Hujuma yafichuka mitungi gesi ya majumbani

Hujuma yafichuka mitungi gesi ya majumbani

Muktasari:

  • Hujuma nzito kwa wateja, hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya kubainika baadhi ya wafanyabiashara wa gesi ya majumbani hupunguza kati ya kilo tatu hadi tano katika kila mtungi wanaouza.

Moshi. Hujuma nzito kwa wateja, hivi ndivyo unavyoweza kusema baada ya kubainika baadhi ya wafanyabiashara wa gesi ya majumbani hupunguza kati ya kilo tatu hadi tano katika kila mtungi wanaouza.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini hujuma hiyo hufanyika zaidi mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Singida, Dodoma, Manyara, Arusha na Tanga huku Kilimanjaro ukitajwa kuwa kinara.

Kuthibitisha ukubwa wa tatizo hilo, taarifa zinaeleza kwa muda wa wiki mbili sasa, mitungi 400 ya kampuni moja ya gesi ilikamatwa mkoani Kilimanjaro ikiwa na ujazo pungufu.

Miji ya Moshi, Bomang’ombe na Himo mkoani Kilimanjaro inatajwa kuwa kinara na mamlaka zinazohusika zimeanza kulimulika suala hilo.

Mbinu wanazotumika ni wafanyakazi wa magari yanayosafirisha gesi kwenda kwenye depoti za makampuni, ambapo huipunguza njiani na kuijaza kwenye mitungi kwa siri katika baadhi ya nyumba.

Hii inadaiwa kuzisababishia hasara kampuni husika ambazo hulazimika kufidia gesi iliyopungua pale wateja wanaposhtukia huku Serikali nayo ikipoteza mapato yanayotokana na kodi.

Mbinu nyingine ni wajazaji haramu kununua mtungi mkubwa wa kilo 38 na kuijaza kwenye mitungi ya kilo 15 ambapo hupata faida ya zaidi ya Sh30,000.

Uchunguzi umebaini ujazaji huo haramu unasababisha mitungi isiwe na gesi ya kutosha kusukuma gesi yote itumike na mwisho wa siku gesi huisha wakati kukiwa na kati ya kilo mbili hadi tatu hivyo ujazaji upya huwa pungufu pia.

“Huu ujazaji ni hatarishi kwa sababu unafanyika kienyeji mitaani ambako kukitokea mlipuko madhara yake ni majanga. Kwanza wateja wanapunjwa na kuibiwa lakini ni hatari sana,” kilidokeza chanzo chetu.


Taifa Gesi, mawakala wanena

Meneja mauzo wa kampuni ya Taifa Gesi mikoa ya Kaskazini, Victor Kihwilo alikiri kuwapo kwa hujuma kwenye mitungi na Kilimanjaro ni zaidi.

“Ni kweli wiki hii tumekuwa kwenye hizo operesheni mkoani Kilimanjaro ambao ndio unaongoza kati ya mikoa yote Tanzania,” alisema.

Kutokana na hujuma hiyo, alisema kama walitarajia kuuza tani 200 mjini Moshi kwa mfano, matokeo yake huuza tani 100 mpaka 120.

Mmoja wa mawakala wa gesi, Thadey Massawe alisema kudhibiti hujuma hizo wananchi wasikubali kuchukua mtungi kabla hawajapimiwa uzito.


Ewura wafungua kucha

Meneja mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Titus Kaguo alisema uuzaji wa gesi ya kiholela ni hatari hivyo wanaimarisha ukaguzi wa kushtukiza.

“Tunafanya hivi ili kuhakikisha sheria inazingatiwa. Tunawakumbusha wananchi kufanya biashara yeyote ya petroli ikiwamo gesi bila leseni ni kosa na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika ikiwemo faini au kifungo,” alisema.