Kwa nini kampuni changa bunifu ni muhimu kwauchumi wa sasa

Kwa mujibu wa mtandao wa kimataifa wa Startupblink, kampuni changa bunifu (startup) huchangia asilimia 20 ya kazi zote zilizopo sasa, huku zikiongeza uzalishaji na tija katika shughuli mbalimbali.

Ripoti zilizopo zinaonyesha kuwa kwa mwaka 2022 Startup zilichangia Dola 5.4 katika uchumi wa Afrika, lakini makadirio yaliyopo ni kuwa biashara hizo zinaweza kuchangia hadi Dola 2.6 trilioni ifikapo mwaka 2030.

Athari zake kiuchumi ni kuongezeka kwa mapato ya kodi katika mataifa ambayo yatakuwa na ukuaji mzuri wa biashara hizo, lakini pia startup ni kivutio kikubwa cha uwekezaji kutoka nje (FDI) katika ulimwengu wa sasa.

Loading...

Loading...

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, Philip Besiimire anaelezea umuhimu wa kampuni kubwa zilizopo sasa kuwashika mkono vijana wabunifu na kuwasaidia kukuza biashara zao.

“Kuna kampuni nyingi kubwa duniani ambazo mawazo yake yalianzia bwenini vijana wakiwa wamekaa tu, lakini leo hii zina thamani ya mabilioni ya Dola, hivyo naamini kwa kutoa fursa na kuwashika mkono wabunifu tunaweza kutengeneza mabilionea siku zijazo,” alisema wakati wa uzinduzi wa awamu ya tatu ya mradi wa Accelerator unaoendeshwa na kampuni hiyo.

Bosi huyo wa mtandao wa simu wenye wateja wengi zaidi Tanzania anasema kupitia mtandao mpana wa Vodacom wenye wateja karibu milioni 20 wanatoa fursa kwa vijana kuendeleza startup zinazoleta suluhu ya changamoto za kijamii hata kama haizalishi fedha nyingi kama faida.

Hata hivyo, Besiimire anasema mwamko wa wanawake kuwa na biashara bunifu ni mdogo, lakini anatamani kuona wengi wakiibuka kupitia programu hiyo waliyoianzisha.

Kupitia programu ya Accelerator inayolenga kuunga mkono ubunifu wa kidijitali unaochipukia katika maeneo ambayo yana fursa kuzalisha mapato makubwa lakini pia kutatua changamoto ambazo zinaikabili jamii, Besiimire anaalika wanawake wengi zaidi kujitokeza.

Kupitia programu hiyo mwaka huu Vodacom inakusudia kuunga mkono wabunifu katika sekta ya elimu, afya, kilimo biashara, usalama wa mitandao, teknolojia ya huduma za fedha na masoko ya mitandaoni.

Miongoni mwa waanzilishi wa programu hiyo na mkuu wa mikakati na usimamizi wa Vodacom Tanzania, Yvone Maruma anasema walichagua kada hizo kwa kuwa ndizo ambazo ni rahisi kutekeleza ubunifu wake, lakini pia ni kipaumbele katika maisha ya sasa.

Hata hivyo, kwa mujibu wa tovuti ya Africa The Big Deal, kushuka mtaji uliovutwa nchini kwa ajili ya biashara bunifu, kutoka dola za Kimarekani milioni 80 (Sh201.1 bilioni) mwaka 2022 hadi dola milioni 25 (Sh62.8 bilioni) mwaka jana.

Ili kutatua changamoto zilizopo na kuvutia zaidi mitaji katika biashara bunifu nchini, Maruma anasema Taasisi ya Masschallenge ya nchini Boston itafanya kazi kwa karibu kati yake na Vodacom ili kuwalea na kuwasimamia vijana hao katika shughuli zao.

Taasisi hiyo inamiliki kituo atamizi tangu mwaka 2009, hivyo ina uzoefu mkubwa kwa kulea na kukuza vipaji kwa muda mrefu, hivyo watasaidia kwa sehemu kubwa kupunguza changamoto zinazokabili ubunifu nchini.

“Ubunifu unaofanywa na wengi haukidhi viwango vya kupata fedha za wawekezaji wa nje, Masschallange ni wazoefu katika eneo la biashara bunifu, lakini pia wana mtandao mkubwa wa wawekezaji, hivyo ni rahisi kuwakutanisha na kuongeza kiwango cha mitaji ya nje inayokuja nchini,” anasema.

Ili kukuza ubunifu nchini, mbali na programu ya Accelerator, Vodacom ina miradi mingine, ikiwemo ya elimu ya kidijitali (e-fahamu, mafunzo ya dijitali kwa wasichana (Code like a Girl) na imekuwa ikitoa msaada wa hali na mali kwa vijana wabunifu na wenye kampuni chipukizi katika sekta ya dijitali (Startups).

Aidha, suala la kampuni kubwa za teknolojia kusaidia kampuni za kiteknolojia zinazochipukia imekuwa kama njia yao mpya ya kuwajibika kwa jamii, pengine ni kwa kuzingatia fursa kubwa iliyopo katika eneo hilo.

Mbali na Vodacom, Huawei naye ni miongoni mwa kampuni zinazosaidia ukuzaji wa startup, hususan uvumbuzi wa dijitali na wanaofanikiwa kunufaika na kuwepo katika programu zao na zile ambazo wao ni washirika hupelekwa China kwa ajili ya matembezi ya kujifunza.

Huawei imekuwa na utaratibu wa kuwapatia mafunzo kwa vitendo vijana wa kibunifu kupitia miradi yao mbalimbali na ile wanayoishiriki kampuni nyingine, wanufaika hutembezwa katika baadhi ya kampuni kubwa za teknolojia nchini China.

