwaani ndiyo kazi yako inaanza kuhesabika, ukikosa shoo, maana yake hakuna kipato siku hiyo,” anasema Samwel msanii wa muziki wa dansi.
Tofauti ya malipo umaarufu wa bendi unaamua
Kiwango cha malipo hutofautiana kwa kiasi kikubwa kati ya bendi na bendi. Kuna bendi zinazolipa Sh30,000 hadi Sh50,000 kwa shoo moja, huku nyingine zikitoa Sh20,000, Sh25,000 au hata chini ya hapo.
Hali hii imekuwa ikizua mjadala miongoni mwa wanamuziki, baadhi wakiamini juhudi wanazoweka hazilingani na malipo wanayopokea.
“Unaweza kupiga shoo nne kwa wiki, lakini ukijumlisha fedha unapata kidogo ukilinganisha na gharama za maisha,” anaeleza mwanamuziki mwingine, Scola.
Wiki ya kazi, shoo nyingi, kipato kisichotabirika
Kwa kawaida, bendi nyingi hupiga shoo kadhaa kwa wiki, hasa siku za mwisho wa wiki na burudani huwa juu. Hii ina maana mwanamuziki anaweza kupata kipato cha wastani kulingana na idadi ya shoo alizoshiriki.
Hata hivyo, changamoto kubwa ni kutokuwepo kwa uhakika wa shoo kila siku, wakati mwingine bendi hukosa mialiko au hupiga shoo chache, jambo linalopunguza kipato kwa wanamuziki.
Changamoto ya mfumo wa posho
Mfumo huu wa kulipwa kwa shoo una faida na hasara zake, kwa upande mmoja, unawapa wanamuziki motisha ya kufanya kazi kwa bidii ili kupata shoo nyingi. Lakini kwa upande mwingine, unawaweka katika hali ya kutokuwa na uhakika wa kipato cha kudumu.
Baadhi ya wanamuziki wamekuwa wakipendekeza kuwepo kwa mikataba ya kudumu au mishahara ya msingi ili kuwapa uhakika wa maisha bora zaidi.
“Tungekuwa na mshahara wa msingi hata mdogo, ungeleta utulivu, posho ibaki kama nyongeza,” anashauri msanii mkongwe wa dansi.
Fedha inavyogawanyika kabla ya wanamuziki
Uchunguzi unaonyesha bendi inapolipwa, kwanza hutoa gharama za msingi za uendeshaji wa shoo, kwa baadhi ya bendi zisizo na vyombo vyao, gharama za ukodishaji huongeza mzigo zaidi.
Baada ya makato hayo, kiasi kinachobaki hugawanywa kwa wanamuziki, ambao wakati mwingine huzidi 10 kwa bendi moja.
“Unaweza kukuta tumepiga shoo ya milioni hadi laki nane, lakini baada ya kutoa matumizi ya gari, sound (muziki) na vyombo, kinachobaki ni kidogo sana. Ukigawa kwa watu wengi, kila mmoja anabaki na kiasi kidogo na hata pesa ya bendi inakuwa ndogo,” anaeleza mwanamuziki na kiongozi wa bendi.
Tasnia inavyoweza kuboreshwa
Wadau wa burudani wanaamini ili kuboresha maisha ya wanamuziki wa dansi, kuna haja ya kubadili mfumo wa malipo na kuendana na mabadiliko ya kisasa ya tasnia ya muziki.
Mapendekezo yanajumuisha
Kuanzishwa kwa mikataba ya kazi
Kuongeza viwango vya malipo kwa shoo
Kuboresha masoko ya muziki wa dansi
Kutumia majukwaa ya kidijitali kuongeza kipato
licha ya changamoto zilizopo, wanamuziki wa dansi wanaendelea kuwa nguzo muhimu ya burudani Tanzania.
Wanapanda jukwaani kila siku, wakiburudisha mashabiki huku wakitegemea posho kama chanzo kikuu cha maisha yao.
Swali linalobaki ni je, muda umefika wa kubadili mfumo huu ili kuwapa wanamuziki hadhi na usalama wa kipato wanaostahili?