Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kwanini ni muhimu kuwekeza katika nishati jadidifu?

Dar es Salaam. Wakati mataifa duniani yakiongeza uwekezaji katika nishati mbadala ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika, wachumi wanasema Tanzania haiwezi kuachwa nyuma katika mbio hizo.

Hiyo ni kutokana na umuhimu wa umeme wa uhakika unaotegemea vyanzo asilia kwa ajili ya mageuzi ya sekta ya viwanda.

Hivyo, uwekezaji wa Serikali wa Sh25 bilioni kwa ajili ya kuendeleza miradi ya jotoardhi si tu zitawezesha kuzalisha umeme, bali ni hatua ya kimkakati inayoweza kuamua namna uchumi wa Tanzania utakavyokuwa katika miongo ijayo.

Mchambuzi wa uchumi, Marcelina Magenzi anasema kadri uchumi wa nchi unavyokua, mahitaji ya nishati ya uhakika yanaongezeka, hivyo kuwekeza katika vyanzo vya nishati visivyoathiriwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya tabianchi ni jambo lisiloepukika.

Anasema jotoardhi ni miongoni mwa vyanzo vichache vya nishati mbadala vinavyoweza kuzalisha umeme saa zote za siku bila kutegemea mvua, upepo au mwanga wa jua.

“Tunapozungumzia viwanda, uchakataji wa mazao na uwekezaji mkubwa, msingi wake ni upatikanaji wa umeme wa uhakika. Jotoardhi inaweza kuwa moja ya nguzo za usalama wa nishati wa Tanzania katika miaka ijayo,” anasema.

Maneno yake yanaungwa mkono na Massawe Malisa, anayesema dunia ya sasa inaingia katika enzi ya uchumi wa kijani ambapo nchi zenye vyanzo vya nishati safi zitakuwa na faida kubwa zaidi katika ushindani wa kiuchumi.

“Uwekezaji katika nishati mbadala unasaidia kuvutia wawekezaji, kupunguza gharama za uzalishaji na kufungua fursa mpya za ajira na ubunifu wa teknolojia,” anasema.

Umeme unaotoka katika jotoardhi ni miongoni mwa nishati jadidifu ambazo Tanzania inalenga kuzalisha umeme kutoka huko huku ikilenga kupata megawati 130 ifikapo mwaka 2030.

Akizungumzia utendaji wake kufikia malengo waliyowekewa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TGDC, Shakiru Kajugus anasema fedha walizotengewa katika mwaka huu wa fedha zitatumika kuendeleza miradi katika maeneo ya Ngozi mkoani Mbeya na Kiejo-Mbaka mkoani Songwe, huku maeneo ya Luhoi mkoani Pwani na Natron yakiendelea kufanyiwa utafiti wa awali.

Kajugus anasema katika mwaka huu wa fedha ulioanza Julai mosi, kampuni hiyo inatarajia kuchoronga visima vitatu na kufanya uhakiki katika mradi wa Ngozi, ambapo kila kisima kitafikia kina cha takribani kilomita 1.5 chini ya ardhi.

“Tumetengewa Sh25 bilioni kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya shughuli za uchorongaji. Hii ni kazi inayoendelea kwa miaka kadhaa na bajeti imekuwa ikitengwa kulingana na hatua za utekelezaji,” anasema.

Kajugus anasema TGDC kwa sasa ipo katika hatua ya uhakiki wa rasilimali ya jotoardhi ambayo ni hatua muhimu kabla ya kuanza uzalishaji wa umeme.

Mbali na miradi inayofanyiwa uchorongaji anasema katika maeneo ya Luhoi na Natron yanafanyiwa tafiti mbalimbali za kisayansi zinazojumuisha jiolojia, jiokemia na jiografia ya kijiolojia. kabla ya kubainisha maeneo yatakayochorongwa.

“Tuko katika hatua ya uziduaji. Baada ya tafiti hizo tunafanya tathmini za mazingira na hatimaye kubaini maeneo sahihi ya kuchoronga visima,” anasema.

Hili linafanyika wakati ambao Tanzania imejiwekea lengo la kuzalisha megawati 130 za umeme wa jotoardhi ifikapo mwaka 2030 lengo ambalo limeainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na mikakati mingine.

Anasema licha ya kutokuwa wameanza uzalishaji wa umeme, utekelezaji wa miradi unaenda sambamba na ratiba iliyopangwa.

“Bado tuko ndani ya muda, miradi tunayoifanyia kazi sasa itatuwezesha kufikia megawati 130 ifikapo mwaka 2030. Mradi wa Ngozi unatarajiwa kuzalisha megawati 70 huku mradi wa Kiejo-Mbaka ukitarajiwa kuzalisha megawati 60, hivyo kufikisha jumla ya megawati 130,” anasema.

Akizungumzia changamoto ya wataalamu wa ndani, Kajugus anasema teknolojia ya uchorongaji wa visima vya jotoardhi bado ni mpya nchini, hivyo kwa sasa wataalamu wengi wanaotumika wanatoka nje ya Tanzania.

Hata hivyo ili kukabiliana na hali hiyo TGDC imeingia mikataba ya ushirikiano na vyuo mbalimbali vya elimu ya juu ili kuongeza wataalamu wazawa katika sekta hiyo.

“Tunaamini ndani ya miaka mitano ijayo tutakuwa na wataalamu wengi wa ndani na sekta ya jotoardhi haitakuwa tena ngeni nchini,” anasema.

Kajugus anasema pamoja na kuzalisha umeme, rasilimali ya jotoardhi ina matumizi mengi ya moja kwa moja katika shughuli za kiuchumi, ikiwamo usindikaji wa mazao, viwanda, kilimo cha nyumba kitalu, ufugaji wa samaki na kuku, usindikaji wa maziwa pamoja na matumizi mengine yanayohitaji joto au baridi.

Anasema matumizi hayo yanafungua fursa kwa wabunifu na wawekezaji kuendeleza teknolojia mbalimbali zinazotumia nishati ya jotoardhi, hivyo kuongeza thamani ya rasilimali hiyo na kuchochea maendeleo ya uchumi.

Mmoja wa watembeleaji wa maonyesho hayo, Masanja Masumbuko ametaka uwezeshaji zaidi kwa Watanzania ili waweze kufahamu faida nyingine zinazotokana na jotoardhi ili waweze kuzitumia katika kukuza uchumi.

“Kwanza jotoardhi tu ni kitu ambacho watu wengi hawakifahamu, wasijifungie, watoke nje waelimishe watu, huenda huku kwenye makazi yetu kuna maeneo ambayo yanaweza kubeba rasilimali hii,” anasema.