Idadi ya wageni, mapato Ruaha yapaa baada ya Uviko-19

What you need to know:

  • Hakuna ubishi kwamba athari za ugonjwa wa Uviko-19 zilikuwa kubwa na zilitikisa sekta nyingi nchini na duniani. Eneo la utalii ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi baada ya nchi nyingi duniani kufunga mipaka na kuweka karantini.

Hakuna ubishi kwamba athari za ugonjwa wa Uviko-19 zilikuwa kubwa na zilitikisa sekta nyingi nchini na duniani. Eneo la utalii ni miongoni mwa maeneo yaliyoathirika zaidi baada ya nchi nyingi duniani kufunga mipaka na kuweka karantini.

Katika kipindi hicho, wageni katika hifadhi za Taifa na vivutio vingine nchini walipungua badala ya 10 walikuja watano na vivyo hivyo mapato yatokanayo na shughuli hizo nayo yalipungua kwa kiwango hicho.

Hata hivyo, mara tu baada ya janga hilo la dunia, kutokana na mikakati iliyowekwa mambo yanaonekana kubadilika haraka na idadi ya wageni imeanza kuongezeka sambamba na mapato yatokanayo na wageni hao.

Mfano dhahiri wa hali hiyo ni katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha yenye ukubwa wa kilomita za mraba 20,226, ambayo ni makutano ya wanyamapori kutoka kusini na mashariki kwa Afrika.

Ukiacha kipindi cha Uviko-19, mwaka 2020/21 wageni walioitembelea walikuwa nusu ya wale wa mwaka uliotangulia, wanaofika sasa kwa shughuli mbalimbali za kiutalii wameendelea kuongezeka na kuingiza mabilioni ya shilingi.

Kabla, baada ya uviko

Katika mwaka 2018/2019 wageni 21,367 walitembelea Ruaha na kuingiza mapato ya Sh4.75 bilioni huku mwaka uliofuata, 2019/2020, wageni 18,678 waliitembelea hifadhi hiyo na kuingiza Sh4.29 bilioni.

Katika mwaka 2020/21 (kipindi cha Uviko-19) wageni walipungua katika hifadhi hiyo hadi 9,657 na kuingiza Sh1.89 bilioni pekee.

Kutokana na hatua mbalimbali, ikiwemo ya kutojifungia na harakati nyingine za kuutangaza utalii, baada ya Uviko-19 wageni walianza tena kuongezeka mwaka 2021/22 hadi 13,657 na kuingiza mapato ya Sh3.3 bilioni.

Hata mwaka huu wa fedha, yapo matumaini na dalili za kupata wageni wengi zaidi, kwa mujibu wa mkuu wa hifadhi hiyo, kamishna msaidizi wa uhifadhi, Godwell Ole Meing’ataki.

Meing’ataki anasema zipo dalili nzuri za wageni na mapato kuongezeka kwa kuwa ndani ya miezi sita ya kwanza, wageni 7,105 wameshatembelea hifadhi hiyo na kuingiza Sh2.34 bilioni.

Kwa mujibu wa Meing’ataki, ili kuendeleza mafanikio hayo, kinachohitajika ni kuweka mazingira vizuri ili wageni wazidi kuvutiwa, wanyama watunzwe na kuongezeka na hali ya mazingira hifadhini yazidi kuvutia kwa uasili wake.

Uboreshaji huduma

Ili kuongeza ufanisi na kuwavutia zaidi wageni, Hifadhi ya Taifa ya Ruaha imeweka mikakati na kampeni ya kuongeza ubora wa huduma, kuzuia na kupambana na uharibifu wa mazingira pamoja na kupambana na majangili wanaoua wanyama kwa ajili ya meno, pembe, ngozi na nyama.

Ujangili mwingine inaokabiliana nao ni wa kusababisha moto unaoteketeza maeneo mbalimbali ya hifadhi wakati wa shughuli za urinaji asali.

Ili kufanikisha hayo, Meing’ataki anasema hifadhi hiyo inaishirikisha jamii katika vijiji jirani kwa kuwa askari na watumishi wa hifadhi hiyo pekee hawawezi kufika kila mahali na kuilinda hifadhi wakati wote.

Chini ya utaratibu huo, jamii inashirikishwa na hifadhi kwa kuanzisha miradi ya kuisaidia kama ya maji, visima, majengo ya shule kama njia ya kurejesha faida ambayo hiadhi inapata kwa wananchi wanaosaidia kuilinda hifadhi.

Kwa mfano, hivi karibuni hifadhi hiyo imejenga mradi wa kisima na birika la kunywesha mifugo wenye thamani ya Sh68 milioni katika Kijiji cha Nyeregete, Kata ya Rujewa mkoani Mbeya.

Ofisa Uhifadhi, Priscus Mrosso anasema mradi huo pamoja na kuwasaidia wananchi na wafugaji, pia umepunguza kasi ya wafugaji kupeleka mifugo kwenye Bonde la Ihefu ambako inaharibu mazingira na uoto wake wa asili.

Sawa na anavyoona Mrosso, mkazi wa Kijiji cha Nyeregete, Walla Simba anasema mg’ombe sasa wanakunywa maji kwa furaha na safari za Ihefu zimekwisha.

