Zuchu kuendeleza ubabe TMA na kumtikisa Diamond?

Muktasari:

  • Ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki, msimu uliopita Zuchu aliandika rekodi ya kushinda tuzo nyingi za TMA kwa mpigo na kuivunja rekodi ya Nandy.

Ndilo swali la wengi kwa Zuchu baada ya Baraza la Sanaa Taifa (Basata), kutangaza kuwa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023/24 zitafanyika Juni 15 mwaka huu, huku kwa mara kwanza zikirushwa mubashara na vituo vya BET na MTV Base.

Ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki, msimu uliopita Zuchu aliandika rekodi ya kushinda tuzo nyingi za TMA kwa mpigo na kuivunja rekodi ya Nandy.

Zuchu alishinda vipengele vya Msanii Bora wa Kike wa Mwaka, Video Bora ya Mwaka (Mwambieni), Msanii Bora wa Kike Bongo Fleva, Wimbo Bora wa Bongo Fleva (Kwikwi) na Mwanamuziki Bora wa Kike Chaguo la Watu Kidigitali.

Staa huyo wa WCB Wasafi kuondoka na tuzo tano, alivunja rekodi ya Nandy ambaye katika TMA 2021 alishinda kama Msanii Bora wa Kike wa Mwaka, Msanii Bora wa Kike Bongo Fleva na Mwanamuziki Bora wa Kike Chaguo la Watu Kidigitali.

Utakumbuka TMA 2021, wasanii wote wa WCB Wasafi hawakushiriki kutokana na kile kilichoelezwa ni kutoridhishwa na mchakato wake, ila TMA 2022 walishiriki na kwa ujumla waliondoka na tuzo saba, ndio lebo iliyofanya vizuri zaidi!.

Tuzo hizi zilianzishwa mwaka 1999 na Basata na baadaye mwaka 2003 zilikuja kupata mdhamini na kujulikana kama Kilimanjaro Tanzania Music Awards (KTMA) hadi mwaka 2015 ziliposimama na kurejea mwaka 2022 baada ya serikali kutia mkono.

Endapo Zuchu atawasilisha kazi zake kuwania TMA 2023/24, atakuwa anaanza safari ya kuzifikia rekodi za bosi wake, Diamond Platnumz.

Hadi sasa Diamond anashikilia rekodi ya kushinda tuzo nyingi za TMA kwa usiku mmoja ambapo msimu wa 2014 aliondoka nazo saba, rekodi hiyo inakaribiwa na Alikiba aliyeshinda tuzo tano 2015 ikiwa ni sawa na 20 Percent 2011 na Zuchu 2022.

Zuchu aliyetoka kimuziki takribani miaka minne iliyopita baada ya kusainiwa WCB Wasafi yake Diamond, ana changamoto ya kushinda tuzo nyingi TMA ili aweze kufikisha jumla ya tuzo 18 alizoshinda Diamond.

Katika kipindi cha miaka 12 iliyopita, hakuna mwanamuziki Bongo aliyeshinda tuzo nyingi za TMA kama Diamond, kwa ujumla akikaribiwa na Alikiba ambaye ameshinda tuzo 17 za TMA katika miaka yake 20 aliyokuwepo katika muziki.

Utakumbuka tuzo ya kwanza ya TMA kushinda Diamond ilikuwa msimu wa 2010 kama Msanii Bora Chipukizi kisha wakafuata wengine katika kipengele hicho ambao ni Linah (2011), Ommy Dimpoz (2012), Ally Nipishe (2013) na Young Killer (2014).

Wengine ni Barakah The Prince (2015), Rapcha & Phina (2021) na Kontawa & Gachi (2022). Kuanzia 2021 kipengele cha Msanii Bora Chipukizi kilianza kutoa washindi wawili.

Diamond aliyetoka kimuziki 2009 na wimbo ‘Kamwambie’ chini ya Sharobaro Records, ameshinda tuzo zaidi ya 40 za ndani na nje, kimataifa ameshinda Channel O, MTV, Soundcity, Headies, Afrima, Afrimma, Kora, AEA, EAUSA, the HiPipo Music Awards, Trace n.k.

Hivyo Zuchu ambaye ameshirikiana na Diamond katika nyimbo tatu, ana kazi kufanya ili  na kuzivunja rekodi hizo.