Mizigo ya shaba kushushiwa bandari kavu Kwala

Malori ya mizigo yakiwa kwenye foleni ya kususha shaba katika eneo la Ubungo -Maziwa, jijini Dar es Salaam leo Februari 4, 2024. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Uamuzi huo umefikiwa kutokana na kuwapo kwa msongamano mrefu wa magari yanayosubiri kushusha mizigo hiyo katika bandari kavu ikiwemo iliyopo Ubungo-Maziwa, Dar es Salaam

Dar es Salaam. Kutokana na msongamano wa malori yanayosubiri kushusha shaba, bandari kavu ya Kwala sasa itatumika kushushia mizigo yote ya madini hayo, imeelezwa.

Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Mrisho Mrisho amesema malori yote yatapeleka mzigo Kwala, ili kuondoa msongamano katika bandari kavu, ikiwamo ya Ubungo ambayo kwa sasa madereva wanalazimika kusubiri kwa takriban siku 10 kabla ya kushusha shaba.

Ismail Issa, dereva anayesubiri kushusha mzigo wa shaba Ubungo, amesema leo Februari 4, 2024 kuwa amefika eneo hilo tangu Januari 22, 2024 na bado anasubiri waliotangulie washushe kwanza.

"Hapa tunasubiriana, wenzako wakishusha wewe unasubiri kuna wakati kunajaa na ikitokea hivyo inabidi kusubiri mzigo upungue. Hapo ndiyo huwa tunasubiri muda mrefu zaidi," amesema Issa.

Manemba Osward, ameonyesha kukosa tumaini la kuondoka katika eneo hilo kwa kile anachoeleza, ndiyo kwanza amefika Februari 2, 2024.

"Wenzangu waliomaliza wiki hapa bado wapo hawajui wataondoka lini. Mimi ndiyo nimefika, sioni kama nitaondoka niponipo sana," amesema.

Kinachomuumiza Lucas Lucas, dereva mwingine aliyekwama katika msongamano huo ni kile anachoeleza, kusalia eneo hilo ni hasara kwake.

Hasara hiyo inatokana na ufafanuzi wake kuwa, bosi wake amegoma kumlipa posho tangu siku nne zilizopita, akimweleza hayupo nje ya mkoa au nchi.

"Amesema hawezi kunipa posho kwa sababu nipo Dar es Salaam na nyumbani ni hapahapa ningekuwa nje ya mkoa angenilipa.

"Si kwamba hataki mzee wa watu (bosi wake) ameishiwa, anapata hasara sana. Nipo hapa wiki ya pili leo, kila siku analipa ada ya kuchelewesha kontena, amenilipa posho na sasa amechoka," amesema.

Lucas hana cha kufanya zaidi ya kuendelea na kazi kwa kile anachoeleza, "ukiacha kazi wenzako wanasubiri kwa hamu, madereva ni wengi sana Kaka wanasubiri gari."

Wamiliki wa malori nao, wanaufananisha msongamano huo na mlango wa hasara kweye biashara, hasa wakitaja tozo la Dola 60 za Marekani (Sh150,000) kwa siku ya kuchelewesha kurudisha kasha.

Mussa Hassan, dereva wa lori aliyekwama katika eneo hilo amesema kuna hofu ya wizi wa shaba.

"Ukiibiwa mzigo tajiri hatakuelewa, hapa kuna walinzi, lakini hawatoshelezi kudhibiti uhalifu, Pwani huko tunasikia kuna wenzetu wameibiwa. Mtu anaogopa hata kutoka kwenda kula," amesema.

Kutokana na msongamano uliopo, Mrisho amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Februari 4, 2024 kwamba bandari hiyo imepanga kuwa na kituo kimoja cha kushusha mzigo wa shaba. Kituo hicho amesema ni bandari kavu ya Kwala iliyopo Kibaha mkoani Pwani.

Amesema tayari mazungumzo kati ya Bandari ya Dar es Salaam na wadau wa usafirishaji yanaendelea kufanyika kufanikisha hilo.

Mrisho amesema shaba ndiyo mzigo mkubwa unaosafirishwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam, na ndiyo maana uamuzi wa kuwa na eneo moja la kuhifadhi umefanyika.

“Mzigo mkubwa unaoingia katika Bandari ya Dar es Salaam kwa ajili ya kusafirishwa ni shaba na kwa sababu hiyo tumeona kuwe na eneo moja la kuhifadhia mizigo hiyo,” amesema bila kuweka wazi kiwango cha mzigo huo.

Hata hivyo, amesema kumekuwa na malalamiko ya kukwama kwa malori ya shaba Misugusugu mkoani Pwani, ndiyo maana uamuzi wa kupelekwa katika bandari kavu unapangwa kufanyika.

“Mizigo hiyo ya shaba itafikishwa Bandari ya Kwala kisha itasafirishwa kwa reli kutoka Kwala hadi Bandari ya Dar es Salaam, tayari kusafirishwa kwenda nje,” amesema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki Wadogo wa Malori Tanzania (Tamstoa), Chuki Shaaban amesema hatua hiyo itaponya donda ndugu lililokuwa likisumbua wakati wote.

Amesema kwa sasa malori yanakaa hadi siku 20 kusubiri kushusha mzigo kutokana na uhaba wa maeneo ya kuhifadhi shaba, jambo ambalo ni hasara kwa wasafirishaji.

Iwapo lori litakaa kwenye foleni kwa siku moja, amesema msafirishaji atagharimia malipo ya posho ya dereva na Dola 60 za Marekani kwa siku ada ya kuchelewesha kasha.

“Msongamano umekuwa ukisababisha hadi mizigo kuibwa. Wiki mbili zilizopita malori matatu yameibwa mzigo wa shaba,” amesema.

Amesema uamuzi wa kupeleka mzigo bandari kavu ya Kwala utapunguza msongamano na changamoto nyingine zinazowakabili wasafirishaji.