Ihefu ni eneo chepechepe katika Bonde la Usangu ambalo likijaa maji, huyamwaga katika Mto Ruaha Mkuu ambao kwa mujibu wa Meing’ataki ndio “uhai wa Hifadhi ya Taifa Ruaha”. Mto huo ndio hukusanya wanyama wa aina mbalimbali katika hifadhi hiyo, hasa wakati wa kiangazi, na hivyo ni kivutio cha wageni na mapato.

Hata hivyo, Mto huo kwa sasa umekauka kutokana na kinachoelezwa ni ongezeko la shughuli za binadamu katika Konde la Usangu na Uhefu, hali inayosababisha hatua mbalimbali kuchukuliwa ili kuunusuru.

Miradi mingine iliyojengwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) kupitia hifadhi hiyo ni kisima cha maji katika Shule ya Sekondari Mbarali wenye thamani ya Sh66 milioni, ambao Ester Mwalukasa, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo anasema umewakomboa kwa kuwaondolea adha ya kusaka maji, hivyo wanatumia muda mwingi kwa masomo.

Pia, hifadhi hiyo imejenga bwalo na vyoo katika Shule ya Sekondari Mawindi kwa jumla ya Sh192 milioni.

Maji kufika Desemba

Pamoja na umuhimu wake na kuingiza fedha nyingi, Hifadhi ya Ruaha haikuwa na maji safi ya uhakika kwa ajili ya matumizi ya wageni na wafanyakazi, lakini kuanzia Desemba 2022 itakamilisha mradi wa maji wenye thamani ya Sh1.6 bilioni.

Mradi huo unaojengwa kuanzia Septemba 2022 katika Kijiji cha Tungamalenga -- kilomita 36 kutoka hifadhini -- una lengo la kufikisha maji ndani ya hifadhi hiyo unaotekelekezwa kwa ushirikiano wa hifadhi na wananchi wa Tungamalenga.

“Maji haya yanaelekea katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, hasa eneo la Msembe lakini pia yatapelekwa kwenye tenki lililopo Tungamalenga mkoani Iringa kwa ajili ya jamii ya watu wa pale,” anasema Meing’ataki.

Kwa mujibu wa Meing’ataki, hifadhi hiyo kwa miaka 58 tangu ianzishwe, imekuwa na changamoto ya maji na yaliyokuwepo hayakuwa na ubora wala usalama.

“Maji yalikuwa hayafai kwa ajili ya kupikia wala kunywa kwa kuwa yana chumvichumvi na ukijaribu kuyaoga hautakati hata ukitumia sabuni. Na pia viwango vya madini mbalimbali kwenye maji haya yako juu na si mazuri kupikia. Hata ukitaka kupikia utakuta sufuria inabadilika kutokana na chumvi nyingi,” alisema Kamishna huyo msaidizi wa uhifadhi, akisisitiza kuwa wageni wa hifadhi sasa watapata maji safi na salama.

Akizungumzia faida za mradi huo kwa wananchi, Mrosso alisema awamu ya kwanza ya mradi huo itawezesha taasisi za umma kama shule na zahanati kupata maji kijijini hapo na awamu ya pili watapata maji mengi kwa ajili ya Kijiji cha Tungamalenga.

Mtendaji Kijiji cha Tungamalenga, Linus Mheluka anasema mahusiano kati yao, Tanapa na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha hayajaanza leo, ni ya muda mrefu na kuwa wamekuwa wakipata msaada wa kujengewa majengo mbalimbali ya taasisi, hasa za elimu na afya.

“Lakini kwa mradi huu wa maji tunasema umefika kwa wakati kwa sababu kijiji chetu kilikuwa na changamoto sana ya maji ya bomba,” alisema Mheluka.


Changamoto ya ujangili

Kasi ya maendeleo ya Hifadhi ya Taifa Ruaha inapunguzwa na ujangili ambalo kwa kiwango kikubwa unasababisha uharibifu na kuathiri uoto wa asili wa hifadhi na wakati mwingine kusababisha wanyama kutoka hifadhini kwenda kwenye maeneo ya makazi kusaka maji.

Licha ya hatua zinazofanywa na Tanapa na Serikali za kukabiliana na wavamizi wa mabonde ya Usangu na Ihefu, hifadhi hiyo imekuwa inachimba mchanga katika baadhi ya maeneo ya Mto Ruaha ambao umekauka, ili wanyama waweze kupata maji yaliyosalia chini.

Kukauka kwa mto huo, Meing’ataki anasema kumesababisha wanyama kama mamba, viboko, samaji na wengineo kurundika kana katika vibwawa vichache vilivyosalia kwenye maji yasiyokuwa salama.

Anasema madimbwi hayo yamekuwa yakipelekea baadhi ya wanyama kufa au kuambulizana maradhi kama kimeta na mengineyo.

Licha ya kuwekwa faini kubwa ya kukabiliana na ujangili na uingizaji mifugo kwenye bonde hilo, hali hiyo bado inajitokeza na kusababisha athari kubwa.

Mfano wa karibuni ni moto uliozuka na kudhibitiwa katika eneo la Ikupa, ambao uongozi wa hifadhi hiyo na hata wanajiji jirani wanaamini ulisababishwa na majangili wanaorina asali.

Kukabiliana na hali hiyo kwa vyovyote kutawezesha ubora wa huduma, kurejea kwa uotoa wa asili na vivutio kwa wageni na hivyo kuongeza idadi yao na mapato kwa Serikali.