Benki ya TIB kuwakopesha wakulima wa alizeti Handeni

Benki ya TIB kuwakopesha wakulima wa alizeti Handeni

Muktasari:

  • Zaidi ya wakulima 3,600 wa alizeti wilayani hapa wanatarajia kukopeshwa kati ya Sh50 milioni mpaka Sh1 bilioni na Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB) ili kuongeza tija ya shughuli zao.

Handeni. Zaidi ya wakulima 3,600 wa alizeti wilayani hapa wanatarajia kukopeshwa kati ya Sh50 milioni mpaka Sh1 bilioni na Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB) ili kuongeza tija ya shughuli zao.

Mpango huo ni sehemu ya mkakati wa kuhamasisha kilimo cha zao hilo ili kukabili upungufu wa uzalishaji mafuta ya kula nchini. Wakulima hao watakopeshwa kupitia vikundi 182 vilivyopo wilayani Handeni.

Kaimu mkurugenzi fedha za uwakala wa TIB, Monica Luziro amesema “tunatoa mikopo ya kuanzia Sh50 milioni mpaka Sh 1 bilioni kwa masharti tofauti kwa benki za kijamii, kampuni na vikundi vya Amcos na Saccos.”

Monica aliwataka viongozi wa vikundi hivyo kuhakikisha wanaacha urasimu na kuchukua watu ambao kweli wanahitaji kulima alizeti badala ya wanaohitaji fedha kwa ajili ya kwenda kufanyia kazi nyingine tofauti na kilimo.

Wakiwa kwenye kikao cha wadau wa kilimo cha alizeti kilichoitishwa na mbunge wa Handeni Vijijini, John Sallu wakulima hao walisema wapo tayari kuimarisha kilimo lakini changamoto iliyopo ni kukosekana kwa maofisa ugani wanaotakiwa kuwaongoza kukifanya kiwe cha kisasa na chenye tija zaidi.

Mmoja wa wakulima waliohudhuria mkutano huo, Farouk Mhina wa Kwasunga alisema ili kuepuka kukopeshwa fedha ambazo baadaye zinaweza kuwaletea matatizo watakaposhindwa kurejesha kwa sababu tofauti, maofisa kilimo wanatakiwa kuwatembelea shambani na kutoa ushauri badala ya kujifungia ofisini.

“Maofisa kilimo wanatakiwa kutembelea mashamba yetu na kushauri ili tuweze kupata mavuno bora na kurejesha fedha za watu ila wakikaa ofisini wataweza kusababisha sisi kufungwa hilo tunaomba lizingatiwe,” alisema Mhina.

Ofisa maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya Handeni, Recho Mbelwa alisema mpaka sasa wameshasajili vikundi 745 wakati lengo lao lilikuwa kupata vikundi 1,000. recho aliwataka wakulima hao kuacha ubinafsi katika kusaidiana ili wafike mbali zaidi.

Akieleza sababu ya kuwatafutia mkopo wakulima wa alizeti, mbunge Sallu alisema ameona kuna fursa ya kuzalisha mafuta ya kula nchini ambayo yana soko la kutosha litakaloinua uchumi wa wananchi watakaochangamkia.