Mafanikio ya EnDev yachochea wito wa uwekezaji sekta ya nishati
Muktasari:
- Serikali yasisitiza uwekezaji sekta ya nishati, mafanikio ya EnDev yaelezwa kubadilisha maisha ya mamilioni.
Dar es Salaam. Serikali imeitaka sekta binafsi, taasisi za kifedha na washirika wa maendeleo kuongeza uwekezaji katika sekta ya nishati nchini kufuatia mafanikio ya kubadilisha maisha ya karibu watu milioni mbili kupitia mpango wa Energising Development (EnDev).
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, wakati wa maadhimisho ya miaka 13 ya mpango wa EnDev leo Jumatatu, Juni 15, 2026, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Innocent Luoga, amesema soko la suluhisho za nishati safi sasa ni halisi na linaendelea kukua.
Amesema kwa sekta binafsi, wasambazaji, wazalishaji na wajasiriamali, kuna haja ya kuendelea kuwekeza katika ubora, ubunifu na huduma kwa wateja, akibainisha kuwa mahitaji yapo na Serikali iko tayari kuwaunga mkono.
Kamishna huyo pia amezitaka taasisi za kifedha na vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (Saccos) kutambua fursa za kibiashara zilizopo katika sekta hiyo, hususan katika upatikanaji wa mikopo kwa nishati safi ya kupikia.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2013, mpango wa EnDev unaoshirikisha Serikali, Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV) pamoja na wafadhili wa kimataifa, umeleta mabadiliko makubwa katika sekta ya nishati nchini Tanzania.
Luoga amesema takwimu zinaonesha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025, sawa na ongezeko kubwa ndani ya miaka minne.
Amesema kupitia Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034), Serikali inalenga kufikia asilimia 80 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Mpango huo umeongeza upatikanaji wa suluhisho za taa kwa takribani watu 300,000 pamoja na teknolojia za nishati safi ya kupikia kwa watu karibu milioni mbili.
Amesema mchango mkubwa katika mafanikio hayo umetokana na jiko banifu la “Jiko Matawi”, ambapo zaidi ya majiko 962,000 yameuzwa kupitia mtandao wa wazalishaji 120 katika mikoa 20.
Majiko hayo hupunguza matumizi ya kuni kwa hadi asilimia 40, hatua inayotoa faida za haraka kiuchumi na kimazingira kwa kaya. Mkurugenzi wa muda wa SNV nchini, Mary Rauscher, amesema athari za mpango huo zimevuka takwimu za upatikanaji wa nishati na kugusa maisha ya jamii kwa ujumla.
Amesema familia zinaokoa fedha huku wanawake na wasichana wakipata muda zaidi wa elimu na shughuli za kuongeza kipato.
Amebainisha kuwa hatua inayofuata ya EnDev itajikita katika umiliki na uongozi wa Waafrika, huku Tume ya Umoja wa Afrika ikitarajiwa kuwa mshirika muhimu wa kisiasa.
Amesema maendeleo endelevu yanahitaji mabadiliko ya mifumo, iwe katika sekta ya nishati, kilimo au maji, ili kuimarisha taasisi na kuwezesha masoko jumuishi.
Kwa mujibu wa Kamishna Luoga, kasi ya maendeleo katika sekta hiyo inatokana na uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameifanya ajenda ya nishati safi ya kupikia kuwa kipaumbele cha Taifa.
Ameendelea kusema licha ya mafanikio, bado kuna changamoto ikiwemo uwezo mdogo wa baadhi ya kaya za vijijini kumudu gharama pamoja na haja ya mifumo ya udhibiti kwenda sambamba na ubunifu.
Mpango wa EnDev unatekelezwa kupitia ushirikiano wa wafadhili mbalimbali ukiwemo Serikali za Ujerumani, Uholanzi, Norway, Uswisi, Uingereza, Australia na Sweden.