Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hizi hapa nauli mpya za mabasi, daladala

Muktasari:

  • Latra imesema mabadiliko ya nauli yanalenga kuendana na hali halisi ya gharama za uendeshaji wa huduma za usafiri.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imetangaza viwango vipya vya nauli kwa mabasi ya masafa marefu, mabasi ya mijini (daladala), teksi mtandao pamoja na pikipiki mtandao.

Tangazo hilo limetolewa jana Ijumaa Aprili 17, 2026 kupitia Gazeti la Serikali ambapo zitaanza kutumika siku 14 tangu kutangazwa rasmi kwa mujibu wa gazeti hilo.

Aidha, imeeleza kuwa marekebisho hayo yamefanywa kwa mujibu wa kifungu cha 19 cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini, Sura ya 413, kinachoiruhusu LATRA kupanga na kurekebisha viwango vya nauli na tozo za huduma za usafiri.

Kwa mujibu wa jedwali lililotolewa, nauli za mabasi ya masafa marefu zimepangwa kulingana na daraja la basi na hali ya barabara. Kwa mabasi ya kawaida (ordinary), abiria atalipa Sh57.93 kwa kilometa moja katika barabara ya lami na Sh66.62 kwa barabara ya vumbi.

Kwa upande wa mabasi ya kati (semi-luxury), nauli kwa kilometa moja kwenye barabara ya lami ni Sh74.18.

Pia, mabasi ya mijini (daladala), viwango vipya vinaonyesha kuwa safari ya hadi kilomita 10 itagharimu Sh700, huku nauli ikiongezeka kulingana na umbali hadi kufikia Sh1,500 kwa safari ya kilomita 36 hadi 40.

Awali, nauli ilikuwa inaanzia Sh600 kwa umbali usiozidi kilometa 10 ambapo sasa imeongezeka kuwa Sh700.Pia umbali wa kilometa 34 hadi 40 ilikuwa Sh1,400 ambapo sasa itakuwa Sh1,500.

 Hata hivyo, wanafunzi wataendelea kulipa Sh200 kwa safari bila kujali umbali.

Teksi mtandao, nauli zimepangwa kwa viwango vya chini na juu. Kwa safari isiyozidi kilomita moja, abiria atalipa kati ya Sh4,000 hadi Sh5,000, huku gharama ya kuanzia safari ikiwa kati ya Sh1,100 na Sh1,200.

Vilevile, nauli kwa kila kilomita ni kati ya Sh1,100 hadi Sh1,300 na kwa dakika ni kati ya Sh120 hadi Sh150.

Tozo nyingine ni pamoja na ada ya kusubiri ambayo inaweza kufikia asilimia 3, kamisheni ya asilimia 10 hadi 20, pamoja na tozo ya LATRA ya asilimia 0.5 hadi 1.

Latra imesema mabadiliko hayo yanalenga kuendana na hali halisi ya gharama za uendeshaji wa huduma za usafiri huku yakihakikisha uwiano kati ya maslahi ya watoa huduma na uwezo wa wananchi kumudu nauli.

Kufuatia tangazo hilo wadau wa usafirishaji wakiwamo wamiliki wa mabasi na daladala wamesema wamepokea kwa mikono miwili hatua ya nyongeza kidogo ya nauli ingawa si kubwa lakini wanashukuru Mungu.

"Tunashukuru kwa hiki kidogo maana usiposhukuru kwa kidogo huwezi kupata kikubwa maana gharama za uendeshaji zimependa hivi sasa," amesema Sabri Mabrouk ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala( Darcoboa).

Kauli hiyo ya Mabrouk iliungwa mkono na Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania ( Taboa), Priscus John aliyesema wanaishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio chao.

"Nauli imepanda si kwa sababu tunatafuta faida bali kupunguza gharama za uendeshaji, walichokifanya Latra ni kukidhi gharama zetu za mafuta katika shughuli zetu za kila siku. Hata hivyo, tunashukuru kwa hicho hicho kidogo, sio mbaya maana tunapambana sana haikuwa kazi rahisi kama watu wanavyodhani," amesema John.

Hata hivyo John Essau mtumiaji wa daladala amesema ongezeko hilo lilipaswa kusubiri kwa muda ili kupata mwelekeo halisi wa bei ya mafuta kwani hata bei ikishuka badaye haoni nauli ikishushwa na imekuwa hivyo mara zote.

“Kilichosababisha kupanda kwa bei ya mafuta kinaweza kuisha muda wowote kwani ni mgogoro unaohusisha masilahi ya watu wengi duniani, Latra ingejipa muda kidogo ili kuona mwelekeo halisi maana walivyopandisha hivi hata mafuta yakishuka hawatoshusha tena,” amesema Essau.

Nyongeza na Bakari Kiango