Kilimo cha mboga, matunda kinavyozibeba familia nyingi

Muktasari:

  • Kutokana na mikakati madhubuti iliyowekwa, kilimo cha mbogamboga, matunda na viungo kinazidi kukua nchini hivyo kuwa mkombozi wa kipato kwa kaya zilizoiona fursa.

Kutokana na mikakati madhubuti iliyowekwa, kilimo cha mbogamboga, matunda na viungo kinazidi kukua nchini hivyo kuwa mkombozi wa kipato kwa kaya zilizoiona fursa.

Ukiacha kipato cha uhakika, faida nyingine katika sekta hiyo ni ongezeko la ajira pamoja na fursa za mikopo kutoka taasisi za fedha.

Matrina Chakupewa (36) ni mkulima aliyejikita kwenye kilimo cha pilipili aina ya habanero, karela pamoja na maharage machanga anayefanya shughuli zake katika Kata ya Nduruma wilayani Arumeru, Mkoa wa Arusha.

Awali, anasema alikuwa akishikiri kilimo cha kawaida cha mazao kama vile viazi na mihogo ambayo wakati mwingine hakuwa na uhakika wa soko jambo ambalo kwa sasa hakumbani nalo.

Martina ambaye ni mama wa watoto watano anasema kwa sasa ameungana na wenzake wawili kulima shamba la ekari 20 mazao hayo baada ya kupata ushauri wa kitaalamu kutoka Asasi ya Kilele inayoshirikiana na Chama cha Wakulima wa Matunda na Mbogamboga Tanzania (Taha) kuwawezesha wakulima.

Kutokana na kilimo hicho wanachokifanya kisasa kutokana na miundombinu ya umwagiliaji iliyopo, anasema kimemsaidia kuinua uchumi na kujiongezea kipato tofauti na awali alipokuwa anajishughulisha na biashara ya kuuza vipuri vya magari lakini kwa sasa ameelekeza nguvu kubwa kwenye kilimo.

Kwa sasa, anasema wanavuna mara nne kutokana na maarifa waliyojengewa na Taha iliyowakutanisha na mnunuzi anayesafirisha mazao hayo kwenda nje ya nchi ambaye waliingia mkataba wa kufanya biashara.

“Katika makubaliano yetu, mnunuzi anatuletea mbegu ila baadaye atatukata na tayari tumekubaliana bei ya kununua tofauti na awali nilipokuwa nalima viazi na mihogo, nilikuwa nalima kilimo cha mazoea cha kutegemea mvua za msimu na soko lilikuwa la kubadilika mara kwa mara hata nilichokuwa navuna kilikuwa tofauti. Kuna muda naenda na mihemko naingia shambani vitu vikiwa bei juu lakini wakati wa mavuno unakuta tuko wengi hivyo bei inakuwa chini,” anasema.

Lakini sasa mambo yamebadilika kwani analima huku akiwa na mkataba na anajua anauza kiasi na Bei gani. Kwa wiki anasema mekubaliano yao ni kuvuna mara tatu mpaka nne lakini mnunuzi habadiliki na bei ni ileile waliyokubaliana awali jambo lililomshawishi kuwekeza zaidi kutokana na nuhakika wa soko.

“Kiuchumi kilimo hiki kinatusaidia sana kwani nina duka la vipuri vya magari lakini hadi ukiona nimeacha duka nimekuja huku ujue kinalipa zaidi,” anasema.

Mkulima huyo anasema miongoni mwa manufaa aliyopata ni kukuza kipato cha familia yake ambayo imeweza kununua shamba hilo la ekari 20 kwa nia ya kuachana na mashamba ya kukodisha katika misimu ijayo.

Mbali na masoko, anasema wameunganishwa na taasisi za fedha kwa ajili ya kupata mikopo kwa riba nafuu ya asilimia tisa wanayoitumia kuwekeza zaidi ambapo msimu wa mavuno hutoa ajira za muda hadi 80.

Hata hivyo kuna changamoto hasa upatikanaji wa maji kwa ajili ya umwagiliaji ambayo anasema wanajitahidi kukabiliana nayo.

