Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mfumo wa kilimo unaotumia Akili Unde kuongeza tija kwa wakulima

Muktasari:

  • Mfumo huo wa kidijitali unawapatia wakulima taarifa muhimu ikiwamo aina ya udongo, kiwango cha unyevunyevu, tindikali ya udongo, mazao yanayofaa kulimwa, mahali pa kupata pembejeo bora pamoja na masoko ya uhakika ya kuuza mazao yao

Dar es Salaam. Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) kupitia Chuo cha Ufundi Stadi Kipawa, imebuni mfumo wa kilimo unaotumia Akili Unde (AI) utakaowasaidia wakulima kufanya uamuzi sahihi, kuongeza uzalishaji na kuinua faida katika shughuli za kilimo.

Mfumo huo wa kidijitali unawapatia wakulima taarifa muhimu ikiwamo aina ya udongo, kiwango cha unyevunyevu, tindikali ya udongo, mazao yanayofaa kulimwa, mahali pa kupata pembejeo bora pamoja na masoko ya uhakika ya kuuza mazao yao.

Akizungumza kwenye Banda la Veta jana Jumatano Julai mosi 2026 katika Maonyesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DiTF) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, mmoja wa wabunifu wa mfumo huo, mwanafunzi Salum Mohamed amesema lengo la ubunifu huo ni kuwafanya wakulima wapate kwa urahisi maarifa ya kilimo cha kisasa.

“Ubunifu huu unawapatia wakulima taarifa za wakati halisi kuhusu hali ya udongo, utabiri wa hali ya hewa, uchaguzi wa mazao, masoko na usimamizi wa shughuli za shamba ili kuwasaidia kufanya kilimo chenye tija na faida zaidi,” amesema.

Ameeleza mfumo huo unatumia teknolojia ya Akili Unde kuchambua taarifa mbalimbali za kilimo na kutoa mapendekezo sahihi.

Akielezea namna unavyoweza kuongeza tija amesema mfumo huo huchambua sifa za udongo, ikiwamo kiwango cha unyevunyevu na tindikali, kabla ya kupendekeza mazao yanayofaa kulimwa katika eneo husika, hatua inayosaidia kuongeza mavuno na kupunguza hatari za uzalishaji.

Mbali na kusaidia uzalishaji wa mazao, mfumo huo pia unamwezesha mkulima kurekodi na kufuatilia mapato na matumizi ya shamba, kupata ushauri wa usimamizi wa biashara ya kilimo na kutambua masoko yanayoweza kununua mazao yake.

Ili kuhakikisha mfumo huo hauishii katika maonyesho, tayari wabunifu wa mfumo huo wameingia ushirikiano na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuunganisha huduma za utabiri wa hali ya hewa, jambo litakalowawezesha wakulima kupanga shughuli zao kwa kuzingatia taarifa sahihi za hali ya hewa.

“Mfumo huo unatarajiwa kuwasaidia zaidi wakulima wadogo, ambao ndio kundi kubwa la wazalishaji nchini, kwa kuwapa taarifa muhimu kwa wakati ambazo awali zilikuwa vigumu au ghali kuzipata,” amesema.

Ubunifu huo unakuja wakati ambao Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sekta ya kilimo imepewa nafasi ya kimkakati kama injini ya ukuaji wa uchumi jumuishi kutokana na mchango wake mkubwa katika ajira na ustawi wa wananchi.

Dira hiyo inalenga kuunganisha kilimo na sekta ya viwanda ili kuongeza thamani ya mazao kabla ya kuuzwa ndani na nje ya nchi, hatua inayotarajiwa kuongeza kipato cha wakulima, kuzalisha ajira na kuongeza mapato ya taifa.

Salim Sadick ambaye ni mmoja wa waliotembelea Sabasaba, ametaka teknolojia zinazolenga kuongeza mageuzi hasa kwenye sekta ya uzalishaji kupewa nafasi hasa kwenye upatikanaji wa ruzuku ili tija yake ionekane.

“Vitu kama hivi vingekuwa vinafanyiwa mapitio mapema na kupelekwa kwa wakulima ili vilete tija kwani ni wakati sasa wa kuachana na kilimo cha mazoea,” amesema.