“Ni muhimu sana kuwekeza katika rasilimali watu kwa kuwapa ujuzi stahiki. Miti midogo ndiyo hutengeneza msitu,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa Huawei Tanzania, Damon Zhang wakati akizungumza katika hafla ya kuwapongeza wahitimu walioshiriki mradi wa Seed for the future Tanzania.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe anasema Serikali inawaunga mkono ubunifu kupitia programu za taasisi ikiwemo Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo, (Sido) kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa.

“Kuna fedha maalumu ambayo vijana wanaofuzu na ubunifu wanasaidiwa na tayari kuna vijana wengi wako huko. Hata wale wenye mawazo ya kiviwanda kupitia Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Viwanda, (Tirdo) wanawasaidia kukuza mawazo yao,” anasema Kigahe.

“Kisha tunawaunganisha na mashirika ya kimataifa ambayo yanawasaidia vijana wabunifu, si hivyo tu hivyo bali hata wale wanaozalisha bidhaa tunawasaidia kwenye maonesho ya kimataifa ili wadau wengine wanaonunua na kushirikiana kibishara wanaona,” alisema Kigahe.

Anasema Serikali inatambua changamoto walizonazo startup nchini lakini kwa suala la mitaji inawatengeneza mazingira kuweza kupata fedha za nje lakini pia inatoa mikopo kwa ajili yao kupitia.

“Licha ya changamoto ya mitaji waliyonayo vijana wana mawazo ya kibiashara lakini hawana fedha hivyo Serikali inawawezesha hata waweze kuomba taasisi za fedha za kimataifa ukiacha zile za ndani lakini pia kutenga bajeti kupitia taasisi zetu za kiserikali,” anasema Kigahe.


Ubunifu wenye mvuto zaidi kwa sekta mwaka 2023

Kwa mujibu wa mtando wa Africa the Big Deal, bunifu zinzovutia uwekezaji zaidi na zinazoongoza kwa kukua ni sekta ya fedha kidijitali ambayo ilivutia dola 1.2 bilioni kwa asilimia 42, nishati dola 800 milioni (asilimia 28) na usafiri na uchukuzi dola 210 milioni (asilimia 12.5).

Nyingine zinazoongoza kuvutia zaidi wawekezaji ni huduma za afya Dola 190 milioni (kwa asilimia 6.5), chakula na kilimo kwa Dola 180 milioni (asilimia 6.3) zikifuatiwa na biashara za rejareja, ubunifu wa kihandisi, huduma za simu, vyombo vya habari na burudani.

Hata hivyo, ripoti hiyo inaonyesha kuwa kwa jumla mwaka 2023 haukuvutia uwekezaji mwingi kwa Startup ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita, kwani mwaka 2021 na 2022 uwekezaji ulikuwa zaidi ya Dola 4.4 bilioni.


Namna ya kuvuta uwekezaji zaidi wa Startup nchini

Akizungumzia kushuka fedha zinazowekezwa kwenye ubunifu nchini, Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Mwinuka Lutengano anasema kuanzia mwaka 2019 kulikuwa na juhudi kubwa eneo hili kuanzisha, kuimarisha na kuwezesha vituo vya uatamizi na ubunifu katika Taasisi za elimu na vyuo nchini.

"Mwamko ule tunaona umeanza kupungua hivi karibuni na hiyo maana yake matokeo yatokanayo na uwekezaji wa kampuni changa na ubunifu vinashuka," anasema.

Dk Lutengano anaongeza kuwa ili kuvuta wawekezaji wengi zaidi, ni vyema suala hili pia lipate msukumo mkubwa wa kitaifa, hasa kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na COSTECH.

"Kuwa na mashindano ya kuwaleta wabunifu pamoja. Kikubwa ni kuona wabunifu wanawezeshwa, kuunganishwa na masoko ya bidhaa na mitaji ili wakue na wawe wawekezaji wenye tija kwa taifa," anasema.

Kwa upande wake Jumanne Mtambalike, mwanzilishi wa kampuni ya ushauri ya usimamizi wa miradi, Sahara Ventures anasema kampuni changa na bunifu ni mustakabali wa bara zima la Afrika.

Anasema wakati Serikali za Kiafrika zikihangaika na changamoto ya ukosefu wa ajira, kuwekeza katika kampuni hizi kunaweza kuwa mojawapo ya suluhu kwa tatizo hilo.

"Tafiti zinaonyesha ajira zaidi ya milioni 450 zinahitajika ifikapo mwaka 2035 ili kuhudumia vijana wanaotafuta kazi barani Afrika. Kwa hivyo ni lazima tujenge mifumo ikolojia ya Startup ili kufaidika na uchumi wake kwa kushughulikia masuala ya ukosefu wa ajira," anasema Mtambalike.

Akishauri kuhusu masuala ambayo Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwenye mifumo iliyokomaa ili kufikia uchumi wa Startups, anasema ni pamoja na kuwekeza kwenye vipaji na ustadi wa kidijiti.

Anasema ili Tanzania unufaike na hilo, kuna haja ya kuwa na programu na majukwaa ya ustadi wa kidijitali ya kiwango cha juu zaidi ili kusaidia kutoa vipaji kwa mifumo ya startups ya ndani, kikanda na kimataifa.

Eneo jingine anashauri kuwekeza kwa Watanzania waishio nje (diaspora), huku akisema kuwa Startups ni biashara za kimataifa.

"Pia, Tanzania inahitaji kuangalia upya nafasi ya diaspora katika kusaidia biashara za ndani. Mojawapo ya sababu za kufaulu kwa mfumo wa ikolojia wa Nigeria ni jukumu linalotekelezwa na jumuiya za diaspora," anasema.