‘Kituo cha biashara Ubungo hakitaua Soko la Kariakoo’

Muktasari:

  • Serikali imesema Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kinachojengwa eneo la Ubungo jijini hapa hakitadhoofisha uwepo Soko Kuu la Kimataifa la Kariakoo, badala yake kitakuwa msaada.

Dar es Salaam. Serikali imesema Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kinachojengwa eneo la Ubungo jijini hapa hakitadhoofisha uwepo Soko Kuu la Kimataifa la Kariakoo, badala yake kitakuwa msaada.

Kituo hicho kitaanza kutoa huduma za bidhaa kutoka China moja kwa moja badala ya wafanyabiashara nchini, Afrika Mashariki na kusini mwa jangwa la Sahara kusafiri au kuagiza mizigo.

Uwekezaji wa kituo hicho unatajwa kuwa Dola 110 milioni za Marekani (Sh275.55 bilioni), huku kikijengwa na Kampuni ya Linghang Group ya China na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.

Akizungumza baada ya kutembelea ujenzi wa kituo hicho juzi, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alisema wafanyabiashara wa Kariakoo hawana sababu ya kuwa na hofu na mradi huo.

“Nataka kuwatoa wasiwasi wafanyabiashara wengine kwamba, eti ujio wa kituo hiki utakwenda kuua Kariakoo, hapana. Lengo sio hilo, Kariakoo itakuwepo biashara zitaendelea, kituo hiki ni kikubwa zaidi kuliko suala la Kariakoo na tayari kituo kinashirikiana na jumuiya ya wafanyabiashara,” alisema Profesa Mkumbo.

Kituo hicho kinachojengwa katika eneo la mita za mraba 7,500, mahali palipokuwa kituo cha mabasi yaendayo mikoani kabla ya kuhamishiwa Mbezi ya Kimara, kinatarajiwa kuwa na mauzo ya Dola 500 milioni za Marekani, (kwa sasa ni Sh1.2 bilioni) kwa mwaka.

“Kituo hiki kitakuwa na bidhaa ambazo zingeenda kununuliwa nje,” alisema Profesa Mkumbo, huku Mkurugenzi Mkuu wa EACLC, Cathy Wang akiahidi mageuzi makubwa ya kibiashara baada ya kuanza kazi kituo hicho.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), Taifa Khamisi Livembe alisema tayari majadiliano ya kuangalia manufaa ya kituo hicho yalishafanyika.

“Tulifanya kikao na wakatoa kipaumbele kwa masharti nafuu tofauti na wengine nje ya Kariakoo, hadi sasa tayari kuna waliokabidhiwa mabanda, tulisisitiza kipaumbele cha wazawa,” alisema Livembe.

“Hata kama wakihamia wafanyabiashara wote wa Kariakoo pale, hakutakuwa na tofauti, watu watakuwa walewale, kwa hiyo hii ni hatua ya mipango lakini tusubiri tuone kwenye utekelezaji itakuwaje, maana mipango ni tofauti na kutenda.”

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo kwa upande wa Kariakoo, Martin Mbwana alisema kituo hicho kitakuwa na msaada wa kuokoa muda na usumbufu wakati wa uagizaji bidhaa kutoka China.

“Hiki kituo kitahamisha baadhi ya maduka yaliyopo China na kuyaweka hapo, kwa hiyo tutaokoa Dola 4 bilioni za Marekani tunazotumia kuagiza mizigo China, unaweka oda kiwandani kwa siku kama 30 halafu unasubiri meli isafirishe kuleta mzigo kwa siku kati ya 24 hadi 35,” alisema Mbwana.

“Lakini hatutaki Wachina waje kufungua maduka huku ila walete hivyo viwanda vyao.”

Kwa mujibu wa EACLC, kituo hicho kitauza na kupangisha maduka hayo, yakiwamo ya huduma za kifedha, ofisi za maduka ya mtandaoni pamoja na wafanyabiashara mbalimbali, wakiwamo wa Kariakoo.

Kwa mujibu wa AECLC, ili uweze kumiliki duka lenye ukubwa wa mita za mraba 11.89, utalazimika kulipia asilimia 10 ya thamani halisi ya Sh162 milioni. Endapo utahitaji kuwa mpangaji wa duka la aina hiyo utalipia Sh16.2milioni kwa mwaka, sawa na makadirio ya Sh1.3 milioni kwa mwezi.