Katika kuitatua changamoto hiyo, anasema wamechimba bwawa wanalolitumia kumwagilia.

“Awali tulikuwa tunateseka kwa kugombea maji ila baada ya kuchimba bwawa tuna nafuu. Kwa sasa linatusaidia katika kilimo.Tunaomba Serikali ilitizame hili na kuangalia namna mgao wa maji ya kumwagili unavyoweza kutolewa kwa usawa,” anashauri Martina.

Mkulima huyu anataja changamoto nyingine ambayo inapaswa kufanyiwa kazi na Serikali kuwa ni kuangalia namna ya kugawa au kukodisha mashamba makubwa ambayo hayatumiki ili wakulima waweze kuyatumia ikiwamo vijana kwa kuwapa mafunzo ili washiriki kuikuza sekta hiyo.

“Kuhusu masoko, Serikali iangalie namna inaweza kutuletea wanunuzi wengi ili kuwe na ushindani. Kwa mfano, mimi nimelima karela ikitokea kwa mnunuzi huyu bei yake iko chini niwe na uchaguzi mwingine, kukiwa na wanunuzi wengi itasaidia kupata bei tofauti na ushindani utakuwa mkubwa katika sekta hii,” anasema.

Mkulima mwingine, Daniel Maina anayelima mbogamboga katika Kijiji cha Oleijoruno wilayani Arumeru akijikita zaidi kulima maharage machanga na vitunguu anasema huu ni mwaka wa nne tangu aanze kilimo hicho kilichomwinua kiuchumi kikimwezesha kusomesha watoto na kujenga nyumba.

Mkulima huyo anasema ameingia mkataba na mnunuzi kumuuzia maharage kwa Sh1,200 kwa kilo moja tofauti na ilivyo kwenye masoko ya kawaida alikokuwa akiuza kwa kati ya Sh600 hadi Sh800.

“Moja ya faida za kilimo hiki ni kwamba hili ni zao la muda mfupi, yaani ndani ya siku 45 yameshaiva na kwa sasa hivi navuna hadi tani mbili na kuendelea na msimu uliopita niliuza kilo 2,500 ila kwa mwaka huu natarajia kuuza zaidi kwani nimeongeza shamba jingine la ekari moja hivyo mazao yataongezeka,” anasema Maina.

Kuhusu changamoto, anasema mikopo ya wakulima ni moja ya masuala yanayopaswa kuangaliwa ili waweze kukopesheka hivyo kuwarahisishia kubadilika na kulima kilimo chenye tija ili kuongeza kipato chao na kuchangia zaidi pato la Taifa.

Kati ya anayoshauri yafanywe, anasema ni wakulima kukopeshwa pembejeo zitakazowawezesha kulima kwa wakati.

Naye Aziza Madoda mkulima wa pililipi mwenye shamba la ekari 10 lililopo Nduruma anasena alianza kilimo cha mkataba tangu mwaka jana na mambo yake yamebadilika tofauti na awali alipikuwa analima matikiti, nyanya na mazao mengine na kuyapeleka sokoni huku bei zikiwa hazieleweki na kufanya ashindwe kukua kiuchumi.

“Mimi ni mjane nina watoto wanne hivyo kupitia kilimo naweza kuwasomesha watoto na kumudu mahitaji ya msingi ya familia. Nimewekeza nguvu nyingi katika kilimo na msimu huu unaoanza natarajia kulima maeneo mengi zaidi,” anasema Aziza.

Kuhusu changamoto zinazopaswa kutatuliwa haraka anasema ni mbolea ya ruzuku kwani yeye mwenye ekari 10 anapewa mifuko 20 ambayo haitoshelezi hivyo kushauri pawe na utaratibu utakaokidhi mahitaji yao.

“Hii mbolea inatusaidia lakini haitoshelezi mahitaji, natamani hiki kilio kifike huko juu, dawa pia ni ghali zaidi kuliko mbolea hivyo inakuwa changamoto,” anasema.