Wasomi vyuo vikuu nchini watakiwa kujifunza Kichina

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera PICHA|MAKTABA

Muktasari:

Hotuba hiyo ilisomwa katika uzinduzi wa ushirikiano wa ufundishaji wa lugha ya Kichina katika Chuo Kikuu cha Waislamu cha mjini Morogoro.

Morogoro. Wasomi nchini, wamehimizwa kujifunza lugha ya Kichina, ili washiriki katika kukuza uchumi wa nchi kwa kuzingatia kuwa uchumi wa dunia unategemea sana bidhaa na mchango wa China kwa sasa.

Rai hiyo ilitolewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Saidi Amanzi.

Hotuba hiyo ilisomwa katika uzinduzi wa ushirikiano wa ufundishaji wa lugha ya Kichina katika Chuo Kikuu cha Waislamu cha mjini Morogoro.

Bendera aliwaasa wasomi kutumia fursa ya Kichina, kujifunza kwa bidii na kupanua wigo takaayowawezesha kuwasiliana katika kufanya biashara kati ya Watanzania na Wachina. Katika uzinduzi wa ushirikiano huo, Makamu mkuu wa chuo hicho, Profesa Hamza Ngozi, alisema kuwa ni vyema wanafunzi wakajifuza lugha hiyo na kuitumia kama nyenzo ya kutafuta maarifa zaidi katika dunia ya utandawazi.

Alisema chuo kikuu hicho ni tatu nchini kuanza kufundisha lugha ya Kichina, baada ya Chuko Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma.

Wanafunzi wa chuo kikuu hicho walisema ushirikiano huo ni mzuri na upaswa kuigwa na vyuo vikuu vingine.