Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Jinsi ya kukieleza kizazi cha simu janja kuhusu kazi

Picha na Mtandao

Dar es Salaam.  Katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita, dunia ya kazi imepitia mabadiliko makubwa ambayo hayajawahi kushuhudiwa hapo awali.

Wakati zamani kazi ilitafsiriwa kama uwepo wa mfanyakazi ofisini kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni, leo dhana hiyo imebadilika kwa kasi kubwa.

Kwa kizazi cha simu janja, maarufu kama Smartphone Generation, kazi si tena mahali pa kwenda bali ni shughuli inayoweza kufanyika popote na wakati wowote. Simu janja zimekuwa zaidi ya vifaa vya mawasiliano kwani zimegeuka kuwa ofisi zinazobebeka mifukoni mwa watu.  Kupitia simu hizi, mtu anaweza kuendesha biashara, kuhudhuria mikutano, kufanya malipo, kusimamia timu za kazi, kutafuta wateja na mafunzo ya kitaaluma bila kufika katika eneo maalumu la kazi.  Hali hii imeleta kile kinachoitwa “new normal” hali mpya ya kawaida katika ulimwengu wa ajira na uzalishaji.

Kwa vijana wengi, mafanikio hayapimwi tena kwa ukubwa wa ofisi au idadi ya wafanyakazi walio chini yao badala yake, yanapimwa kwa uwezo wa kutumia teknolojia kuzalisha thamani, ubunifu na mapato. 

Ndiyo sababu tunaona ongezeko kubwa la wa wanaojiajiri mtandaoni kama waandishi wa maudhui, wabunifu wa mitandao, wauzaji wa bidhaa kupitia majukwaa ya kidijitali, na wataalamu wanaotoa huduma kwa wateja walioko katika mabara tofauti. Tanzania nayo haijaachwa nyuma katika mabadiliko haya kwani kuongezeka kwa matumizi ya intaneti, huduma za kifedha za kidijitali na mitandao ya kijamii kumeunda mazingira mapya ya kiuchumi.

Vijana wengi wanatumia simu zao kama zana kuu za biashara kutoka kwa wauzaji wa mitindo kupitia Instagram hadi wakulima wanaopata taarifa za masoko kupitia programu za simu, teknolojia imepanua maana ya kazi na kuongeza fursa za kipato. Hata hivyo, pamoja na manufaa hayo, hali hii mpya inaleta changamoto zake ikiwamo kuweka ugumu wa kuwapo kwa mipaka kati ya maisha binafsi na kazi imeanza kufifia.

 Jambo lingine ni kuwapo kwa hatari ya kuongezeka kwa pengo la kidijitali kati ya wale wenye uwezo wa kupata teknolojia na wale wasiokuwa nao. Kwa upande mwingine wa waajiri nao hujikuta wanalazimika kubadilisha mitazamo yao.

Badala ya kupima tija kwa kuangalia muda ambao mfanyakazi amekaa ofisini, sasa wanapaswa kuzingatia matokeo na ubora wa kazi inayozalishwa.

Hii inahitaji mifumo mipya ya usimamizi, uaminifu mkubwa kati ya mwajiri na mwajiriwa, pamoja na uwekezaji katika teknolojia za mawasiliano na usalama wa taarifa. Katika mazingira haya mapya, ujuzi wa kidijitali umekuwa hitaji la msingi sawa na kusoma na kuandika. Kizazi cha simu janja kinapaswa kujifunza si tu namna ya kutumia teknolojia, bali pia namna ya kuitumia kwa tija, maadili na ubunifu.

 Serikali, taasisi za elimu na sekta binafsi zinapaswa kushirikiana kuwapa maarifa yanayowawezesha kushindana katika soko la ajira la kidijitali.  Kazi ni uwezo wa kutumia maarifa, teknolojia na ubunifu kutatua matatizo na kuleta thamani katika jamii. Hiyo ndiyo hali mpya ya kawaida, na ni ukweli ambao hatuwezi kuupuuza katika safari ya kuelekea uchumi wa kidijitali.