Huduma za fedha zapaa, sarafu mtandao mtihani

Dar es Salaam. Wakati matumizi ya huduma jumuishi za kifedha nchini yakiongezeka kutoka asilimia 65 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 76 mwaka huu, Watanzania wametakiwa kukaa chonjo na matumizi ya sarafu mtandao.

Ripoti ya utafiti wa fedha jumuishi wa Finscope Tanzania uliofanywa na Mfuko wa Kuendeleza sekta ya Fedha Tanzania (FSDT) kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inabainisha idadi ya watu wazima waliotengwa na huduma za kifedha nchini imeshuka kutoka milioni 7.8 mwaka 2017 hadi kufikia milioni 6.4 mwaka huu.

Pia, kati ya asilimia 75 ya wananchi wanaomiliki simu za mkononi, asilimia 72 wanatumia huduma za kifedha kupitia simu zao, kiwango ambacho kimeongezeka ukilinganisha na asilimia 60 iliyokuwepo mwaka 2017.

Hata hivyo, ripoti hiyo inaonyesha kuporomoka kwa matumizi ya huduma za bima kutoka asilimia 15 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 10 mwaka huu.

Pia, ripoti hiyo inaonyesha wanaotumia huduma za vyama vya akiba na mikopo (Saccos) nazo zimeshuka kutoka asilimia mbili mwaka 2017 hadi asilimia moja mwaka huu.

Mafanikio ya kuongezeka kwa watumiaji wa huduma rasmi za kifedha yameelezwa kuchochewa na jitihada za Serikali za kutengeneza mazingira wezeshi.Na kwa maeneo ambayo bado yako nyuma, sekta binafsi inahamasishwa kuona fursa hiyo na kwenda kuwekeza.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa ripoti hiyo jana jijini Dar es Salaam, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba alisema mwaka huu kuna maboresho makubwa yaliyotokana na kukua kwa teknolojia na hamasa inayotolewa na Serikali.

Alisema watu wengi sasa wanatumia mifumo ya kisasa katika kuhifadhi fedha, badala ya kukaa nazo nyumbani. Alisema hata kwenye benki, akaunti za watu zimeendelea kuongezeka mijini na vijijini.

“Tafsiri ya matokeo ya utafiti huu yanatoa fursa kwa sekta binafsi kuendelea kuwekeza zaidi. Kutokana na takwimu, kila mmoja anaweza kuangalia maeneo yenye fursa, Serikali imeweka mazingira wezeshi, tunafahamu imeweka mtandao wa intaneti unafika karibu maeneo yote.

“Katika ripoti hii, tumeona Zanzibar inafikiwa na huduma hizi kwa asilimia 100, kwa Tanzania Bara ni zaidi ya asilimia 80, ambayo bado siyo mbaya,” alisema Tutuba ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Fedha Jumuishi.

Gavana aliongeza kuwa ushiriki wa vijana kwenye fedha jumuishi pia ni mzuri na wengine asilimia 1.7 wameonekana wanatumia huduma za crypocurrency (sarafu mtandao) ambazo alisema bado hazijawa na mifumo mizuri ya udhibiti hapa nchini na kwingineko duniani.

Alitumia nafasi hiyo kuwatahadharisha vijana kuhusu sarafu hizo, kwamba baadhi yao wamekuwa wakipata hasara kwa kutumia huduma hizo, kwani zipo halali na feki na mifumo ya hapa nchini haijaweza kubainisha zipi ni feki na zipi ni halali.

“Tunaendelea kutoa tahadhari kwa umma, watu wajiepushe na kutumia ‘crypocurrency’ ambazo kwa sasa hatujawa na mifumo rasmi ya kufuatilia kama ni genuine (halali).

“Sisi kama Benki Kuu, tunaendelea kufanya utafiti na kuweka mifumo itakayoweza kusimamia vizuri, hadi itakapokamilika. Tutawajulisha na miongozo itatolewa, lakini mpaka sasa bado ni mifumo ambayo haijakaa vizuri,” alisema Tutuba.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Natu Mwamba alisema matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kwamba kuna mwamko katika matumizi ya huduma za fedha na watoa huduma wameweza kutoa huduma tofauti kwa wananchi.

“Sekta ya fedha inakwenda vizuri na watu walio mijini na vijijini wanaendelea kushirikishwa, uelewa wao kwenye masuala ya fedha umeongezeka ndiyo maana matumizi ya huduma hizi zimeongezeka,” alisema Dk Natu.

Alisema wanakwenda kuitumia ripoti hiyo kwa kuangalia maeneo ambayo kuna mianya ili waweke msukumo na kuhakikisha kwamba wananchi wanafikiwa na huduma za kifedha katika maeneo yao.

“Taasisi za kifedha ziongeze juhudi katika kutoa bidhaa zinazowalenga wale wanaowahitaji, maana yake ni kwenda kufanya tafiti kidogo kujua mahitaji yao. Wananchi nao wasisite kwenda kutafuta hizo huduma,’’ alisema.

Kwa upande wake, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa alisema utafiti huo ulilenga kuangalia namna wananchi wanavyotunza fedha zao na kwamba takwimu hizo ni rasmi kutumika katika kuangalia sera za fedha.

Alisema baadhi ya maeneo nchini kama Kilimanjaro, hawahifadhi fedha zao kwa njia rasmi, hivyo utafiti huo utawawezesha wadau wengine kuutumia.